MABADILIKO makubwa ya muundo, utendaji kazi, sheria na kanuni ndani ya Jeshi la Polisi, yanakuja.
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Inspekta Jenerali, Said Mwema, amemweleza Rais Jakaya Kikwete kwamba mabadiliko hayo yameshaanza kutekelezwa.
Akitoa taarifa ya utendaji wa jeshi hilo kwa Rais Kikwete jana, IGP Mwema alisema mabadiliko hayo yatasaidia kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa jeshi hilo.
Rais Kikwete yuko katika ziara ya siku mbili kutembelea Wizara ya Usalama wa Raia na idara zilizo chini yake.
IGP Mwema alisema: “Tumeanza mchakato mzima wa kufanya mabadiliko ya Jeshi la Polisi kwa lengo la kuboresha kwa kuangalia upya muundo wake pamoja na sheria na kanuni kwa lengo la kuboresha utendaji wetu ili kuleta ufanisi zaidi ndani ya Jeshi,” alisema IGP Mwema.
Alisema mabadiliko hayo yamekwenda sambamba na uimarishaji wa Kitemgo cha Intelijensia ambako serikali imepata wataalamu kutoka Scotland Yard, Uingereza.
Wameanza kutoa mafunzo ya awamu ya kwanza kwa askari kutoka mikoa ya Arusha, Dar es Salaam na Zanzibar.
Kuhusu ujambazi, alisema hali ya ujambazi imepungua kwa asilimia zaidi ya 50, na kwamba mianya mingi imedhibitiwa.
“Kunzia kipindi cha mwaka 2005 hadi mwanzoni mwa mwaka huu, hali ya usalama ilionekana kuzorota kwa kiasi fulani.
“Tunakumbuka hali ya ujambazi wa kutumia silaha ilivyokuwa tishio, lakini mpaka sasa tumefanikiwa kupunguza tatizo hili,” alisema IGP Mwema.
Alisema hali hiyo ilisababisha wananchi kupoteza imani kwa jeshi hilo kwa madai kuwa jeshi hilo limeshindwa kukabiliana na vitendo vya uhalifu.
“Takwimu zinaonyesha katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu matukio 20,697 yaliripotiwa katika vituo vya polisi, ikilinganishwa na matukio 22,885 katika kipindi cha mwaka uliopita, hii inamaanisha ni sawa na pungufu ya asilimia 9.6,” alisema.
Alisema kutokana na juhudi mbalimbali zilizochukuliwa na Polisi kuanzia Machi mwaka huu, hali ya uhalifu imeweza kudhibitiwa kwa kiasi kikubwa.
Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya Aprili hadi Juni, mwaka huu matukio ya uhalifu 6,899 yaliripotiwa, ikilinganishwa na matukio 9,605 ambayo ni sawa asilimia 28.1 mwaka uliopita.
“Mafanikio hayo yametokana na mikakati mizuri, ikiwamo doria ya kutumia pikipiki, magari na vifaa vya kisasa katika maeneo mbalimbali nchini,” alisema.
IGP Mwema alisema juhudi hizo pia zilisaidia kukamatwa kwa silaha 1,534, risasi 1,835 na majambazi sugu 24 waliokuwa wakihusika kwenye uporaji wa fedha katika benki na maduka ya fedha.
Kuhusu ajali za barabarani, IGP alisema takwimu zilizopo zinaonyesha kumekuwa na ongezeko kubwa la ajali, hali ambayo inapaswa kudhibitiwa haraka.
Kwa upande wa matatizo yanayolikabili jeshi hilo, IGP Mwema alisema kuna upungufu wa askari.
Alisema jeshi hilo limejiwekea malengo ya kuboresha uhusiano na jamii kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na wadau katika suala zima la usalama, ikiwa ni pamoja na kupunguza msongamano wa kesi na mahabusu.
Katika ziara hiyo, Rais Kikwete alitembelea Wizara ya Usalama wa Raia, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Ofisi ya Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Hospitali ya Jeshi hilo iliyopo kwenye Kambi ya Kilwa Road na Chuo Kikuu cha Maofisa wa Polisi Kilwa Road.
Rais Kikwete atahitimisha ziara yake leo kwa kuzungumza na askari wa jeshi hilo kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee.