RAIS Jakaya Kikwete, jana alitembelea ofisi kadhaa zilizo chini ya Wizara ya Usalama wa Raia mkoani Dar es Salaam, na kwenda hadi ofisini kwa Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Alfred Tibaigana.
Ziara ya Rais Kikwete jana ni mwendelezo wa azima yake ya kupita wizara na idara nyeti za serikali, kuwaeleza wahusika yale anayotaka wawafanyie Watanzania, na wakati huo huo, na yeye kusikia mipango waliyoiandaa na matatizo yanayowakabili.
Ziara yake ya jana ilianzia ofisi ya Waziri wa Usalama wa Raia, Bakari Mwapachu. Hapo alipewa taarifa ya jumla ya jeshi hilo.
Kutoka hapo alikwenda moja kwa moja ofisini kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, ambako alipewa taarifa ndefu ya mafanikio, matatizo na matarajio ya Jeshi la Polisi.
Miongoni mwa mambo makubwa aliyosema IGP Mwema, ni mchakato wa kulijenga upya jeshi hilo, kurekebisha baadhi ya sheria na kanuni; upungufu wa askari, upungufu wa nyumba na vitendea kazi na kadhalika.
Kutoka kwa Mwema, Rais Kikwete alikwenda moja kwa moja hadi ofisini kwa Tibaigana. Ofisi za Kamishna huyo zipo katika jengo la Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Dar es Salaam (Central).
Waandishi wa habari walizuiwa kuingia ndani. Aliteta na maofisa kadhaa wa jeshi hilo kwa muda usiopungua dakika 10.
Kabla na baada ya kumaliza mazungumzo, Kamishna Tibaigana alionekana kuwa mwenye furaha, lakini hakutaka kuweka bayana sababu zilizomfanya awe katika hali hiyo.
Rais Kikwete pia hakupata fursa ya kukutana na mahabusu ambao huwekwa kwenye sero maarufu kwa jina la ‘shimoni.’
Alipotoka hapo alikwenda hadi Kilwa Road. Akazuru hospitali ya Jeshi la Polisi. Alishuhudia vijumba vya kikoloni (vibushuti) ambavyo bado vinatumiwa na askari wazalendo kwa maisha yao ya kila siku wakiwa na familia zao.
Alipewa taarifa na mkuu wa kitengo cha ujenzi cha Jeshi la Polisi, SSP Sospeter Kondela. Alisema kuna nyumba 654 zinazotumiwa na askari, lakini nyumba 625 hazifai binadamu kuishi ndani yake.
Akasema kuna mpango wa kujenga maghorofa ya kisasa 60; kati ya hayo, maghorofa 10 yatajengwa Zanzibar. Yatagharimu sh bilioni 18. Huo utakuwa ukombozi wa polisi hao.
Baadaye Rais Kikwete alipata fursa ya kutembelea Chuo Kikuu cha Maofisa wa Polisi kilichopo Kurasini jirani na Kambi ya Kilwa Road.
Alitembelea mabweni yaliyofanyiwa ukarabati mkubwa, na kisha akakagua mtaro wa maji machafu na kuelezwa na uongozi wa chuo hicho kwamba mtaro huo ni kero kubwa. Rais aliahidi kusaidia kuondoa kero hiyo.
Leo Rais ataendelea na ziara yake. Baadaye atakuwa na mazungumzo na makamanda na askari wa jeshi hilo. Atazindua pia Chama cha Akiba na Mikopo (SACCOS) cha Wizara ya Usalama wa Raia.