BAADA ya kimya kirefu ambacho sikuweza kukivumilia, huku dunia ikiwacheka watu wangu na, kuudhalilisha utu wao wanaoulinganisha na ujinga na umaskini wetu, nimeamua kuzungumza japo kwa kutumia lugha ya kigeni ili wenzetu nao watambue na Watanzania wenzangu pia kuelewa wa kulingana na mawazo yao.
Nikiwa nimeketi kwenye eneo la wazi la hoteli mjini Brussels nikiangalia habari za kimataifa na kundi la wafanyabiashara kutoka Afrika, Mashariki ya Kati na Ulaya, picha ya habari ikionyesha Watanzania wakiandamana kupinga sinema iliyojishindia tuzo kibao ya Hubert Sauper, wakionekana kwenye kioo cha televisheni. Tukio hilo liliteka si tu hisia zangu bali na wenzangu ambao walikuwa wakifahamu utaifa wangu hususan kutokana na uzalendo nilio nao juu ya nchi yangu.
Baada ya habari hiyo kupita, majadiliano kuhusu filamu hiyo yenye utata yalizuka, sehemu kubwa ya watu niliokuwa nao hapo walishawahi kuiona filamu hiyo tangu ilipoanza kuonyeshwa barani Ulaya mwishoni mwa mwaka 2005.
Kutokana na mfumo wa maisha yao na walivyoichukulia sinema hiyo iliyo katika mfumo wa hadithi, wengi wao walionekana kushtushwa na kushangazwa na maandamano hayo, nini wanachogombea? Filamu hiyo imewaathiri vipi? Ni sehemu gani ya jamii wanatoka? Au wanawakilisha kundi gani? Hayo ni miongoni mwa maswali waliyokuwa wakijiuliza.
Wengine hawakuwa na muda wa kujiuliza zaidi ya kupuuza wakisema kwamba ujinga wao unatokana na umaskini uliowagubika.
Nilijisikia vibaya na jinsi walivyoichukulia hali hiyo, binafsi nilijua wageni hawa hawajui wasemalo na pia nilijua wengi wa waandamanaji hawa hawajui na hawatakuja kukijua kamwe kile kilichowafanya waandamane.
Si siri sehemu kubwa ya Watanzania waliomiminika mitaani jijini Mwanza kuipinga sinema hiyo hawakuwahi kuiona sinema yenyewe, na inaonekana hawakuwa wakijua kiini cha wao kuandamana. Walichosikia ni Rais Jakaya Kikwete akiilaani sinema hiyo wakati alipowahutubia wakazi wa Mwanza.
Jambo lisilokanushika ni kwamba maandamano hayo yalipangwa na mamlaka za Mwanza ili tu kuonyesha kwamba kilichoelezwa na sinema hiyo ni uzushi na uongo na kwamba wao hawakulala katika kumuunga mkono rais na kuondoa zana inayouchafua mkoa wanaouongoza.
Tofauti na waandamanaji hao, niliishaiona sinema hiyo kabla hata haijaanza kuwa gumzo.
Nilitazama kwa dhati na kuonyesha kuvutiwa na mtengenezaji wa sinema na mwandishi wa filamu hiyo.
Niliitazama sinema hiyo ‘Darwin’s Nightmare’ au Jinamizi la Darwin nikiwa peke yangu, niliiangalia tena nikiwa na marafiki zangu na kwa mara ya tatu nikiwa na Watanzania wenzangu.
Tulikuwa hatujakubaliana na sehemu nyingi za sinema hiyo, tulikuwa hatujakubaliana na tafsiri iliyotumika wala uhariri lakini sote tulikubaliana na kitu kimoja; filamu hiyo haikuwa na kitu kipya ambacho kingetufanya tuone ni kigeni nchini Tanzania au kuifanya ionekane kuwa ya uongo.
Kueleza mengi zaidi juu ya filamu hii ni kitu kisichowezekana kwa sababu ‘Darwin’s Nightmare’ ni picha ya dakika 107 na kuizungumzia kwa muhtasari bila ujuzi ndani yake wa tathmini na majadiliano, kutasababisha mjadala usio na mwisho. Na hilo si lengo langu, hapa nataka kujadili masuala yanayotukumbushia na sinema hiyo kwa namna ambayo Watanzania wa kawaida wataikubali.
Wengi wanapendelea kuiita picha hiyo yenye utata kwa jina la “Sinema ya Mapanki”, wakichukua neno mapanki ambalo ni Kiswahili lenye maana ya miiba au mifupa ya samaki iliyoachwa baada ya minofu kuondolewa kwa ajili ya kuiuza Ulaya na Asia.
Japokuwa neno mapanki limekuja kusimama kwa zaidi ya lilivyo, linawakilisha umaskini uliokithiri, kutojiweza, utawala mbovu, ufisadi na zaidi makombo.
Tukiwa kama taifa tunatakiwa tuchukue hatua mahsusi kushughulikia masuasla yanayotuhusu na kwa kuangalia sinema hii kwa jinsi ilivyo na si kitu kingine zaidi ya mapanki.
Tuiangalie picha hii na kuchukua mambo ambayo yanatugusa katika taifa hili. Tuwe waangalifu na watu ambao wanatufanya tupuuzie suala la mapanki kwa vile hawataki tulizungumzie kiukweli suala lililojificha.
Sinema hii inapaswa ionyeshwe kwenye televisheni ya taifa ili kila Mtanzania aweze kuiona na kujiunga katika mjadala, kumwezesha kila mtu aamue jinsi kwa mtazamo wake na jinsi maisha ya Mtanzania yanavyopaswa kuwa na jinsi ya kuboresha vyema usimamizi wa mapato na kuyatumia vyema kwa faida ya wananchi.
Tuache nafasi watu wazungumze kwa uhuru, Watanzania waamue wenyewe, tuwasikie wale watoto wa mitaani na makahaba walioshiriki kwenye sinema hiyo ili tuone nini wanachosema na kufikiri kuhusu sinema hiyo?
Ni muda mrefu hatukuwahi kusikia watu wakielezea mawazo yao kwa mapana na marefu waziwazi. Badala yake tumekuwa tukiona mlolongo wa mikutano ya waandishi wa habari inayoendeshwa na makundi fulani ikiwamo chama tawala, chama cha watengeneza filamu, ambacho chenyewe kilijua tangu awali kuwapo kwa filamu hiyo lakini kilikaa kimya kabla ya kuja kugutuka wakati mambo yalipokuwa hadharani kwa kuitisha mkutano na waandishi wa habari kikilaani filamu hiyo.
Wanasiasa na maprofesa nao walitoa tamko kali kuhusu filamu hiyo ambayo wengi wa Watanzania hawaijui kabisa zaidi ya kuisikia juu juu!
Mbaya zaidi kati ya yote yaliyokwishafanywa na kusemwa kuhusu filamu hiyo, hakuna hata moja lenye kuleta suluhisho au kutuambia nini limefaidisha.
Nashangaa na kujiuliza kama kweli wote waliojitokeza kujiingiza katika ushabiki wa kuikosoa filamu hiyo kwa namna tofauti wote waliwahi kuiona au kulikuwa na sababu ya kufanya hivyo?
Pamoja na uzalendo na uaminifu wangu kwa nchi yangu lakini mimi si kipofu. Niliwahi kuhusika katika mradi unaohusiana na filamu uliokuwa maalumu kwa ajili ya Taasisi ya National Geographic Society ya Marekani. Mradi huo ulikuwa na lengo la kutengeneza wasifu wa taifa, Tanzania, kwa kutangaza utalii, kuwavutia wawekezaji na kuvutia wahisani katika kuendeleza sekta hizo. Filamu hiyo ilitangazwa na kuonyeshwa na taasisi hiyo moja kwa moja na ilionyeshwa kwenye miji na majiji zaidi ya 300 nchini Marekani na Canada. Nilisikia fahari kama Mtanzania kuwa sehemu ya mradi huo kwa sababu ya msimamo wangu unaokosoa sana taswira na propaganda potofu zinazofanywa na vyombo vya habari vya Magharibi kuhusu Afrika.
Nilikuwa na furaha kwa sababu niliweza kuhadithia habari za taifa changa lenye matumaini na matarajio makubwa, nilifurahi kuwa sehemu ya kushiriki katika kuifurahia furaha na muhimu zaidi harakati za kimaendeleo zinazolenga taifa langu.
Pia nilifurahi kushiriki kwa sababu sikutia chumvi wala sukari au kupunguza kitu chochote eti kwa sababu tu mimi ni mzalendo.
Mara nyingi vyombo vya habari vya Magharibi vimekuwa vikitoa picha na taswira mbaya kwa Tanzania na Afrika hata pale tunapofanya mambo mazuri.
Sasa nikirudi kama mtengeneza filamu ninayeelezea athari hasi juu ya nini kinachotakiwa kujadiliwa katika picha hiyo.
Sekta ya uvuvi kwenye Ziwa Victoria, ambalo badala ya kuboresha maisha ya Watanzania linafanya kinyume, badala ya kuwainua kiuchumi wakazi wa eneo hilo, watu wanaolitegemea ziwa hilo katika maisha yao ya kila siku wameendelea kutumbukia katika dimbwi la umaskini wa kutupwa na hakuna dalili inayochukuliwa kurekebisha hali hii.
Mtengeneza filamu alitumia alama na maumbo mbalimbali ili kuvutia hadhira juu ya jina la filamu hiyo ‘Darwin’s Nightmare’.
Anaelezea mnyama mpya ambaye alibambikizwa kwenye Ziwa Victoria kama sehemu ya majaribio ya kisayansi. Mnyama huyo mkubwa, Sangara ambaye tangu azalishwe katika maji hayo amekuwa kama jinamizi kwa samaki wengine kwa kujaribu kutokomeza kwa wingi samaki wa asili ziwani hapo. Na hiyo ni moja ya chanzo cha kuwauza sangara nje ya nchi kwa wingi kulinganisha na kiasi kinachobakizwa.
Samaki huyu mpya baada ya kuchomekwa ziwani alizaliana kwa kasi, na minofu yake myeupe leo imekuwa ikiuzwa sana duniani kote. Imekadiriwa kwamba watu milioni mbili kutoka Ulaya na Asia hula sangara kila siku!
Na hilo ndilo lililomtuma mtengeneza filamu kuibatiza filamu hiyo jina hilo kutoka katika mawazo yaliyoibuliwa na Charles Darwin yanayohusiana na samaki mmoja wa ajabu.
Sauper alijaribu kuibadilisha hadithi hii na kuilinganisha na mnyama huyu wa Ziwa Victoria kwa nia ya kuifanya ionekane kama kioja.
Tunachokiona katika mioyo ya kina Darwin ni mfumo wao uliojipangilia vyema na hivyo kufanikisha malengo waliyokusudia.
Mbinu hizo zilishinda kwa kuwatia hatiani maadui wao au kuwamaliza kabisa. Washindi hapa ni watumiaji wa sangara wanaojidai kuwa na demokrasia wa Magharibi, na miongoni mwao ni marubani wa ndege za mizigo za Russia walioshiriki katika filamu hiyo waliokuwa wakionekana wakibeza ‘tunaibaka Afrika’ na hali hiyo pia ilihusisha meli za uvuvi kutoka Ulaya zinazoshusha shehena ya silaha kwa ajili ya kujipatia fedha na almasi na meli hizo hizo zinazobeba minofu ya samaki na matunda ambazo zinafurahia hali hii.
Kwa hali hii je, nini kitakachobaki Afrika? Nani aliyepoteza?
Filamu hii ingeweza kutengenezwa katika nchi kadhaa za Afrika kwa kubadilisha eneo moja hadi jingine kutegemeana na hali halisi kwa mfano Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sierra Leone, ambako samaki pekee wanaweza kugeuka almasi, nchini Honduras, ndizi na Libya, Nigeria au Angola, mafuta ghafi. Tunajua mbinu haribifu zinazotumika siku hizi, tunatambua malengo yanayofanywa na wanaojiita wanademokrasia wa Magharibi, sasa kwanini hatuamki?