MWENYEKITI wa Baraza Kuu la Umoja wa Mahakama za Kiislamu (UIC) la Somalia , Sheikh Sharif Sheikh Ahmed, amezionya nchi za Uganda, Kenya na Ethiopia kutotuma askari nchini humo.
Sheikh Ahmed, ambaye anaongoza UIC alisema hayo wakati akihutubia maelfu ya waandamanaji kwenye mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu Jumanne.
Waandamanaji hao walikuwa wakipinga mpango wa kutuma askari wa kigeni nchini humo.
Sheikh Ahmed ameonya kwamba atapinga na kupigana vikali dhidi ya jeshi lolote la kigeni litakalokanyaga nchini humo.
Wakati wa maandamano hayo, ofisa mwandamizi wa UIC, Ahmed Qare, aliiambia redio binafsi ya HornAfrik Radio kwamba: “Maandamano hayalengi kupinga askari wa Ethiopia pekee bali wanachama wote wa IGAD, na nchi nyingine yoyote.
“Na nchi hizi Ethiopia, Kenya na Uganda ndizo zenye ajenda ya kudhoofisha kwa mara nyingine juhudi za amani nchini Somali, zikikanyaga nchini tutapambana nazo vikali.”
Waziri wa Ulinzi wa Uganda, Dk. Crispus Kiyonga, alikutana na wabunge wa Chama tawala cha NRM Agosti 28 kuwasilisha azimio la kutuma askari wa nchi hii nchini humo kabla ya kukubaliwa baadaye.
Hata hivyo, Televisheni ya Ethiopia, ETV Agosti 29 ilimkariri Waziri Mkuu wa nchi hiyo Meles Zenawi akisema kwamba si lazima kutuma askari nchini Somalia kwa sasa.”
Uganda imepanga kupeleka Somalia askari 3,500 kama sehemu ya jeshi la kulinda amani lenye lengo la kuleta amani na utulivu kwenye taifa hilo la Pembe ya Afrika.
Askari hao watatumwa chini ya mamlaka ya maendeleo ya eneo hilo (IGAD).
Somalia, iliyoparaganyika kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe, imekuwa bila serikali kamili tangu mwaka 1991 wakati kundi la wanamgambo wenye silaha walipoipindua serikali ya mkongwe, Jenerali Mohammed Siad Barre.
Marekani ilituma askari nchini Somalia mwaka 1992 ili kurudisha amani lakini mwaka 1993, wanamgambo wa Somalia waliua askari 18 wa nchi hiyo na kuulazimisha utawala wa Rais Clinton kuondoa askari.
Katika ripoti yake iliyotolewa Septemba 1, kwenye tovuti ya UIC, Qaadisiya.com, ilisema kwamba waziri mkuu wa serikali ya muda ya Somalia, Prof. Ali Muhammad Gedi, na baadhi ya maofisa wa jeshi la Uganda waliwasili katikati na kusini mwa Somalia hivi karibuni na walitembelea kambi ya kijeshi ya Deynuunay nje ya mji wa Baidoa Agosti 31.
MONITOR