WANAWAKE wafanyabiashara ya bidhaa za utalii katika eneo la Forodhani mjini Zanzibar, wameandamana hadi ofisi za mke wa Rais wa Zanzibar, Shadya Karume, wakipinga kuporwa mali zao kulikofanywa na Baraza la Manispaa.
Wafanyabiashara hao 25 walisema kwamba bidhaa zilizoibwa ni za thamani kubwa.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Zanzibar jana, walisema kwamba askari waliwavamia na kukamata bidhaa zao kwa madai ya kuendesha biashara eneo lisiloruhusiwa.
“Sisi tangu mwaka 1990 tumekuwa tukifanya biashara katika eneo la Forodhani na tunalipa kodi ya sh 15,000 kila mwezi, kwa nini tufukuzwe
na kuporwa bidhaa wakati pale ndipo tunapopatia maisha?” alihoji Tatu Ahmada.
Walisema kwamba kitendo hicho kinakwenda kinyume cha kauli ya serikali ya kuwataka kina mama wajiajiri ili waondokane na umaskini.
Walieleza kwamba baada ya kutokea tukio hilo waliamua kwenda kuonana na Mama Karume, lakini walikwama baada ya kuzuiwa na wasaidizi wake.
“Tulipofika ofisini kwake, wasaidizi wake wametwambia suala hilo halimhusu na kututaka tumtafute Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi ili aweze kulishughulikia,” alisema mmoja wa kina mama hao.
Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Zanzibar, Mabrouk Jabu, alithibitisha kukamatwa kwa kina mama hao, na alisema madai ya kuporwa mali zao, linahitaji uchunguzi.
Alisema Baraza la Manispaa Zanzibar linaendesha operesheni ya kuwaondoa wavamizi katika maeneo yasiyoruhusiwa kuendesha biashara.
Alieleza kwamba wafanyabiashara wote ambao wanaendesha biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa, watahamishiwa katika eneo jipya la Saatanei baada ya ujenzi wake kukamilika. Hakusema lini ujenzi huo utakamilika.
Tangu juzi, mji wa Zanzibar, askari wa Manispaa wamekuwa wakifukuzana na wafanyabiashara wadogo wadogo na kubomoa vibanda vyao. Miongoni mwa maeneo yaliyokwisha kufikiwa ni Mji Mkongwe na Michenzani.