Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mawaziri waanzisha vurugu
Mawaziri waanzisha vurugu
By Habari Tanzania | Published  09/8/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Na Mwandishi Wetu, Ulanga

MOTO uliowashwa na mawaziri wawili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kwa kushabikia vurugu kwenye migodi ya madini wilayani Ulanga, sasa umeanza ‘kutoa moshi mzito.’

Wahusika hao ni Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Dk. Juma Ngasongwa, ambaye pia ni Mbunge wa Ulanga Magharibi.

Mwingine ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Celina Kombani. Kombani ni Mbunge wa Ulanga Mashariki.

Dk. Ngasongwa, wiki kadhaa zilizopita, alitoa taarifa rasmi ya maandishi, akikiri wazi kuwaunga mkono wananchi wanaomfukuza mwekezaji mzalendo aliyepewa leseni halali kuchimba madini katika eneo la Ipanko.

Waziri huyo, kwa niaba ya mwenzake, alisema wamechukua uamuzi huo kutokana na ukweli kwamba ‘wanaofukuzwa’ kwenye ardhi yao ya asili, ni wapiga kura wao.

Kwa maneno yake, Dk. Ngasongwa alisema Kampuni ya Interstate, inayomilikiwa na Henry Nyiti, haipaswi kuwapo eneo hilo. Maneno hayo yamewapa jeuri wachimbaji wasio na leseni, ambao sasa wanataka kampuni hiyo iondoke.

Mgogoro huo umesababisha Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha, atume kamati ya uchunguzi, ikiongozwa na Kamishna, Paul Masanja.

Kamati hiyo ilitembelea eneo hilo wiki hii, lakini Dk. Ngasongwa na Kombani, hawakuonekana.

Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Dk. Rajabu Utengwe, anakabiliwa na mtihani mzito wa kusuluhisha mgogoro huo.

DC huyo ambaye ni mara yake ya kwanza kushika nafasi hiyo, aliiambia Tanzania Daima ofisini kwake kuwa Kamati ya Dk. Msabaha, imekiri kuwa Ulanga kuna mgogoro mkubwa wa madini unaohitaji kutatuliwa haraka.

Alisema kamati hiyo imebaini kuwa kuna matatizo ya aina mbili. Matatizo ya kwanza yapo chini ya uwezo wa ofisi yake, na sehemu ya pili inahitaji kutolewa uamuzi na wizara.

“Kamati imekiri kwamba kuna mgogoro wa madini Ulanga, na tumeiambia wizara itoe uamuzi wake haraka ndani ya siku mbili ili kuepusha uwezekano wa kutokea vurugu katika mgodi wa madini ya spino, yanayopatikana katika Kijiji cha Ipanko, nje kidogo ya mji wa Mahenge,” alisema.

Juzi, kutwa nzima, Kamishna wa Madini na ujumbe wake kutoka makao makuu ya Wizara ya Nishati na Madini, alikutana na pande mbili zinazogombana, yaani Kampuni ya Interstate na wachimbaji wadogo.

Serikali imeamua kuwasimamisha wachimbaji wadogo wasio na leseni kuendesha uchimbaji ndani ya eneo ambalo kampuni hiyo imepewa kisheria.

Katika kikao hicho cha usuluhisho, kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Ulanga, kiliwakutanisha pia na Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mkuu wa Usalama wa Wilaya ya Ulanga, Mkuu wa Polisi wa Mahenge na viongozi wa wachimba madiniwadogo wadogo.

Katika kikao hicho, wawakilishi wa wachimbaji hao wadogo wadogo wakiongozwa na Katibu wao, Martin Msakamba, walieleza walivyoanza kufanya kazi ya utafiti na hatimaye kuanza kuchimba madini hayo kabla ya Interstate kupewa leseni.

Wachimbaji wengi wadogo wadogo walibainika kuwa hawana leseni za kufanyia utafiti wala leseni za kuruhusu uchimbaji wa madini hayo.

Kwa upande wake, Nyiti alisema kampuni yake ilituma maombi ya leseni ya biashara hiyo ya madini Ulanga mwaka 2003 na kufanikiwa kupata leseni Mei 5, mwaka huu.

Alisema kutokana na uzoefu wa shughuli za madini alionao, Ulanga hakuna mgogoro, na kwamba kilichopo sasa ni uchochezi unaofanywa na baadhi ya watu.

Alisema kampuni yake mbali ya Ulanga, pia inafanya shughuli kama hizo Arusha, Manyara, Kigoma na Mbeya.

Kutokana na hali hiyo, Kamishna Masanja alisema tatizo lilopo katika mgogoro huo limetokana na baadhi ya wachimbaji wadogo hao kuvunja sheria.

Alisema sheria za madini zinatamka bayana kuwa mchimbaji haruhusiwi hata kuokota madini katika shamba lake bila kupata kibali, lakini wachimbaji wengi wa mjini Mahenge hawana leseni.

“Hapa kuna tatizo la kutoelewa sheria, au watu wanazielewa lakini kwa makusudi hawapendi kufuata sheria hizo. Kifungu cha sita cha sheria za madini kinasema kuwa ‘Madini ni mali ya serikali, si mali ya mwenye shamba’. Kama ni mali ya serikali huruhusiwi kutafuta, kuchimba wala kununua madini bila kibali cha serikali,” alisema.

Mara baada ya kikao hicho, Kamishna na wajumbe wote walitembelea eneo la mgogoro wa machimbo hayo huku wachimbaji wadogo wadogo wakiendelea kuchimba katika eneo la Interstate. Wanachimba mbele ya walinzi wa interstate.

Baada ya kulikagua eneo hilo, Kamishna aliwataka walinzi wa Interstate kubaki kama walivyo bila kufanya shughuli yoyote na kuwaacha wachimbaji wakiendelea kuchimba hadi wizara itakapotoa uamuzi.

Kikao hicho kililitawaliwa na hoja za jazba kutoka kwa wachimbaji wadogo na kama si busara za Kamishna huyo, kulikuwa na uwezekano mkubwa kuzuka vurugu.

Kukosekana kwa Dk. Ngasongwa, na Celina, ambaye wamekuwa wakishirikiana mambo muhimu ya kijamii, kulilalamikiwa na wachimbaji na viongozi wengine.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.