Na Seif Mangwangi, Arusha
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Kaskazini, imetupilia mbali maombi ya Mbunge wa Karatu (CHADEMA), Bw. Wilbrod Slaa, kutaka shauri la kupinga matokeo ya uchaguzi dhidi yake lililofunguliwa na wanachama watatu wa CCM wilayani Karatu, kufutwa.
Shauri hilo lililofunguliwa mahakamani hapo Desemba 20 mwaka jana na
wanachama watatu wa CCM kupinga ushindi wa Bw. Slaa dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Bw. Patrick Tsere, lilitupiliwa mbali Agosti 29 mwaka huu.
Katika shauri hilo lililofunguliwa na wanachama hao watatu, Bw. Joseph Haymu, Bw. Emmanuel Burra na Bw. Thomas Lulu wote wa Karatu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupinga matokeo yaliyomtangaza Dkt. Slaa kuwa mbunge waliiomba mahakama kubatilisha matokeo hayo kwa madai ya kukiukwa kwa taratibu za uchaguzi katika jimbo hilo.
Hata hivyo kwa mujibu wa mwanasheria wa wanachama hao watatu Bw. Edward Mwaluko wa kampuni ya uwakili ya Mwaluko and Advocates Company, baada ya kesi hiyo kufunguliwa, Dkt. Slaa aliiomba Mahakama kuongezwa katika kesi hiyo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Alisema mahakama ilikubaliana na maombi hayo hivyo Dkt. Slaa alijumuishwa kwenye kesi hiyo na wanachama hao waliomshitaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kupinga kuteuliwa Mbunge huyo,
walitakiwa kutoa sh. milioni tatu, ili kesi hiyo iweze kupangiwa terehe ya kusikilizwa kama ambavyo sheria ya kupinga matokeo ya uchaguzi inavyosema.
"Walalamikaji walilipa fedha hizo kisheria, lakini upande wa Dkt. Slaa
unaotetewa na Wakili Bw. Tundu Lisu, uliwasilisha maombi ya kufutwa kwa
kesi hiyo, wakidai kwamba walalamikaji hawakufuata sheria ya uchaguzi
ikiwamo kuiomba mahakama kupangiwa kiwango cha fedha ambacho
watapaswa kutoa," alisema Bw. Mwaluko, huku akionesha nakala ya
pingamizi la kesi hiyo.
Alisema hata hivyo, kifungu cha 111 cha Sheria ya Uchaguzi ya mwaka
1985 kinasema endapo taratibu za kufungua kesi zitafuatwa ikiwa ni pamoja na kulipa sh. milioni tano na kama kuna mtu anaongezwa kulipa milioni tatu hawezi kuomba tena apangiwe kiasi cha kulipa.
Katika hukumu hiyo (nakala tunayo), iliyotolewa na Jaji Edward
Rutakangwa kuhusu kufutwa kwa kesi hiyo, Jaji alisema wanachama wa CCM, walifuata taratibu zote katika kufungua kesi hiyo ya madai, bila kukiuka kanuni na kuwataka wanachama hao wa CCM, kupitia wakili wao Bw. Ezra Mwaluko, kurekebisha kidogo hati ya madai ndani ya siku kumi na kuiwasilisha mahakamani kwa ajili ya kupangiwa siku ya kuanza kusikilizwa kesi hiyo.
Pia katika hukumu hiyo ya pingamizi, Jaji Rutakangwa ambaye hivi
karibuni aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Rufaa alimtaka Dkt.
Slaa kulipa asilimia 60 ya gharama zote za pingamizi la kesi hiyo, baada ya walalamikaji kuandaa gharama walizotumia.