*Inahusu kuhamisha wananchi kutoka Ngorongoro
*Asema Waziri akizidi kung'ang'ania ataleta vita
Na Seif Mangwangi, Arusha
MBUNGE wa Ngorongoro, Bw. Telele ole Saning'o, amepinga kauli ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Anthony Diallo, ya kutaka wananchi waliohamia kwenye hifadhi ya Ngorongoro, kuhamishwa bila ya kutafutiwa eneo la kwenda.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Bw. Telele, alisema kuwa wananchi waliokuwa katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wanapaswa kutafutiwa maeneo ya kwenda na kwamba kuhamishwa bila kutafutiwa eneo la kwenda ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Alisema Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), ambamo yeye ni mjumbe, ilishapitisha kiasi cha sh. milioni 170 kwa ajili ya kuhamisha familia zilizopo kwenye eneo hilo, lakini Waziri Diallo hivi karibuni alipinga kutolewa kwa fedha hizo, kwa madai kwamba ni uharibifu wa fedha.
Alisema hatua ya Waziri Diallo kutaka wananchi hao kutotafutiwa eneo la kwenda, ni kuingilia kazi za Mamlaka ya Bodi yenye viongozi wake akiwamo Mwenyekiti wa Bodi, Bw. Pius Msekwa.
"Kauli ya Waziri Diallo si ya kiungwana kabisa, huwezi kuwahamisha watu usiwaoneshe eneo la kwenda, huko ni kuvunja haki za binadamu, kamwe sitokubaliana naye hata kama ni mjumbe wa Bodi, akitaka abatilishe kauli hiyo kwa kuwa ni ya kuchochea vita," alisema Bw.Telele.
Waziri Diallo akiwa kwenye ziara ya kutembelea hifadhi hiyo, aliitaka bodi ya NCAA kutotoa fedha kwa ajili ya kuhamisha familia zilizomo kwenye hifadhi hiyo.
Kwa mujibu wa Bw.Telele, Waziri Diallo aliwataka wananchi waliohamia katika hifadhi hiyo kuondoka na kwenda katika maeneo ambayo walitokea na kwamba Mamlaka hiyo haitagharimia hasara zitakazotokana na uhamaji
huo.
"Aliwataka wananchi waliohamia kwenye hifadhi hiyo, waende mahali wanapopajua na kwamba hifadhi haitawagharimia chochote, hata hivyo Bodi ilishatenga sh. milioni 170 kwa ajili ya kuhamisha wananchi hawa," alisema Bw.Telele.
Alisema Bodi hiyo ilishawatafutia eneo la kuhamishia familia hizo zipatazo 2,000 katika kijiji cha Oldonyosambu wilayani Ngorongoro na kwamba huduma muhimu kama vile maji, ujenzi wa shule na zahanati zilishatengewa fedha za ujenzi.
Bw. Telele alisema wananchi waliowengi katika hifadhi hiyo ni ambao wazazi wao walihamia katika eneo hilo miaka mingi iliyopita, hivyo hawana mahali pengine pa kwenda.
Alisema kauli ya Waziri Diallo inamaanisha kwamba wananchi hao wataondolewa kwa nguvu ya Dola, hali ambayo inaweza kuzua mgogoro
mkubwa kati ya Serikali na wananchi hao.
"Ni wazi, kwamba mgogoro mkubwa unaweza kutokea endapo askari atatumika kuwahamisha wananchi bila kuwaonesha eneo la kwenda, wengi wao ni ambao wazazi wao walihamia hivyo na wao kujikuta wanazaliwa hapo hapo," alisema Bw.Telele.