WAZIRI Mkuu Edward Lowassa amemaliza ziara nchini Thailand, na kwenda Vietnam kuanza ziara ya siku nne kwa mwaliko wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya nchi hiyo, Nguyen Tan Dung.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Ofisi ya Waziri Mkuu, ilisema Lowassa alitarajiwa kupokewa na kukagua gwaride la heshima katika Ikulu ya nchi hiyo, kabla ya kufanya mazungumzo na mwenyeji wake. Akiwa Hanoi, mji mkuu wa Vietnam, leo mchana amepangiwa kukutana na Mwenyekiti wa Bunge la Vietnam, Nguyen Phu Trong na jioni kukutana na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha Vietnam, Nong Duc Manh.
Kesho Jumatano, Lowassa atakutana na Chama cha Wafanyabiashara na Wenye Viwanda katika Chuo cha Sayansi ya Kilimo, wakati mchana amepangiwa kwenda Taasisi ya Kukuza Teknolojia ya Kilimo cha Kisasa na Uhifadhi wa Mazao ya Chuo Kikuu cha Vietnam.
Jioni hiyo ataondoka kwenda katika mji wa Ho Chi Minh, ulioko kusini mashariki mwa nchi hiyo. Huko amepangiwa kukutana na Jumuiya ya Wafanyabiashara, kutembelea mashamba ya kahawa na korosho na viwanda vya kusindika mazao hayo. Vile vile atazuru mradi wa ufugaji samaki na kuangalia kiwanda cha kusindika samaki.
Katika tukio jingine, Watanzania watano waishio Thailand wametoa hundi ya dola 3,500 za Marekani (sh milioni 4.55/-) ili kusaidia Mfuko wa Maafa ulioanzishwa na Rais Jakaya Kikwete Februari mwaka huu, kwa ajili ya kusaidia kukabili maafa ya njaa.
Watanzania hao waliofika kukutana na Waziri Mkuu katika hoteli ya Shangri-La jijini Bangkok juzi Jumapili, walisema wametoa mchango huo ili kusaidia juhudi za serikali kupunguza matatizo mbalimbali yanayowakabili wananchi.
Watanzania waliotoa mchango huo ni Dk. Kinanga Temba, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mahidol; Laurian Rwehumbiza, Mkurugenzi wa Kampuni ya Broadhurst (Pacific); Nicholas Kipangala, Mkurugenzi Mtendaji wa Assili Gems International; Lucy Kileo, mwalimu wa Kiingereza katika Shule ya Msingi ya Bangkok na Auckland Muhunzi ambaye hufanya biashara ya nguo na vifaa vya umeme kati ya Thailand na Tanzania.
Mwenyekiti wa kikundi cha Watanzania waishio Thailand, Dk. Temba alisema japo wako mbali, wana imani na jinsi serikali inavyojishughulisha katika kutatua matatizo ya wananchi wake. “Tutakabidhi hundi yetu baada ya siku mbili,” alisema.
Waziri Mkuu aliwashukuru wote kwa moyo waliouonyesha na kuwaomba waikabidhi hundi hiyo kwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk. Batilda Burian, ambaye anabaki Thailand kikazi kwa siku kadhaa