MFANYABIASHARA maarufu, John Timothy Nyasanga, anadaiwa kutaka kutapeli nyumba ya urithi aliyopanga.
Mfanyabiashara huyo aliyekuwa akimiliki mabasi ya Nyasanga Transport Co. Ltd, (NYATCO) yaliyokuwa yakifanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Lusaka, Zambia, amedaiwa kutaka kutwaa nyumba hiyo iliyopo eneo la Kurasini, Dar es Salaam.
Nyumba hiyo, mali ya John Celestine Msembelela, ambaye kwa sasa ni marehemu ni namba KUR/KUR/0197 na ipo Plot namba 8A, karibu na NASACO (Kampuni ya Taifa ya Wakala wa Meli) na anadaiwa kupangishwa tangu mwaka 1992.
Akizungumza na Tanzania Daima, msimamizi wa familia hiyo, Frank Msembelela, alisema anahisi mfanyabiashara huyo anataka kuwatapeli nyumba hiyo, kwa sababu wakati mgogoro wao kuhusu suala la nyumba ukiendelea, aliwahi kutamka kuwa hamtambui yeyote na kuwa yeye ndiye mwenye nyumba hiyo.
Msembelela alisema kwamba, mkataba wa Nyasanga kumaliza kupanga katika nyumba hiyo ambayo kwa kipindi hicho alikuwa akitozwa sh 70,000 kwa mwezi, uliisha tangu mwaka 2002 na baadaye alizungumza naye kijamaa akidhani angemsikiliza lakini hakufanya hivyo.
Frank alisema baada ya kipindi kirefu kupita, Machi 15 mwaka 2004 alimpa notisi Nyasanga kupitia wakili wake Wilson Ogunde, lakini alikaidi kuhama wala kulipa kodi.
Aliongeza kuwa, baada ya Nyasanga kukaidi amri hiyo, kwa kuwa yeye anaishi mbali na Kurasini (Tabata), alipata kutembelea katika nyumba ambayo alimpangisha Nyasanga na kukuta imebomolewa baadhi ya sehemu na kuanzisha ujenzi mwingine.
“Nilipoona hivyo nilikwenda Serikali ya Mtaa ya Kurasini kumshitaki na kumtaka asimamishe ujenzi huo na baadaye niliamua pia kwenda Kituo cha Polisi Kilwa Road kutoa taarifa. Nilipewa hati namba WR/RB/6004/2006, lakini sikuona mtu huyo kukamatwa wala kesi kupelekwa mahakamani,
“Mpelelezi wangu anaitwa Emmanuel, mimi na mwenzangu, Leons Msembelela, tumehangaika wiki tatu kufuatilia shauri hilo hapo polisi, lakini tunashangaa polisi wanatuuliza wamshitaki Nyasanga kwa mashitaka gani,” alisema Frank ambaye aliambatana na nduguye Leons.
Kwa mujibu wa Frank, pamoja na mambo mengine, mwaka huu alipokwenda Manispaa ya Temeke kulipia kodi ya majengo ambayo ni sh 30,000 kwa mwaka, alikuta jina la Nyasanga kama mwenye nyumba, wakati ukweli ni kwamba yeye ni mpangaji.
Alidai kwamba, alipowaeleza kuwa huyo si mwenye nyumba hiyo, wanaopokea fedha Manispaa ya Temeke, walimwelewa, wakachukua fedha zake na kumpa stakabadhi.
“Ingawa nililipia fedha hizo kwa ajili ya kodi ya majengo lakini nililitilia shaka suala hilo na kuhisi huenda kuna mchezo mchafu ulichezwa. Nilishangaa kwa namna gani mtu anaweza kulipia kodi ya majengo kwa jina lake wakati yeye si mmiliki wa nyumba au kiwanja.
“Baada ya mgogoro mzima kuhusiana na suala la Nyasanga, Aprili mwaka huu wana familia wenzangu ambao wanaishi Mtaa wa Mwongozo, Kata ya Makuburi, Kinondoni walinishitaki katika Baraza la Kata ya Makuburi kwa kudhani kuwa huenda kuna kitu ninachonufaika nacho kutoka kwa Nyasanga, niliitwa barazani nikaenda,” alisema.
Aliongeza kuwa baadaye alimwita Nyasanga katika kikao cha baraza kama shahidi, na katika majibu ya baraza hilo yenye kumbukumbu namba 54/BK/MWG/05, Frank alikiri kuingia mkataba na Nyasanga na kudai kuwa tangu mwaka 1997 hadi 2002 alipokea sh milioni 2.2 kwa makubaliano ya Nyasanga kulipa nyingine – sh milioni 2.2 Februari 1998 lakini hadi sasa hajalipa fedha hizo.
Baadaye, baraza hilo ambalo barua yake ilionyesha kutolewa na Mwenyekiti, Kassim Msumi, lilimwita Nyasanga shaurini kwa ufafanuzi zaidi, lakini badala ya kwenda Julai 29 mwaka jana, Nyasanga alituma barua ya uwakilishi barazani hapo, akikanusha kwamba yeye si mpangaji wa nyumba namba 8A bali anaishi katika nyumba yake namba KUR/KUR/0197.
Barua hiyo ilionyesha kuwa iliandikwa na Wakili W. Mchome, na ilikuwa na stakabadhi za malipo ya majengo yaliyokuwa na jina la John Timoth Nyasanga.
Kwa mujibu wa vielelezo vya baraza hilo, kutokana na baraza kutoridhishwa na nyaraka zilizowasilishwa na wakili wa Nyasanga, lilimwita Nyasanga na alipohudhuria kikaoni hapo Agosti 11 mwaka jana, alikanusha kuwa yeye si mpangaji na wala hakuwahi kuwa na mkataba wowote na yeyote wa nyumba namba 8A ila kwenye nyumba yake mwenyewe namba KUR/KUR/0197 iliyopo Kurasini.
Baadaye baraza lilizitaka pande zote, yaani ya Msembelela na Nyasanga kuwasilisha hati za umiliki halali wa nyumba Plot namba 8A inayozungumzwa na baada ya pande hizo kufanya hivyo, baraza lilibaini kuwa mmiliki halali wa nyumba hiyo ni hayati John Celestine Msembelela.
“Hiyo ni dhulumati, tunataka jamii ifahamu matendo ya mtu huyo…sisi tupo 18 tuliipangisha nyumba hiyo ili itusaidie kuendesha maisha yetu, lakini tunaona sasa tunaelekea kudhulumiwa,” alisema Leons.
Frank alisema kwamba, kwa sasa wameufikisha mgogoro huo Majembe Auction Mart na kuwa kinachosubiriwa sasa ni kumalizika kwa notisi ya mwezi mmoja iliyobandikwa tangu Agosti 16 mwaka huu anapoishi Nyasanga.
“Endapo akikaidi amri hiyo ya kuhama, Vijana wa Kazi, Majembe Auction Mart watafanya kazi yao kwa kumhamisha kwa nguvu,” alisema.
Tanzania Daima iliwasiliana na hatimaye kumuuliza Nyasanga mwenyewe kuhusu suala hilo. Alikiri kupanga katika nyumba hiyo, na pia kumtambua Frank Msembelela na baadhi ya ndugu zake. Alikiri pia kuitwa katika Baraza la Kata ya Makuburi.
Pamoja na mambo mengine, Nyasanga alidai kuwa alipopanga katika nyumba hiyo aliikuta ikiwa chakavu, hivyo ilimgharimu zaidi ya sh milioni 10 kuikarabati.
Alipoulizwa kuhusu tuhuma za kubadilisha jina la Msembelela na kuweka lake pamoja na suala la kulipia kodi ya majengo Manispaa ya Temeke wakati hakuwa mmiliki wa nyumba hiyo, Nyasanga alisema:
“Watu wa majengo walipita ninapoishi na kutokana na kufahamika kwangu waliandika jina langu na baadaye nilishangaa bili za majengo zikija kwa jina langu kutoka Temeke, nami bila kusita nilikwenda kulipia kodi Temeke.”
Hata hivyo Nyasanga alidai kuwa juzi (Jumapili) alikuwa na kikao na mama wa wana familia hao, yaani mamaye Frank na wenzake ili kujadili suala hilo.