Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Siasa  »  Kikwete na mikakati ya kupambana na rushwa nchini
Kikwete na mikakati ya kupambana na rushwa nchini
By Habari Tanzania | Published  03/13/2006 | Siasa | Rating:
*Asema rushwa inazorotesha demokrasia, *Aahidi kuwapa ushirikiano mkubwa PCB
RUSHWA ni tatizo kubwa nchini Tanzania na nchi nyingine Duniani, katika kuhakikisha tatizo hilo linapungua, Rais Kikwete ameahidi kuwa bega kwa bega na kuwapa ushirikiano Taasisi ya Kuzuia Rushwa (PCB) katika harakati za kupambana na maovu hayo katika jamii. Mwandishi Gladness Mboma anaelezea zaidi katika makala haya.

Hakuna asiyefahamu kuwa kila kitu ndani ya nchi hii ni rushwa, viongozi wetu wengi wameingia madarakani kwa rushwa, ukitaka kupata haki lazima utoe rushwa ukitaka kazi nzuri lazima utangulize rushwa mbele ili mradi mambo yamekuwa shagalabagala.

Pamoja na Rais Kikwete kutoa changamoto kubwa kwa PCB, kazi iliyoko mbele yao ni kubwa sana na inatakiwa kufanyika kwa umakini mkubwa.

Rais Kikwete katika hotuba yake ambayo aliisoma wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa PCB ambao ulifanyika mkoani Mbeya aliwaambia maofisa hao kuwa wao ndio kikosi cha dafrao katika mapambano hayo na ndio wataalam wa kuendesha vita dhidi ya rushwa kisayansi.

"Napenda kuona ni namna gani mmejipanga kwa mbinu na mkakati wa kuikabili rushwa kubwa na rushwa inayowakera wananchi vijijini , mitaani na maofisini,"anasema.

Akielezea tatizo la rushwa anasema kuwa lina historia ndefu kwenye jamii ulimwenguni kote na kwamba ilikuwepo tangu binadamu walipoanza kuwa na mamlaka na dhamana ya kiutawala na kiuongozi kwa binadamu wenzao.

"Sio tatizo la Tanzania pekee wala sio tatizo la Afrika pekee, rushwa ipo kwenye nchi zinazoendelea na zile zilizoendelea, ipo kwenye nchi za kidemokrasia na si za kidikteta,"anasema Rais Kikwete.

Rais Kikwete anasema chimbuko la rushwa ni tamaa ya baadhi ya watu waliopewa dhamana ya utumishi na uongozi wa umma kutumia mamlaka yao kwa manufaa yao binafsi.

Pia ni matokeo ya mmomonyoko wa maadili binafsi ya watu hao kiasi cha kuwafanya wasiogope na wala kujali kabisa kuvunja maadili ya kazi zao na imani ya umma kwao.

Vile vile anasema kuzidi kuenea kwa rushwa katika jamii ni ishara ya mapungufu katika uwezo wao wa kitaasisi kuzuia.

Pia ni ishara ya kushindwa kwa ushawishi wa kisiasa, kijamii na kidini kwa jamii ili ichukie, ikemee na iikatae rushwa na kwamba mafanikio katika vita hivyo yanategemea ushirikiano wa nguvu za kisheria na dola, ushawishi wa kijamii, dhamira ya kisiasa na uimara wa maadili binafsi na ya jamii.

"Rushwa ni kitu hatari sana kwa maendeleo ya taifa letu. Ni dhuluma kubwa kwa haki za jamii na kwa wakati huu tunapoelekeza nguvu zetu nyingi katika kuinua uchumi na kuondoa umasikini, rushwa ni kikwazo kikubwa sana,"anasema.

Anasema kisiasa hasa kwenye uchaguzi wa viongozi wenye mamlaka ya umma, rushwa inazorotesha ukuaji wa demokrasia, inawanyima wananchi haki yao ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa kwa kuifanya haki hiyo iwe ya watu wachache wenye uwezo wa kifedha.

Pia rushwa inafanya uongozi kuwa kitu kunachonunuliwa kama bidhaa hali inayopunguza uhalali wa mamlaka za uongozi na utawala kwa wanaoingia.

Anasema rushwa hiyo ikiachwa na kushamiri inapunguza imani ya wananchi kwa mfumo mzima wa demokrasia na kwamba kwenye vyombo vya haki rushwa inazorotesha utawala bora na utawala wa sheria, inahatarisha amani na utengano wa nchi kwa kuleta dhana kwamba haki inauzwa na haiwezi kupatikana kwa njia ya kawaida, hivyo hakuna budi kuipiga vita rushwa kwa nguvu zote.

Anasema rushwa ikikithiri inaweza kuwa hatari kwa usalama wa nchi, kwa kuwa rushwa ni jambo linalowakera wananchi linaweza kuwafanya wawachukie watumishi wa umma na Serikali yao hasa wanapokata tamaa kwa kushindwa kupata haki, huduma na usalama wao.

Anasisitiza kuwa wananchi wanaweza kupoteza imani kwa viongozi wao na Serikali yao na hivyo kuvuruga mshikamano na utulivu katika nchi. Ikifikia hatua hiyo rushwa inaweza kuwa tatizo la kisiasa na kiusalama.

Kwa kutambua ukweli huo na hatari zinazoweza kutokea hatuna budi basi tupambane na rushwa kwa nguvu zetu zote na uwezo wetu wote,"anasema.

Aliendelea kusema kuwa mapambano dhidi ya rushwa ni vita halali kabisa kwa jamii kupigana na kupata ushiriki. Athari za rushwa kwa uchumi ni kubwa kwani inapunguza kazi ya kuleta maendeleo kwa vile fedha zinakwenda mifukoni mwa watu badala ya kufanya shughuli iliyokusudiwa ya kuiletea jamii maendeleo.

Anasema, Serikali hupoteza mapato stahiki, miradi hutekelezwa chini ya kiwango na huduma zitolewazo kuwa za kiwango cha chini au hata kuwa duni kabisa na kwamba rushwa inaongeza gharama za kufanya biashara.

"Matokeo yake ni kwamba bei ya bidhaa kuwa kubwa isivyo stahili na mzigo hubebeshwa mwananchi. Gharama za kufanya biashara zikiongezeka kutokana na rushwa tunatengeneza uwanja wa ushindani wa kibiashara usio sawia tambarare kwa washindani wote.

Kampuni zilizo na washiriki kwenye Serikali na vyombo vya mamlaka ya umma hata kama hazina ufanisi ndizo zinazonufaika, kampuni ambazo hazina washirika au hazina uwezo wa kugharamia rushwa na mara nyingi hizi huwa ni zile ndogo zinashindwa kushindana kwa ukamilifu,"anasema.

Anasema kutokana na rushwa utendaji wa Serikali na shughuli za umma huyumba. Hadhi ya Serikali mbele ya wananchi hushuka hasa pale sheria na taratibu haziheshimiwi. Unapokuta taratibu za mipango miji, hifadhi ya mazingira, usalama barabarani na nyinginezo hazifuatwi, dhana hujengeka kuwa Serikali haiko makini katika usimamizi wa ubora wa huduma kwa wananchi.

"Kuna dhana potofu kwamba rushwa inarahisisha mambo kwa kuondoa ucheleweshaji. Dhana hii haina msingi kwa sababu wapokea rushwa hujibunia mikakati, sheria na taratibu ndefu za kuongeza ucheleweshaji ili kutengeneza mianya na mazingira zaidi ya kupata rushwa.

Na mara nyingi wanaoathirika na mbinu hizi za wapokea rushwa ni wale wanyonge wasio na uwezo wa kutoa rushwa,"anasema.

Anasema pamoja na kwamba PCB ina mipango na mikakati mizuri ya kupambana na rushwa, ukweli ni kwamba ili wafanikiwe, Serikali inapaswa kuchukua hatua za makusudi za kisera na kiutendaji zitakazoongezea nguvu juhudi za taasisi hiyo.

Anasisitiza kuwa kila kiongozi katika eneo lake awe ndiye kamanda wa vita hiyo pale alipo. Waziri afanye hivyo na Katibu Mkuu pia. Hali kadhalika Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Wakurugenzi na wengineo wote wafanya hivyo na mafanikio yatapatikana.

Rais Kikwete anasema moja ya aina ya rushwa yenye kero kubwa kwa wananchi wa kawaida ni ile ya kutakiwa kumlipa chochote mtumishi wa umma ndipo itolewe huduma.

"Kusema mkono mtu haulambwi ni dhuluma na inakera sana. Ni kweli kwamba kishawishi kikubwa cha rushwa hii inawezekana kuwa kipato kidogo kwa watumishi wa umma. Jawabu lake kwa kiasi kikubwa linawezekana kuwa ni kuongeza kipato cha watumishi wa umma,"anasema.

Anasema kuwa aliahidi kulishughulikia suala hilo ambapo amesema kuwa makusudio yake miezi michache ijayo ataunda tume ya kuangalia maslahi ya watumishi wa umma, lakini kama kwa watumishi wala rushwa imeshakuwa ni hulka ya kuomba na kupokea rushwa inawezekana kabisa kuwa hatua hizo hazitasaidia na huenda ndio kwanza wakapandisha dau.

Anasisiza kuwa ni lazima kubana mianya ya rushwa na kuzidisha mapambano na kwamba kwenye Serikali kuu na serikali za mitaa lazima ziongeze uwezo na ubora wa utoaji huduma na kuakikisha kuwa kuna haki na usawa kwenye upatikanaji wa huduma.

Alionya na kusema watu wanaofanya kinyume na hayo wasionewe haya na kwamba wakati mwingine rushwa inatokana na wananchi wenyewe kutokuzifahamu haki zao.

Anasema kuwa ni lazima PCB wawe wakali zaidi katika kupambana na rushwa na kwamba pasiwepo na kulegeza uzi na kwamba changamoto kubwa iliyoko mbele yao ni rushwa kubwa na rushwa nono.

Rais anasema kwa muda mrefu sasa PCB imekuwa ikilaumiwa kwa kushughulikia rushwa ndogondogo inayohusisha watumishi wa vyeo vya chini na kwamba mara nyingi uongozi wa PCB umekuwa ukijibu na kuelezea ugumu wa muda mrefu unaotakiwa kupata ushahidi wa rushwa kubwa kubwa.

"Maelezo kwamba rushwa ni rushwa tu hata kama ni ndogo na yale ya ugumu wa kupata ushahidi wa rushwa kubwa kubwa hayajaridhisha wananchi walio wengi. Watu wanataka kuona tatizo hilo linashughulikiwa ipasavyo kwani rushwa kubwa kubwa ndizo zinazodumaza maendeleo,"anasema Rais.

Anasema ili kubainisha mikataba hewa, PCB kwa kutumia ujuzi wao ni lazima ibaini mapema mikataba hiyo isiyokuwa na manufaa kwa Taifa na kuishauri Serikali ili ichukue hatua zinazostahili kabla fedha na mali havijapotea.

Anawasisitizi PCB kuwa wasisahau kuangalia pia michakato ya majadiliano, viwango vya utekelezaji muda wa utekelezaji, kuhusika au vinginevyo kwa mamlaka za udhibiti wa utekelezaji na hatua za kuchukua endapo masharti ya mikataba yatavunjwa.

"Ni jukumu lenu PCB kutumia ujuzi wenu kubaini mapema mikataba batili au ile isiyokuwa na manufaa kwa Taifa na kuishauri Serikali ili ichukue hatua zinazostahili kabla fedha hazijapotea kwani kinga ni bora kuliko tiba," anasema Rais Kikwete.

Anasema eneo la pili lenye tuhuma ya kuwa na mianya ya rushwa kubwa kubwa ni la ununuzi serikalini na kwamba anakiri kuwa sheria ya manunuzi na taratibu nzuri na rahisi za ununuzi zilizowekwa zimesaidia sana kupunguza ukubwa wa mwanya wa rushwa katika eneo hilo.

Hata hivyo anasema bado kuna maneno yahusuyo upendeleo mgawanyo usio sawa, kutokuwepo uwazi wa kutosha wala ushindani halisi kwa kuwa washindani wengine hupewa habari za viwango vya gharama mapema.

Hali kadhalika anasema kuna madai kuwa ununuzi hauzingatii gharama na ubora wa bidhaa na kwa ajili hiyo yapo madai kuwa wakati mwingine bidhaa zinapewa gharama za juu zaidi na kama gharama ni za kawaida basi baadhi ya bidhaa hazifikishwi kwa mnunuzi kwa maelewano baina ya wanunuzi na wauzaji.

Rais Kikwete anasema fedha nyingi za Serikali hupotea kupitia mwanya huo wa rushwa na kuwataka PCB kufuatilia taratibu za ununuzi serikalini ili kubaini na kuziba mianya ya rushwa katika eneo hilo.

"Nia yangu ni kutaka kuona kuona fedha kidogo tulizo nazo zinatumika kwa manufaa ya umma na watu walio wengi na siyo kuendeleza maslahi binafsi ya watu wachache,"anasema.

Eneo lingine analosema Rais Kikwete lifuatiliwe ni lile lenye matumizi ya udanganyifu katika miradi ya Taifa na hasa ile inayofadhiliwa na nchi za nje.

Pia anasema yapo malalamiko dhidi ya udanganyifu na matumizi mabaya ya fedha za miradi mikubwa inayofadhiliwa na wahisani ama peke yao au kwa ubia na Serikali.

"Mimi ninaamini Serikali inaweza kudhibiti matumizi ya fedha ili wananchi ambao ndio walengwa wanufaike, naomba mfuatilie madai ya kuwepo rushwa na udanganyifu katika taasisi husika na ichukue hatua zinazostahili zilizopo katika mamlaka yake kisheria na kwa yale ambayo yapo nje ya uwezo wenu toeni ushauri serikalini,"anasema.

Rais aliihakikishia taasisi hiyo kuwa atakuwa nao bega kwa bega na kuwapa kila aina ya ushirikiano katika harakati zao za kupambana na maovu ya rushwa katika jamii.

Anasema pamoja na juhudi zote za kupambana na rushwa, lakini bado kiwango cha rushwa ndogo ndogo kinapanda kwa kasi hasa katika Mahakama, Polisi, ardhi, huduma za afya na sehemu ya jamii.

"Rushwa ikikithiri inaweza kuwa hatari kwa usalama wa nchi kwa kuwa ni jambo linalowakera wananchi na kuwafanya wawachukie watumishi wa umma na Serikali yao hasa wanapokata tamaa kwa kushindwa kupata haki, huduma na usalama wao,"anasema Rais.

Anasema, kutokana na rushwa utendaji wa Serikali na shughuli za umma huyumba na hadhi ya Serikali mbele za wananchi hushuka hasa pale sheria na taratibu zinapokuwa haziheshimiwi.

Anasema serikali kuu na mitaa lazima ziongeze uwezo na ubora wa utoaji huduma na kuhakikisha kuwa kuna haki na usawa kwenye upatikanaji huduma.

Akizungumzia Rushwa katika shughuli za kisiasa anasema yameanza kujitokeza mawazo na hisi kuwa kunaanza kujengeka utamaduni kuwa uongozi unaweza kununuliwa kwa fedha.

"Matendo mengi ya wagombea, washabiki na wapambe yanaelekeza hivyo. Wasiwasi wangu ni kwamba tusipokuwa waangalifu nchi yetu inaweza kuwekwa rehani kwa watu wenye fedha za kununua uongozi.

Jambo hili linasumbua, nakubali kwamba fedha ni nyenzo mojawapo muhimu katika kufakikisha uchaguzi kwa kila chama na kwa kila mgombea. Lakini fedha kutumika kununua ushindi si halali,"anasema.

Anasema kuwa anachotaka kujenga ni taasisi hiyo kuelimisha umma namna ya kupambana na rushwa na mbinu muhimu ya kuzuia.

 

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by KASIGALA)
    Rating
    kamwe tena ni vigumu sana kukomesha rushwa katika serikali yetu endapo MAHAKAMA ITAKUWA CHINI YA VIONGOZI WA SERIKALI KWANI HATUTAWEZA KUTOKOMEZA BIASHARA HARAMU WAKATI SERIKALI YETU INAONGOZA BIASHARA HIZO JE?NANI HATAMUUKUMU MWENZAKE WAKATI SISI WOTE NDIO MCHEZO WETU.KWANZA KABISA YATUPASA KUTAMBUA KWAMBA MAHAKAMA YETU YA TANZANIA HAINA UWEZO WA KUMU HUKUMU KIONGOZI WA SERIKALI KWANI IPO CHINI YA SERIKKALI HIVYO NI VIGUMU KUITOKOMEZA RUSHWA
     
  • Comment #2 (Posted by juma)
    Rating
    Angalia kesi ya dito, Tanzania legislation is BIASED... maskini sheria haimlindi kabisa ingawa ndo anatakiwa kulindwa kabisa. tuko wapi?
     
  • Comment #3 (Posted by joseph)
    Rating
    rais anastahili kuchukua hatua za haraka ikiwa ni pamoja kuwasimamisha au kuwajibisha watuhumiwa walioko serikalini na taasisi ili pcb ifanye kazi yake ipasavyo hivi sasa pcb haiwezi kwakuwa watuhumiwa wako kazini na inawapa nafasi ya kuingilia kati upelelezi kwa nafsi walizonazo.
     
Submit Comment


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Is Tanzania a safe place to invest?
  4. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Linda Garner
  4. Nthelezi Nesaa
  5. Marshy Abdu
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.