BODI ya Wakurugenzi ya Chuo cha Uandishi wa Habari cha Time, Dar es Salaam, imesema inaunga mkono kauli ya serikali ya kuunda chombo kitakachoangalia ubora wa kazi za wandishi wa habari na vyombo wanavyofanyia kazi.
Akizungumuza katika hafla ya kuwakaribisha wanafunzi wapya chuoni hapo, mmoja wa wakurugenzi wa bodi hiyo, Maurice Maugo, alisema uamuzi huo utaleta ufanisi kwenye taaluma hiyo.
“Sisi tunaunga mkono suala hili kwani itafanya taaluma hii iwe na ubora unaotakiwa, tunakitaka chombo hicho kuwa makini katika kufanya ukaguzi na kwenye vyuo vinavyotoa taaluma hiyo.
“Tunataka watembelee vyuo vyote vidogo na vikubwa, lakini wasitoe hukumu ya kufanana kwa sababu vingine haviko kwenye ngazi ya vyuo vikuu, vikaguliwe kwa kiwango chao,” alisema Maugo.
Hata hivyo, aliitaka serikali kuweka mtaala mmoja kwenye vyuo vinavyotoa mafunzo ya taaluma hiyo ili kupata ubora wa wanataaluma hiyo.
“Ili kuepusha tofauti iliyopo kati ya chuo kimoja na kingine, serikali ikubali kutumia rasilimali zake kuhakikisha kuwa kinatunga mtihani wa aina moja katika vyuo vyote vya uandishi wa habari,” alisema.
Chuo hicho kilianzishwa mwaka 2000 na kinatoa elimu ya uandishi wa habari katika ngazi ya cheti na diploma.