WAKATI wananchi wa Zanzibar wakijiandaa kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, hofu kubwa imetanda kutokana na mfumuko wa bei za vyakula muhimu, ikiwemo mikate ya boflo.
Mfumuko huo wa bei umeanza kujitokeza mara baada ya kampuni zinazoingiza mafuta Zanzibar kutangaza bei mpya ya mafuta ikiwa ni mara ya pili katika kipindi cha mwezi mmoja.
Mkate mmoja wa boflo ambao hutumika kwa chakula cha asubuhi na usiku, umepanda bei kutoka sh 70 hadi sh 100 huku wauzaji wa mikate hiyo wakidai chanzo kikubwa ni kupanda bei unga wa ngano na mafuta ya kula.
Mbali na bidhaa hizo, pia maharage yamefikia kilo moja sh 1,100 pamoja na mchele wa Pakistan ambao sasa unauzwa sh 800 kwa kilo moja, mchele wa Mbeya sh 1,200 kilo moja wakati pato la mwananchi ni dola moja kwa siku.
Kupanda kwa bei ya mafuta pia kutaathiri sekta ya usafirishaji wa mazao ya kilimo kama vile ndizi na mihogo kwa vile hivi sasa nauli za magari zimepanda na kufikia sh 1,500 kati ya mji na vijijini ambapo kwenda na kurudi ni sh 3,000.
Awali, bei hizo zilikuwa kati ya sh 1,000 na 1,200 na kusababisha baadhi ya wananchi wanaokuja kupata huduma mjini mtu mmoja kuja kwa niaba ya watu wengine kununua mahitaji muhimu ikiwemo chumvi, mafuta ya taa na vyakula.
Uchunguzi zaidi umegundua kwamba tangu kupanda kwa bei za mafuta Zanzibar, baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakitembea kwa miguu kutokana na kukaa vituoni muda mrefu kutokana na tofauti zilizojitokeza kati yao na makondakta wa daladala.
Wakati makondakta wakisisitiza walipe sh 150, wanafunzi hao wanaendelea kutetea msimamo wa serikali uliotangazwa hivi karibuni na Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Adam Mwakanjuki kuwa nauli ya wanafunzi ni sh 100.
Hadi sasa kesi mbili zimefunguliwa mahakamani za makondakta kuwanyanyasa wanafunzi, ikiwemo kuwashusha katika maeneo tofauti na wanakokwenda kwa kukataa kulipa sh 150.
Abiria wanaosafiri njia ya Bububu na Mjini Unguja wameanza rasmi kutozwa nauli ya sh 300 badala ya 250 kama ilivyotangazwa na serikali.
“Sisi hatujaziwi mafuta na serikali, kama wewe unafuata bei za serikali, subiri gari zao zije zikubebe, lakini nauli ni sh 300,” alisema kondakta wa gari ya Bububu.
Baadhi ya wananchi wameshauri serikali katika kipindi hiki cha kuelekea mwezi Mtukufu wa Ramadhan kukutana na wafanyabiashara kujadili hali ya mfumuko wa bei za bidhaa muhimu na kuangalia uwezekano wa kushusha kiwango cha ushuru ili wananchi waweze kumudu mahitaji muhimu.
Hata hivyo, pamoja na bei ya mafuta kupanda, bado upatikanaji wa nishati hiyo umekuwa ukizorota kila siku tangu serikali kuvunja mkataba na Kampuni ya ECOTECH iliyokuwa na jukumu la kuingiza mafuta Zanzibar.
Katika hatua nyingine, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetangaza kujiondoa rasmi katika udhibiti wa bei za mafuta na kwamba sasa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa hiyo Zanzibar watauza kulingana na gharama walizozitumia.
Uamuzi huo umetolewa na serikali kupitia Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) siku moja tokea kampuni za mafuta kupandisha bei za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa.
Meneja wa Elimu kwa Walipa Kodi, Rashid Ali Juma alisema Wizara ya Fedha hivi sasa itasimamia ulipaji kodi na Idara ya Nishati itakagua viwango vya ubora wa mafuta yanayoingizwa katika soko la ndani.
Alisema kwamba hatua hiyo imechukuliwa baada ya waagizaji wa mafuta kuwa na kinyongo kuwa gharama wanazozitumia hazilingani na viwango vya bei kutokana na mabadiliko ya kupanda bei na thamani ya dola ya Marekani mara kwa mara katika soko la dunia.
“Serikali haitapanga tena viwango vya bei ya mafuta hili litakuwa jukumu la makampuni yenyewe, kazi yetu ni kudhibiti viwango vya ubora na kukusanya kodi,” alisema Juma.
Alieleza kuanzia sasa ni ruhusa kwa kampuni yoyote yenye uwezo kuingiza mafuta Zanzibar ambapo hadi sasa ni kampuni za GAPCO na Zanzibar Petroleum pekee zinazoingiza mafuta.
Bei za mafuta zimepanda wiki iliyopita ambapo lita moja ya petroli ni sh 1,350 kutoka sh 1,250, dizeli sh 1,310 kutoka sh 1,260 na mafuta ya taa sh 980 kwa lita kutoka sh 900.