MTANZANIA mwenzangu,
Leo nina mada ngumu kidogo. Mara nyingi nimejiepusha na mijadala ya namna hii.
Lakini hilo halina maana kwamba sisikii wala sielewi kinachoendelea juu ya mada yangu ya leo. Udini.
Mojawapo ya mambo ambayo sisi kama Watanzania, hususan tunapokuwa nje ya nchi, hatuishi kujivunia nayo ni suala la kutobaguana kwa kutumia dini wala kabila.
Ilifikia mahali ikawa kama ni kosa la jinai kumuuliza mwenzako ni kabila gani au ni dini gani. Udini au ukabila si misingi ya taifa letu. Utanzania tuliuweka mbele zaidi.
Misingi hiyo iliwekwa na waasisi wa taifa letu, wote kwa pamoja, mababu na mabibi zetu.
Sifa nyingi zaidi humwendea hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwa sababu tupende au tusipende, alikuwa kiongozi wa nchi yetu, kiongozi wa kweli.
Mataifa ya nje yaliyowahi kutuheshimu, yamefanya hivyo kwa kuzingatia umoja wetu, hata kama umekuwa wa kinadharia zaidi kwenye nafsi zetu.
Tumeonekana wamoja hata kama baadhi yetu katika makundi mbalimbali tumeshindana kitabia. Kama Mtanzania, hapa Canada najawa na furaha sana ninapokutana na Mtanzania mwenzangu.
Kwa bahati nzuri lugha ya Kiswahili imechangia sana katika kudumisha au kupalilia umoja wetu. Hatukuchekeana kwa minajili ya dini wala kabila. Hili lisimaanishe kwamba mambo hayo hayajapewa kipaumbele na baadhi ya watu, la, ila cha msingi na muhimu sana ni kwamba hatukuwa tunayapa nafasi ya kutuelekeza jinsi gani tuhusiane na binadamu wenzetu, Watanzania wenzetu.
Hali ya kutokuwa na udini au ukabila imedumu kwa muda mrefu japokuwa vuguvugu za udini na hata ukabila zimekuwa zikichomoza na kupotea. Hii ni hali halisi ya ubinadamu popote pale. Hatufanani na si wote tunaopendana na kuheshimiana bila kujali imani na dini. Mambo nasikia yanabadilika, hofu inaanza kuingia na ndiyo maana siwezi tena kukaa kimya.
Rais wetu na makamu wake wa rais hivi sasa ni Waislamu. Kama ni Waislamu kwa majina tu au kiimani hasa, ni Mungu pekee anayeweza kujua hilo. Tanzania si nchi ya Kiislamu na wala falsafa yake haifungamani na dini yoyote.
Wakati mwingine huwa nahoji hata ule utaratibu wa kuapisha viongozi wetu kwa kutumia Korani au Biblia wakati serikali yenyewe haina dini yoyote. Unaapa kuilinda katiba ambayo ndani mwake inatamka wazi kwamba haina dini wala kabila!
Haina shaka, hiyo ni baadhi ya minyororo ya ukoloni na utumwa ambao baadhi yetu hawachoki kuikumbatia. Hii ni pamoja na viongozi wetu ambao masuala kama hayo wangeweza kuyabadili baada ya uhuru au hata sasa.
Katika siku za karibuni mijadala ya kuhoji mbinu anazozitumia rais wetu katika kuteua viongozi zimezidi kuwa gumzo.
Madai ni kwamba JK anatumia dini kama kigezo. Amechagua viongozi wengi Waislamu kuliko Wakristo na bado anaendelea kufanya hivyo.
Madai yanaendelea kwamba kila anapotaka kupoza mambo kidogo huchagua Mkristo ambaye si mshika dini. Mkristo wa jina tu. Yanayosemwa ni mengi sana na ndiyo maana nadhani wakati umefika tukumbushane sisi ni kina nani.
Dini na ukabila ni silaha ambazo zimetumiwa katika nchi nyingi sana duniani kuondoa mshikamano na umoja.
Utengano, vita, mifarakano na mengine mengi, yametokea kwa kutumia misingi ya dini.
Je, sisi kama Watanzania tumefikia mahali tumeanza kuonea wivu wenzetu wanaochinjana na kupigana vita zisizoisha kwa sababu ya imani zetu bila hata kuwa na ushahidi kwamba dini hii au ile itakupeleka peponi?
Hisia niliyonayo ni kwamba kuna watu wanatumika kueneza sumu hii ya udini.
Kuna mamluki ndani yake. Ni kina nani, wanataka nini? Maswali haya ni magumu ila majibu mepesi niliyonayo ni kwamba watu hao wanataka Tanzania iwe kama nchi nyingine nyingi. Hivi tumesahau kwamba dini hizi zote tunazoziruhusu ziongoze fikra zetu zililetwa na wakoloni ambao walizitumia vizuri sana kututawala?
Hatukumbuki kwamba dini zenyewe zina upungufu mwingi tu na kwamba wazee wetu wa zamani (waliokuwa na dini za asili) walipojaribu kuhoji walipewa majibu kwamba “ni dhambi kuhoji?” Leo hii ukinikataa mimi kwa sababu za kidini au kikabila huoni kwamba unakuwa umejifunga kwenye minyororo ya utumwa wa akili?
Yawezekana ni kweli kwamba Rais JK ameteua viongozi wengi Waislamu.
Sina takwimu rasmi. Lakini je, dini ya mtu ina uhusiano gani na utendaji wake?
Kama fulani amechaguliwa kwa dini yake na si uwezo wake wa kiutendaji kwa nini tusiseme, tusifungue kesi kutaka aondolewe pindi tunapoona kwamba kazi hawezi?
Lipi muhimu kwetu hivi sasa, dini au uchapaji kazi ili taifa letu nalo lisogee mbele? Je, anayeeneza hii sumu ya udini ni nani kama si adui yetu namba moja?
Mifano ya madhara ya mifarakano ya kidini ipo lukuki. Tuanze sasa kujifunza kutokana na makosa yao. Tusipofanya hivyo tunatafuta balaa na tutakuwa wajinga sana kuanza kutoana macho kwa sababu za dini. ‘We know better than that’ watanzania wenzangu.
Tunayo nchi ya kujenga. Hizi dini za mapokeo umeshazikubali, kuziruhusu ziturudishe nyuma kama zilivyorahisisha kutawaliwa kwetu na wakoloni, hata wakati huu tunapojua kwa undani wapi tulikosea, ni kosa ambalo hatuwezi kuwa na visingizio kwamba hatukujua, hatukuona likija. Jumapili njema.
jeffmsangi@sympatico.ca
www.harakati.blogspot.com