SALAMU kwenu waheshimiwa mabwana na mabibi.
Nianze barua yangu kwenu mlio mbali na upeo wa macho yangu kwa kuwatakia matashi mema. Kuwaombea baraka za Mola na kujiombea mimi na wengine wote walio chini yenu enyi watukufu.
Nikishawatakia yaliyo mema, naomba kwa mara nyingine tena nitete nanyi kwa unyenyekevu mkubwa, nikitambua kwamba mimi kiumbe mdogo sana, tena nina shaka ikiwa ninastahili hata kuthubutu kuwaamkia enyi waheshimiwa mabibi na mabwana. Hata hivyo, kwangu lengo langu ni kuwakumbusha yale mliyoahidi. Mniwie radhi kwa kuwa nahisi nitakuwa kero kwenu.
Waheshimiwa, unakumbuka sio miezi mingi sana imepita tangu mlipokuwa mkija kwetu? Mnakumbuka ule unyenyekevu wenu? Baadhi yenu walikuwa wakiwapa hata watoto wao wa kuzaa amkio la shikamoo. Mlikuwa wanyenyekevu kuliko malaika. Mlikuwa watu wa watu. Wengi wenu mkihudhuria hadi miba msiyokuwa na nasaba nayo. Naam tukawaamini, tukawapa mlichotaka.
Waheshimiwa mabibi na mabwana, bado mpo na sisi katika hali zote? Katika raha na furaha? Et waheshimiwa mbona nyakati zile mliweza kukaa nasi katika vilabu tukanywa wote mbege na rubisi? Tukagigida wote ulanzi na mnazi? Mkatueleza yaliyo katika uvungu wa mioyo yenu nasi tukawasikia? Nimeanza kuona dalili zisizo njema kwa baadhi yenu.
Tulikuwa tukilia wote, sasa mbona mmekubali haya yanayozidi kututesa yakapita bila ninyi kuweka pingamizi? Sitaweza kuyataja yote mliyoyaacha yakapita bila ninyi kuweka zuio. Waraka huu ni mfupi mno, nitataja machache tu na hiyo haina maana kwamba hayo ndiyo ya kipaumbele zaidi. La hasha, hayo ndiyo yaliyotosha kuenea hapa.
Nianze na hili la kisomo cha elimu ya juu. Waheshimiwa, wengi wenu mmesoma, lakini wengi wenu zaidi mmesoma bure kabisa wakati katika mpango madhubuti wa elimu ya bure iliyokuwa ikitolewa na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Nyerere. Sitaki kusema kwamba sasa bado watu wasome bure kama wakati ule. La hasha. Najua tumeshaagizwa tufuate sera ya kukopesha katika suala zima la elimu ya juu. Hata hivyo wengi wenu ninyi hamkusoma kwa mkopo. Mmesoma bure kabisa, tena wakati mwingine hata kusafirishwa bure na mkalipwa posho!
Kinachonifanya nilazimike kuandika kajiwaraka haka na kuwauliza ikiwa ninyi ndio tuliokuwa nanyi katika mitaa yetu mkitueleza namna ambavyo mnahitaji msaada wetu ili mje kuwa wakombozi wetu, ni namna ambavyo sikuona mkiyashupalia baadhi ya mambo likiwemo hili la mikopo. Mbona mmeamua kukaa kimya pale wakubwa wa kaya waliposema kwamba eti kaya yetu haina fedha za kutosha, hivyo mikopo itakuwa kwa wale waliopata daraja la kwanza upande wa wavulana na wale wa daraja la kwanza na la pili kwa wasichana.
Mbona hamkugoma mkasema sio? Ninyi si mpo kwa ajili yetu? Mngeuliza kwa sauti kubwa, wavulana watakaopata daraja la pili waende wapi? Mbona hamkuuliza wasichana wanaopata daraja la tatu waende wapi? Mbona hamkuuliza hao wanaoweka vigezo hivyo vigumu kama wao walijigharamia elimu yao au walikopeshwa? Kwa nini hamkuwaweka kitimoto? Waheshimiwa sisi tulikuwa tukiwatazama kwa matumaini kwamba mtatimiza ahadi yenu mtutetee kwa nguvu.
Kwamba baba na mama zenu hawana uwezo wa kugharamia elimu ya juu ya watoto wao na wala hawajaandaliwa kuweza kuingia katika mfumo mpya. Kwa nini hamkuwaambia wakuu wa kaya kwamba Roma haikujengwa siku moja? Kwamba watu wanahitaji kuandaliwa kuingia katika sera mpya? Unajua gharama ya kuingiza sera bila maandalizi? Ukitaka kujua chungulia tuvyoingia kichwa kichwa katika uhuria wa soko hadi tukajikuta kwenye uholela wa soko. Tukajikuta tumepitiliza na sasa tupo kwenye soko holela badala ya soko huria!
Kwa nini hamkuwahoji wakuu wetu wa kaya kwa nini tusiwe na fedha za kutosha kukopesha wanafunzi wote wenye sifa za kuingia elimu ya juu? Kwa nini hamkuuliza serikali inatumiaje vyanzo vyake vya mapato? Nilitamani niwe mmoja wenu niulize thamani ya dhahabu inayozalishwa nchini. Nilitamani nijue thamani ya tanzanite tunayozalisha. Ilikuwa hamu yangu nihoji almasi yetu, ni hoji biashara ya uwindaji, nihoji madini mengine kama ruby.
Kwa nini hamkuhoji awamu zilizopita zilipata wapi sarafu, sio za kuwakopesha bali za kuwasomesha bure? Yawezekana wakati huo tulikuwa na taifa tajiri zaidi? Yawezekana mliogopa kuuliza kwa kuwa mlijua kwamba jibu lingekuwa fedha tuliyonayo ni kidogo kuliko mahitaji. Sawa. Wakiwajibu hivyo mngeuliza swali jingine. Unapokuwa na fedha chache na matumizi mengi unafanya uamuzi gani? Wakuu wetu wa kaya ni watu werevu tena wenye ufahamu. Wangewapa jibu sahihi kwamba unapokuwa na fedha kidogo inabidi uzitumie kwa kuanzia na yale mahitaji muhimu na ya lazima kwanza.
Naam. Mngepata pa kuwabana hapo. Mngehoji ni kipi cha muhimu kwanza? Kuwekeza katika elimu ili vijana wetu waje kutengeneza ndege ikiwepo ya rais au kununua ndege ya rais na vijana wetu washindwe kukopesheka? Mngeuliza ni kipi bora zaidi kati ya kusomesha vijana wetu ili waje wawe wahandisi na watujengee kwa ujuzi wao wenyewe minara pacha ya benki kuu au kujenga minara pacha bila kujua wahandisi wa kesho watapatikanaje kwa kuwa hatuwezi kuwasomesha?
Ningekuwa mimi ningediriki kuuliza, jumla ya mikopo ya waheshimiwa wabunge ingetosha kusomesha wanafunzi wangapi? Najua wanahitaji usafiri, lakini kwani lazima usafiri huo uwe wa milioni arobaini na zaidi? Kwani kuna ubaya gani kila jimbo likawa na gari la ofisi ya bunge ambalo watarithishana wabunge wa jimbo hilo? Gari litanunuliwa tu kufuatana na mahitaji kama zilivyo ofisi nyingine. Mbunge naye si ana ofisi yake? Kama ambavyo anaondoka anaacha ofisini meza, viti na makaratasi, basi pia aache humo gari ili kuepuka gharama za kununua magari kila baada ya miaka mitano.
Waheshimiwa mabibi na mabwana, hamkuhoji hayo. Yawezekana hampo na sisi kwa hiyo hamjui kwamba hatuwezi kusomesha vijukuu vyetu elimu ya juu bila mikopo? Yawezekana mlisahahu kuwakumbusha wakubwa wa kaya yetu kwamba kama unadhani elimu ni ghali basi tujaribu ujinga? Mbona mngewaambia hivyo wangebadili mara moja kauli zao?
Mbona hamkuhoji mshahara wa mtumishi wa kada ya kawaida serikalini ni shilingi ngapi? Ale nini na atumie nini kumsomesha mwanae? Au yawezekana tumesomesha wasomi wa kutosha na sasa twahitaji kupumzika? Kwa nini hamkuwabana wakubwa ili wawatajie nchi yoyote ulimwenguni ambayo imefanikiwa kupiga kasi ya maendeleo bila kuwekeza kwanza katika elimu? Tuliwategemea mtusaidie katika hili, lakini hamkufanya vya kutosha. Ole wetu tutakaopata chini ya daraja la kwanza. Tutaishia kutegemea mvua za msimu.
kevinmakyao@hotmail.com
0784 265 072