Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kuendekeza sungusungu kunadhalilisha ulinzi
Kuendekeza sungusungu kunadhalilisha ulinzi
By Habari Tanzania | Published  09/3/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated

SITAKI kuambiwa kwenda nje ya nyumba yangu usiku kwa madai kwamba ninakwenda kulinda. Sitaki kabisa. Hasa katika mazingira ya sasa.

Kama huelewi ninachosema waulize waandishi wa habari wa mjini Iringa. Muulize Kamanda wa Polisi mkoani Iringa. Waulize alipo Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwembetogwa mjini humo.

Wote watakwambia hayupo. Yuko wapi? Amekufa. Yuko wapi? Utang’ang’ania. Amezikwa. Basi! Hatunaye Hashim Lugono aliyekuwa amefikisha umri wa miaka 53.

Lugono anasadikiwa kuuawa na ‘kundi la watu’ usiku alipokuwa akienda kwenye lindo. Mzee huyu siyo kolokoloni. Ni raia, mwenyekiti wa serikali ya mtaa anayeheshimika.

Kamanda wa Polisi mkoani anasema Lugono aliuawa kama saa 8:30 usiku, wiki hii, akiwa anakwenda kwenye lindo.

Kundi la watu linasadikiwa kumshambulia kabla hajafika walipokuwa wenzake waliokuwa kwenye ulinzi unaofahamika sana kama ‘sungusungu.’

Ulinzi wa sungusungu ni ulinzi unaofanywa na wananchi katika makundi. Wanaamshana usiku; wanachukua fimbo, rungu, panga, visu, mawe, nondo, mikuki na wengine hutoka na mbwa wao.

Wanaanza mzunguko – nyumba hadi nyumba; mtaa hadi mtaa wakipeana zamu za kulinda siku baada ya siku. Shabaha ya ulinzi huu ni ‘kukomesha uhalifu’ katika maeneo yao.

Ulinzi huu ulianzishwa rasmi katika miaka ya 1980. Kuna ulinzi mwingine wa aina hii ambao huitwa ‘wasalama.’ Huu uko katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga.

Baada ya wafugaji kuchoka kuibiwa ng’ombe na mifugo mingine; na baada ya kuona polisi ama walikuwa hawafiki vijijini au walikuwa wanazembea kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa, wananchi waliamua kuanzisha ulinzi wao wenyewe.

Kwa kiwango fulani wizi ulidhibitiwa katika maeneo ya wafugaji.

Lakini ulinzi huu uliandamana na ukamataji na utoaji hukumu nje ya mfumo wa utoaji haki – mahakama. Baadhi ya watu waliuawa, hata kwa kushukiwa tu.

Si tu kwamba utaratibu huu ulikuwa unakiuka mfumo wa utoaji haki, bali pia ulikuwa unaendesha ukatili usiomithilika dhidi ya watuhumiwa na hata ‘wezi wa kweli’ na ulikiuka haki za binadamu.

Utaratibu huu bado unaendelea katika sehemu mbalimbali za mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria. Ni kutokana na utaratibu huu, serikali ya wakati huo ilibuni utaratibu wa watu mijini na shamba kutoka usiku na ‘kujilinda’ – sungusungu.

Neno sungusungu lina maana ya wadudu aina ya mchwa ambao hukaa na ‘kufanya kazi’ kwa pamoja – kwa mfano kujenga vichuguu vikubwa na virefu, kuvamia mizoga na kuikata chembechembe na kuisafirisha hadi kwenye makazi yake. Hakika sungusungu wanafahamika kwa kuwa na umoja.

Ni umoja huo na nguvu hiyo ya wingi wa wananchi katika maeneo yao vilivyofanya serikali ione kwamba wanaweza kuchukua jukumu la kujilinda usiku.

Hili lilikuja baada ya kutokea wizi wa mara kwa mara katika miji na vijiji. Ndipo siasa zikavuma, “Sharti wananchi wajilinde wenyewe. Polisi peke yao hawawezi kutosha kulinda nchi nzima! Kila mwananchi na hasa kila mzalendo sharti ashiriki ulinzi wa nchi yake.” Siasa! Siasa!

Watawala hawakujiuliza kwa nini kuna wimbi la wizi na unyang’anyi. Hawakutafuta chanzo cha wimbi hili. Hawakutaka kutafiti au kufikiri. Waliona wananchi waingie mitaani wapambane na wezi na wanyang’anyi.

Wizi na unyang’anyi vilikomaa kadiri vyanzo vyake vilivyokua na kuongezeka, na kadiri vilivyobaki bila kudhibitiwa. Wizi wa sehemu moja ulinufaisha mafisadi sehemu nyingine.

Manufaa kutokana na wizi na unyang’anyi yalijenga mitandao na kuhusisha wenye uwezo wa kupata silaha. Sasa silaha zikaanza kutumika na kwa kasi ambayo ilikuwa haijawahi kushuhudiwa nchini.

Wezi wa sasa si wa kawaida na jina lao limebadilika. Wanaitwa majambazi. Wanatumia nguvu na wana silaha. Wengine wana silaha za kivita ambazo hupatikana katika makambi ya jeshi au stoo za silaha za vituo vikuu vya polisi.

Kama ilivyokuwa mwanzo, kwamba watawala hawakutafiti chanzo cha mlipuko wa ukwapuaji, wizi wa mfukoni, wizi wa kuvamia nyumba na hatimaye wizi wa kutumia nguvu na silaha kali, hawakuweza pia kutafiti uwezo wa kukabiliana na wimbi la uhalifu uliokomaa.

Hadi leo, katika mazingira ya wahalifu kutumia silaha za kivita katika uvamizi wa hapa na pale, bado watawala wanasisitiza kwamba wananchi watoke nje ya nyumba zao usiku na waende kulinda mitaani.

Bado watawala wanadiriki kuwaambia wananchi kwamba watoke majumbani mwao – wengine hawana nyumba kwa maana halisi bali vibanda vya ‘mbavu za mbwa’ – wakiwa wamebeba fimbo (za kuulia panya), rungu, panga, visu, mawe, nondo na mikuki ili wapambane na majambazi wanaotumia silaha za kisasa za kivita.

Wananchi wanaelewa kwamba hawana uwezo wa kukabiliana na majambazi wenye silaha za kisasa. Wanajua serikali haiwatakii mema. Wanatambua kwamba wanafanywa kuwa chambo. Wanaogopa kukataa. Wanajitosa gizani; hatarini.

Huko ndiko alikofia Hashim Lugono wa Iringa mjini. Bali si wa kwanza kufa katika hali hiyo. Majeruhi ni wengi pia; mijini na shamba ambako ujambazi umekithiri.

Sitaki ulinzi wa sungusungu ambao unamweka mwananchi mwenye fimbo ya kuulia panya, mbele ya jambazi lenye silaha kali za kivita na za kisasa. Huu si ulinzi. Huku ni kutoa wananchi ‘sadaka’ kwa silaha za maangamizi.

Katika hali ya kawaida, kila mtu ana haki ya kuchagua kazi anayopenda kufanya. Anaweza pia kutua katika kazi fulani, hata bila kuipenda au kuichagua, kutokana na mpangilio wa matukio kihistoria katika maisha yake.

Bali nchi hii ina watu waliopenda kazi ya ulinzi, wakaisomea, wakahitimu na wakaanza kuifanya. Bado wengine wengi wako vyuoni na wengine wanaoihusudu wangali wanatembelea vituo vya polisi.

Kuacha waliopenda na kuisomea kazi ya ulinzi walale na kukoroma wakati raia wako mitaani wanapambana na majambazi, ni dhambi isiyosameheka.

Sitaki wananchi wasio na ulinzi wafe wakilinda wenye madaraka, wenye silaha majumbani mwao na askari waliosomea kolokoloni. Sitaki!

nikitanaikata@yahoo.com


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.