KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Koffi Anan, alisema kwamba Syria itaweka jeshi la doria mpakani na kushirikiana na jeshi la Lebanon kuzuia uvushaji wa silaha kwa kundi la Hezbollah.
“Syria itaongeza jeshi lake la doria kwenye mpaka wa Lebanon na Syria na kuuunda jeshi la pamoja na Lebanon ikiwezekana,” Anan alisema baada ya kukutana na Rais wa Syria Bashar Assad mjini hapa juzi.
Assad hakutoa kauli yoyote hadharani baada ya mkutano huo, lakini Anan alizungumza na waandishi wa habari kwenye uwanja wa ndege mjini hapa kabla ya kuondoka kuelekea Qatar.
Azimio la UN lililomaliza mapigano kati ya Israel na Hezbollah linataka kuwekewa vikwazo kwa wapiganaji hao wa msituni, na Lebanon kulinda mipaka yake na sehemu nyingine za kuingilia.
Anan alisema Assad amemfahamisha kwamba Syria itachukua hatua madhubuti kutekeleza aya ya 15 ya azimio la UN namba 1701, linalozitaka nchi zisiuze au kugawa silaha kwa vikundi nchini Lebanon bila kibali cha Serikali ya Lebanon au walinda amani wa UN.
Pia Anan aliitaka Syria itumie ushawishi wake ili kuachiwa kwa askari watatu wa Israel, wawili wakiwa wametekwa na Hezbollah Julai 12 wakati wa mapigano ya mpakani yaliyosababisha vita na mmoja akiwa ametekwa na wanamgambo wanaohisiwa kuwa wa Hamas huko Gaza miezi michache iliyopita.
Assad alisema kwamba anaunga mkono kuachiwa kwao, lakini pia alitaka kuachiwa kwa wafungwa wa Syria wanaoshikiliwa Israel, Anan alisema.
Anan alitarajia kutembelea Iran jana ambako miongoni mwa mambo atakayolenga ni programu ya nyuklia ya nchi hiyo na suala la vita Mashariki ya Kati.
AP