KAMANDA wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Gregory Puka, amekuwa kituko na aibu kwa serikali ya awamu ya nne kutokana na hatua aliyoichukua kuwacharaza viboko abiria kama watoto wadogo.
Habari kutoka Bukoba kwa watu waliopigwa na kamanda huyo na wengine walioshuhudia unyanyasaji huo, zinasema amekuwa akifanya hivyo kwa abiria wanaokosa viti katika magari.
Anasimamisha gari, anawashusha abiria, anawalaza chini na kuwacharaza viboko. Anapochoka anawaamuru askari wa vyeo vya chini wanaokuwa naye, wanamsaidia ‘kazi.’
Katika tukio mojawapo la wiki hii, Puka aliwashusha abiria wote waliokuwa wamesimama ndani ya basi moja lililokuwa linaelekea Bukoba mjini kutoka Mutukula.
Lilipofika eneo la Kyaka, aliwacharaza viboko abiria akidai wanahatarisha maisha yao.
Mmoja wa watu waliocharazwa katika tukio hilo alisema hakumbuki hata idadi ya viboko alivyocharazwa.
Mmoja wa walioshuhudia tukio hilo alisema ilikuwa hali ya kusikitisha, na kwamba tangu nchi hii ipate uhuru, hajawahi kuona ofisa yeyote wa serikali akinyanyasa raia kwa kiwango kile.
Baadhi yao wanasema anapofanya hivyo amekuwa akitoa kauli kwamba watu wa Kagera wana jeuri, kwa hiyo anawashikisha adabu.
Lakini wanasisitiza kuwa huo ni uvunjaji wa haki za binadamu na sheria za nchi, ila wanashangaa uongozi wa serikali hauchukui hatua kumdhibiti.
Wanasema hata kama angekuwa anataka kudhibiti ujazaji abiria uliopindukia, hatua anayochukua haiendani na dhamana aliyonayo, na si wajibu wake. Kwamba ni vema angewakamata na kuwapeleka mbele ya vyombo vya sheria.
Alipohojiwa na gazeti kwa njia ya simu kutoka Bukoba, Kamanda Puka alikiri kuwateremsha abiria wanaozidi kwenye magari ya abiria, lakini hakukubali wala kukataa kwamba anawacharaza viboko.
“Zoezi la kushusha abiria wanaozidi kwenye magari ni la nchi nzima na si Kagera pekee… we huoni hizo ajali zinazotokea?” alisema Kamanda Puka halafu akazima simu yake. Alipotafutwa tena hakupatikana