IKICHEZA mbele ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete, na maelfu ya mashabiki wa soka waliofurika uwanjani, timu ya Tanzania, Taifa Stars, jana iliichapa Burkina Faso mabao 2-1 katika mchezo wa awali wa kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2008.
Katika mchezo huo, timu hizo zilikuwa sare hadi kipindi cha kwanza. Tanzania ilitangulia kupata bao katika dakika ya 29, baada ya Waburkina kujifunga kutokana na mshike mshike langoni mwao kwa kuzongwazongwa na washambuliaji, Gaudance Mwaikimba na Said Maulid ‘SMG’. Aliyejifunga ni Tall Mamadou wakati akirejesha mpira kwa kipa wake, Kabore Mohamod na mpira kujaa wavuni.
Burkina Faso, walisawazisha bao hilo katika dakika ya 39 kutokana na mpira wa adhabu kabla ya kumkuta Abdilaye Cisse aliyeihadaa ngome ya Stars na kupachika bao, hivyo kufanya timu hizo kutoshana nguvu katika dakika 45 za kwanza.
Kipindi cha pili, Burkina Faso, walionekana kutulia zaidi, lakini Stars bado waliweza kujipanga vema na kufanya mabadiliko ambayo yaliongeza uhai.
Mbrazil Marcio Maximo, yalisababisha timu hiyo kupata bao katika dakika ya 59 lililofungwa na Nizar Khalfan.
Khalfan ambaye ni zao la timu hiyo kutoka timu ya vijana wenye umri wa miaka 17 ya Tanzania, ‘Serengeti Boys’ alifunga bao hilo kwa shuti baada ya kupokea pasi ya kisigino au pasi ya kizungu kutoka kwa SMG.
Kabla ya bao hilo, Nizar aliyeingia kuchukua nafasi ya Renatus Njohole aliyeumia, mashabiki walionekana kutofurahia mabadiliko hayo.
Kuingia kwa bao hilo, kulipokewa kwa shangwe iliyomfanya Rais Kikwete kuinuka katika kiti na kushangilia.
Katika kuonyesha mshikamano wa kitaifa, mechi hiyo ilishuhudiwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wanasiasa.
Baadhi ya wanasiasa hao ni Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe; Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba; Mwenyekiti wa Chama cha Labour (TLP), Augustine Mrema na Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia.
Wakihojiwa baada ya mchezo kumalizika, Rais Kikwete, alisema yeye amefarijika na kusema, huu ni mwanzo wa safari ngumu, hivyo akawataka vijana wakaze mkwiji.
Baada ya mwamuzi, Alfred Ndinya kutoka Kenya kupuliza filimbi ya mwisho, Kikwete aliwaita wachezaji na makocha na kupeana mkono.
Kikwete, aliwapa mikono wachezaji wote na kuwanong’oneza mmoja baada ya mwingine.
Mbowe kwa upande wake alisema: “Imethibitika wazi kuwa penye nia pana njia. Hamasa iliyofanywa imezaa matunda na leo tumeshinda.”
Mbatia kwa upande wake, alisema: “Mpira wa leo (jana) umerejesha umoja wa kitaifa.”
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Profesa Juma Kapuya, yeye alisema: “Raha teeeeele. Ni furaha kubwa, tuendeleze kazi.”
Mbunge wa Ukonga na Naibu Waziri wa Miundombinu, Dk. Makongoro Mahanga, yeye alisema ushindi uliopatikana leo ni ishara kuwa safari ya kwenda Ghana imeanza.
Akizungumzia mechi hiyo, Maximo aliyeonekana kujawa na furaha kubwa, alisema ni mwanzo mzuri.
“Ni mwanzo mzuri, lakini bado tunahitaji kufanya bidii na marekebisho zaidi,” alisema kocha huyo kwa kifupi.
Stars jana iliwakilishwa na Ivo Mapunda, Shadrack Nsajigwa, Mecky Maxime, Salum Swedi, Victor Costa, Henry Joseph, Renatus Njohole/Nizar Khalfan, Athumani Idd, Abdi Kassim/Ulimboka Mwakingwe, Gaudance Mwaikimba/Mussa Hassan Mgosi na Said Maulid.
Burkina Faso: Kabore Mohamod, Joel Kamosi, Tall Mamadou, Haruna Bamogo, Paul, Coulibaly, Mahmoud Kere, Tansa Kabore/Georgies Termus, Tangui Bano, Alasane Quedraogo/Andulaziz Nikiteyama, Abdilaye Cisse/Yahya Kebe na Aristides Bance.
Katika matokeo mengine ya jana, Nigeria iliichapa Niger mabao 2-0, wakati Uganda iliishinda Lesotho mabao 3-0. Timu hizo zote ziko kundi la tatu.
Katika kundi la sita, Kenya ililala mabao 2-1 kwa Eritrea na katika kundi la 11, Bafana Bafana ya Afrika Kusini ililazimishwa sare ya bila kufungana na Congo (Brazaville).