LAMBA lamba ya asali ilimponza mlambaji, kwa sababu akiisha kuweka ulimi wake au kidole akipelekacho kwenye huo ulimiwe, hakomi.
Safari za kwenda mzingani huongezeka baada ya ile ya kwanza, hasa ikiwa nyuki ni ‘wakali’ ambao ukali wao ndio utamu wa asali waitoayo, ikawavuta watu elfu elfu kuiendea.
Kwa kasi hiyo hiyo, idadi ya safari za kidole kutoka ulimini kwenda mzingani au kombeni ilimopakuliwa, hurudufiwa kila uchao, ilimradi kutekeleza azma ya mtakaji – akombe!
Wamelamba wenye kujua, hapana ubaya mlaji anapoongeza ulaji, lakini pia hawakuchelewa kuongeza busara, kwamba ubaya ni kukomba mboga. Mmoja aliona mambo hayaendi, akamwaga ugali, mwenzake badala alambe mboga, akaimwaga pia, akasema heri wakose wote.
Safari za ilipo hazina hazitapungua, labda hazina yenyewe ipungue na kubaki isiyokidhi gharama, kwani shuruti faida ipindukie mara kadhaa gharama za safari, matumizi ya mabwanyenye, vijakazi, watumwa na wajinga waliwao. Ndiyo basi tena!
Na safari wazifunga, kusema wanaendea kutafuta watoto. Asubuhi mchana na jioni, ni kukwea midege yao kwenda hazina ilipokuwa imesitirika, isiwasitiri walioisitiri, bali wajanja waliojidai kuigundua, wakaamua kugagadua, kana kwamba wananasua ndege matopeni. Walioisitiri wamesafiri, Manani warehemu!
Kwa nini zisifungwe safari hizo, wakati hawajakinai chao? Waache vipi wakati vyao wameweka hifadhini kwao, ili ikitokea hamad hazina imeisha kwa wale waigawao ovyo, basi kibindoni wawe na chochote. Hamad kibindoni!
Na wamedhamiria kweli kweli kuhamisha, kwa sababu ndiyo njia ya kujiendeleza kuwa bora kuliko sie, wasiridhike na uzuri wao, lakini wasione hata huruma au aibu na ubaya wetu, hata wahangaike kutusafisha vidonda, kutuganga na kutupaka mafuta!
Labda kwa mgongo wa chupa watatupaka, na chupa wanazo nyingi, ni kusema kipande aina gani wakibetue kwetu. Kikitukata hakuna wa kujuta, itakuwa hadithi ya mtoto akililia wembe!
Wamerogwa watupendezeshe? Wamekinai uzuri wao hadi wautamani wetu – hivyo watuundie? Chao kimeendelea kuwa chao daima, chetu nacho wakivuta kwa nguvu kukifungamanisha nao. Hawaoni faida kutupendezesha, hawaoni ya nini kuingia gharama kwa kile wawezacho kupata kwa bure. Lakini bure huua, wamesahau, kama si leo, kesho!
Ndivyo iendavyo falsafa yao; ng’ang’ania chako kwa nguvu zote wakati wote, ili mradi kina sifa za uzuri na ubora, mng’aro na uzito, bila kusahau thamani na kukubalika! Ni vyao.
Hawakusahau katika falsafa hiyo ya kikwao, inayorithishwa kwa wachache wa kwetu wenye kuweza kuwafaidisha wao na kuwadanganya wengine wa kwetu; kwamba daima geuza cha mwenzio kuwa chako, kwa sababu ukicheza, utalala njaa kwa uvivu wa kuvuta.
Hawataki kulala njaa, hawapendi na hawakubali, wakati uwezo wa kufunga safari kuiendea hazina iliyositiriwa miaka na miaka wanao, ukubali wameupokea, ridhaa wameitoa – kilichobaki ni kulamba. Hawaoni hatari ya lambalamba, wala hawanayo akilini katika fikra – eti kwamba yaweza kuwavimbisha matumbo, yaje yapasuke.
Acha yaje yapasuke, wapumbavu wajisemea wenyewe vyumbani, na angani wakiwa safarini katika zoa zoa, kusanya kusanya na bandua bandua! Wakajiridhisha kwa kusema haitakuwa bure kazi yao, wakisha kulamba kwa ajili yao na vizazi vyao, kisha matumbo yakapasuka, walivyolamba vitatoka, watoto watakula, wenyewe wakiwa kufani!
Kumbe iwe isiwe, hawawezi kuacha chetu, kwa sababu chao hawakinai, wakati sisi twakinai chetu na chao, twabaki kujishughulisha kidogo, senti mbili zikiingia ni nyingi sana, mapumziko twaomba, tukikubaliwa twafurahia kwa mvinyo!
Wanabeba kwa kubeba, wasijali ghama za mafuta wala kulika kwa vyombo vyao, kupasua anga ni jadi yao, kwa sababu pori halina mwenyewe. Shamba la bibi wajukuu wataacha kuingia kuchuma matunda?
Ya nini wahangaike ‘hamu kuwaua’ wakati bibi yupo, shamba lipo, na walaji ndio wenyewe? Wahangaike vipi na mashamba yao, wakati wanahitaji kujiwekea akiba, na mkarimu kwa wajukuu yupo?
Wenyewe twawabeba, tumekinai chetu, na kwa namna yoyote ile iwayo, hatuonyeshi hata chembe kubabaikia chao, wakati mwingine kwa uvivu tu wa ‘kuacha vidole vitembee’, kwa uvivu wa kufungua kurasa, kuangaza na kurambaza, na kuthubutu kuvuka maji.
Tubabaike vipi wakati kwetu hakuna haraka? Twakimbilia wapi wakati kesho ipo? Tuchume nini wakati kaulimbiu ni kuponda mali kufa kwaja? Kusipokuja kufa twajifariji, kwamba mambo yatajipa.
Hili ndilo fungu letu, wajinga wajiambia, wasitake kuondoka huko, wasijibidishe kuwa kama hao watokao ng’ambo na kuja kukumbatia wetu na vyetu, wakitumia nguvu kugagadua ili wapate wakitakacho, wafunge safari, wapeleke kwao, watuletee majanga.
Majalalani ndiyo fungu letu, nani katudanganya? Yupo wapi aliyetuelekeza tushinde huko kuchukua vyuma chakavu, mifupa na vioo vilivyopasuka? Hata lini tutawaacha waendelee kula minofu na madini yenye thamani kuu kidunia?
Kwa kutokinai kwao, waendelea kupanda hadi kileleni, kwa kutobabaika kwetu wala kuona aibu kwa kudhalilishwa, twabakia jaani. Tumewadharau waliotueleza wenye kughani, kwamba kama si leo au kesho, tutaishia kula utumbo.
Ndiyo zetu, twajifariji! Mifupa yetu, twajidhili! Twajidai kufuata waliyonena wa kale, twafa! Twajimaliza kwa uvivu wa kufikiri, uvivu wa kuchagua na hivyo kuamua ovyo! Twajidai kuridhika na ‘uzito’ wa supu itokayo humo.
Supu nao waijua, lakini kwao pia mifupa wanayo. Labda waitumia kwa supu, na minofu kwa kile roho inachopenda. Je, si imenenwa ipe roho kitu inachopenda? Nani awezaye kuisaliti roho yake, licha ya udhaifu uliojaa katika miili? Supu!
Hata mawe yana supu, mbunifu mwingine aweza kutukumbusha! Labda akimaanisha yatumike yaliyobanduliwa vyenye thamani, na kubakishwa mahali petu, ikibidi tutainywa, Maulana tunusuru!
Viumbe wapo wa juu na chini, twaendelea kujifariji. Wa juu hufika mahali wakashuka, twajipa moyo. Wa chini wakapanda, twakenua. Hujafa hujaumbika, twajipumbaza, tukisahau stelingi hauawi, na akiuawa ndiyo mchezo umekwisha. Ndiyo basi tena!
barakamakyao@yahoo.com 0713589856