Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Uheshimiwa bila heshima?
Uheshimiwa bila heshima?
By Habari Tanzania | Published  09/2/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated

TUSIPOSHANGAA hili tutashangaa nini Yarabi? Twashuhudia vituko, halafu mwajidai mambo yote yako sawa? Hii ni laana naapa. Iwezekaneje vituko vinatokea kwetu halafu hakuna wa kushangaa zaidi ya Mzee wa Kujitoa? Nasema katika hili lazima nijitoe.

Kila mtu anajiita mheshimiwa sisi tubakie kimya tu? Katika hili mwataka niweke super glue mdomoni? Iwezekaneje tangu rais hadi mkuu wa kaya wote waitwe waheshimiwa halafu sisi tubakie bubu? Niambieni siku hizi ni nani haitwi mheshimiwa! Mwadhani Nyerere alikuwa bwege alipokataa kuitwa mheshimiwa akatumia neno ndugu? Mmeliwa katika hili nawaapia.

Kwenu hakuna anayemzidi mwingine siyo? Mwalimu wa madrasa aitwe mheshimiwa, sheikh aitwe mheshimiwa, paroko naye ni mheshimiwa, katekista anataka jina hilo hilo. Huu ni ugonjwa? Kwenye siasa nako wote wanataka kuitwa waheshimiwa. Kwamba chama kina wanachama elfu hiyo si hoja, hata mhazini wake anataka aitwe mheshimiwa. Niambieni kwa hakika leo nani hatangulizi neno mheshimiwa kabla ya jina lake? Mwafanya mzaha wa neno hili. Nijitoe haraka katika hili kabla hamjanitusi.

Si afadhali basi mngesubiri watu wawaite waheshimiwa? Mwajiita wenyewe wakati wa kujitambulisha? Nasema simo. Mtu mzima unayemtarajia awe na akili zake anasimama na kusema “Naitwa Mheshimiwa Ndumbaro Kanjenje!” Kwani ulipozaliwa uliitwa mheshimiwa? Si useme tu Ndumbaro Kanjenje usubiri sisi tukuite mheshimiwa kama unastahili? Ndivyo mlivyofunzwa kujitambulisha? Nauliza, ni paroko yupi alikubatiza hilo jina la mheshimiwa? Mie simo mwanakwetu!

Mbona vyeo vingine wala havinogi unapotanguliza neno mheshimiwa? Fikiria huyu anayejitambulisha kwa kusema: “Mimi ni mheshimiwa profesa Akilimali, mbunge!” Mbona wakati mwingine eneo ulilopo wala halina uhusiano na uprofesa wako? Mizaha mingine mbona inachefua Yarabi? Mwadhani itakuwaje kila mmoja wetu akitaja shughuli yake? Nianze mimi naitwa mheshimiwa Mzee wa Kujitoa, mwandishi wa safu ya Simo! Mwingine naye aseme “Mimi naitwa mheshimiwa Yolanda, mama wa nyumbani.” Tutafika kwa mtaji huu?

Cheo na kazi yako si ni huko ofisini? Waja baa kunywa halafu wataka tukusalimu kwa kutaja cheo chako? Mbona hayo ni maisha ya kitumwa? Baa tupo wanywaji wewe waleta mambo yako ya udaktari? Mambo mengine yanakera na kukereketa roho. Tunapohitaji daktari si twajua hospitali zilipo? Unafika baa na kusema mimi ni mheshimiwa daktari wa Tumbi? Nasema katika hili simo.

Mtu mzima unayeitwa baba huko kwenu unathubutu kujitambulisha baa kwa kusema mimi ni yule wakili maarufu wa mjini! Ebo! Nani ana haja ya kujua kazi yako sehemu zisizohusika? Kuna ‘kuboa’ gani kunakozidi huku kwa kutuletea mambo ya ofisini kwenye starehe zetu? Kama huna cha kuzungumza si ufunge mdomo? Najitoa katika hili.

Na nyie mnaojiita waheshimiwa, mbona matendo yenu hayana heshima? Acheni kutusanifu kwa vyeo vyenu. Wataka kuitwa mheshimiwa wakati madeni yamekukaba koo? Udaiwe elfu kumi au ishirini bado ung’ang’anie jina la mheshimiwa? Huu ni uchizi naapa. Mbona jina uheshimiwa linakwenda na matendo ya mtu? Wajifungia ndani kuogopa wanaokudai bado uitwe mheshimiwa? Uzezeta ni upi zaidi ya huu mwanangu?

Kwa akili yako, unaweza kuwa mheshimiwa kwa uhuni unaoufanya? Wadhani hatukuoni huko vichochoroni ukikojoa pasipo choo? Heshima gani ya kukojoa palipoandikwa “Usijisaidie hapa?” Kina baba wazima twawashuhudia mkichafua mazingira wakati kwenye vibarua vyenu na kila mahali mwataka muitwe waheshimiwa? Simo katika hili.

Tangu lini uheshimiwa ukaambatana na kuhamisha vifaa vya ofisini kupeleka nyumbani? Pini na karatasi za ofisini zafikaje kwenye nyumba yako mheshimiwa? Mwabisha hatuoni mnavyookoteza peni na majalada ya ofisini kupeleka kwenu? Wajidai mfadhili wa mikutano ya mtaani kwa ‘stationery’ ulizoiba ofisini? Bado kwa mtaji huu wataka uitwe mheshimiwa? Nasema simo, tena simo kabisa.

Twakushuhudia ukighushi stakabadhi kusudi ukadai fidia ofisini, halafu wagangamala kuitwa mheshimiwa? Huu ni ushenzi usio kifani. Aliyekwambia vitegemezi vyako vitasoma kwa kughushi risiti yu wapi? Mwadhani hatujui vitambi vyenu na mavazi yenu ni mazao ya wizi? Bisheni tu, lakini mimi siwezi kuwaita ninyi waheshimiwa.

Utakuwaje mheshimiwa wakati mwenyewe huna heshima? Utembee na vijukuu vyetu bado na wewe wajiweka katika orodha ya waheshimiwa? Mwabisha ninyi na akili zenu (nadhani si timamu) hamfanyi zinaa na vibinti ambavyo hata havijaacha ziwa? Bisheni. Kwani hizo mimba za wanafunzi wa shule za msingi zinatoka wapi? Nasema katika hili lazima nijitoe.

Sasa wanuna nini watu wanapoacha kukuita mheshimiwa? Kwani wapungukiwa na siku za kuishi usipoitwa hilo jina? Nimemshuhudia mtoa haki mmoja akimfokea raia, kwa sababu tu eti hakutanguliza neno ‘mheshimiwa’ kabla ya kutaja jina la mhusika. Wapagawa kwa vile tu hukupewa sifa ambayo hata kwa hakika huistahili? Nasema simo katika hili mzee mwenzenu.

Kwa mtaji huu si tuweke gredi za uheshimiwa kusudi tutofautiane? Mwaonaje kama tutakuwa na mheshimiwa, mheshimiwa sana na mheshimiwa zaidi tena sana? Lakini, nani ataamua nani awe katika gredi gani? Simo. Meneja wa klabu cha pombe anataka naye aitwe mheshimiwa. Katibu kata, diwani na mwenyekiti wa kitongoji wote wanakimbilia hilo jina. Neno mheshimiwa lina muujiza gani lakini? Wenye akili zenu sasa kataeni kuitwa hilo jina maana halina heshima yoyote. Niondoke katika hili upesi.

Mwajidai hamkumsikia yule mwanamama aliyekuwa akitoa sababu zake za kugombea ubunge? Kati ya sababu alizoziona za msingi ni pamoja na kutaka kuitwa mheshimiwa. Naapa hii ni taahira ya akili na mtindio wa ubongo. Mtu mzima anatiririsha machozi kwa huzuni, eti hajaitwa mheshimiwa! Nasema huu ni ushamba. Kutoitwa mheshimiwa kwakufanya uwe na majonzi kama aliyepata msiba? Nikisema huu ni upunguani sitakuwa nimekosea.

Mbona mwachezea neno uheshimiwa kama mnavyochezea majoho? Tangu wanafunzi wa chekechea hadi madaktari wa falsafa wote si wanavaa majoho siku hizi?

Mwahitaji operesheni dondola hata katika mambo haya? Bongo mwaiga kila kitu bila kujua maana yake. Mtoto hajui kusoma nyie mwamvisha joho? Hiyo ni sawa na anayeitwa mheshimiwa huku haoni aibu kuropoka matusi ya nguoni mbele ya watu. Uheshimiwa sasa umekosa hadhi. Nasema katika haya simo!

0784265072 kevinmakyao@hotmail.com


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.