Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Biashara ya samaki na jinamizi linalonyemelea maisha yetu
Biashara ya samaki na jinamizi linalonyemelea maisha yetu
By Habari Tanzania | Published  09/2/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated

SAMAKI wa Ziwa Victoria wanazidi kupungua, kutokana na uchafuzi wa mazingira, uvuvi usio endelevu na uchoyo wa watu kutaka kuhakikisha hawakomi kuwasomba hadi ziwa litakapokauka!

Taasisi ya Globefish iliyo chini ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), imesema athari zilizoletwa na filamu ya Darwin’s Nightmare katika masoko ya minofu ya sangara Ulaya, zilidunu kwa muda mfupi tu.

Kulingana na ripoti ya mwezi Agosti, iliyosainiwa na Helga Josupit; inayopatikana katika intaneti, soko la minofu ya sangara liliathiriwa haraka kiasi cha kutosha, mara baada ya filamu ya Darwin’s Nightmare kuonyeshwa katika televisheni, lakini athari hizo zilikoma baada ya kitambo kifupi.

Ripoti hiyo imesema hivi sasa sababu za kushuka kwa mauzo ya minofu ya sangara katika masoko ya Umoja wa Ulaya (EU) ni uzalishaji kupungua kulinganisha na miaka ya 2000, 2003 na 2004.

Katika nchi zote tatu za Afrika Mashariki; Kenya, Uganda na Tanzania, sangara walioagizwa Ulaya walipungua kutoka tani 56,000 mwaka 2004 hadi 52,800 mwaka jana; ingawa thamani ya minofu hiyo iliongezeka.

Ongezeko lilikuwa kutoka Euro milioni 192 hadi milioni 210 kutokana na matatizo katika usambazaji, yaliyosababisha ongezeko la Euro 3.43 kwa kilo mwaka juzi, hadi Euro 4.00 kwa kilo mwaka jana. Hata hivyo bei hiyo haijafikia rekodi ya Euro 5.00 kwa kilo; iliyofikiwa mwaka 2002, muda mfupi baada ya EU kuanza tena kuagiza samaki, baada ya kufungiwa.

Kulingana na FAO, kupungua kwa sangara waliopandikizwa Ziwa Victoria miaka ya sitini, kumeletwa na kupungua kwa kina cha maji ya Ziwa Victoria; na kwamba hali hiyo huenda ikawasababishia maelfu ya wafanyabiashara ya samaki na wavuvi kukosa kazi.

Hivi sasa, wavuvi hulazimika kuvua mbali, lakini mahitaji bado ni makubwa kulingana na kiasi kinachopatikana; hali inayowafanya wavuvi kugharimia fedha nyingi ili kumudu gharama za uendeshaji.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Kapteni Jaka Mwambi, alitoa tamko la chama kuiunga mkono kauli ya serikali kuilaani filamu hiyo iliyobatizwa jina la mapanki, kwamba ndiyo chanzo cha kupungua kwa ulaji wa minofu ya sangara katika nchi filamu hiyo ilikoonyeshwa.

Kauli hiyo ya CCM juu ya athari za Darwin’s Nightmare inatafsiriwa kuwa ya kisiasa zaidi, kwa kuwa imeacha kuainisha matatizo mengine yanayoikumba sekta ya samaki, hadi kusababisha mauzo kupungua, kutokana na samaki wa aina nyingi kutoweka Ziwa Victoria.

Hata hivyo, ripoti ya FAO inaonyesha kupingana na kauli hiyo ya CCM, ikionyesha dhahiri kuwa kushuka kwa mauzo ya samaki Ulaya sasa kunatokana na matatizo ya kimazingira, na wala si filamu ya Darwin’s Nightmare.

“Madhara iliyopata minofu ya sangara mwaka jana yalitokea haraka katika nchi filamu hiyo (documentary) ilikoonyeshwa katika televisheni, hali hiyo ikasababisha upungufu wa kutosha; lakini kwa bahati athari hizo zilidumu kwa muda mfupi,” imesema ripoti hiyo.

Iliongeza kwa kusema kwamba, juhudi zinafanywa kuhakikisha hali hiyo inarekebishwa, ikiwamo kutafuta mazingira ya haki ya biashara hiyo ya minofu ya sangara katika masoko ya Ulaya.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, pamoja na kupungua kwa samaki katika Ziwa Victoria, bado Tanzania ni nchi inayoongoza kwa mauzo ya sangara Ulaya. Kenya pia imeripotiwa mauzo yake kupungua, wakati Uganda mauzo yao yameongezeka kwa tani 5,000 na kuifanya nchi hiyo sasa ‘kuikalia kooni’ Tanzania kwa mauzo hayo ya sangara katika masoko ya Umoja wa Ulaya.

Mwaka jana Uganda iliuza tani 23,793 ambazo ni tani 87 tu nyuma ya Tanzania iliyouza minofu yenye uzito wa tani 23,880. Kenya mwaka jana iliuza tani 5,176. Hata hivyo, Uganda ilinufaika zaidi kwa kupata Euro milioni 101,318; wakati Tanzania ikipata Euro milioni 87,723. Kenya ilipata Euro milioni 19,087 mwaka jana kutokana na mauzo yake.

Nchi zinazoongoza kwa manunuzi ya sangara katika masoko ya Ulaya ni Hispania, Ufaransa na Italia. Hata hivyo, Uholanzi na Ubelgiji ndiyo kituo cha kwanza cha kusambazia sangara katika masoko ya Ulaya; wakati Ufaransa na Italia siku za karibuni zilianza kuagiza sangara moja kwa moja kutoka Afrika Mashariki.

Mbunge wa Ukerewe ambaye sasa ni Rais wa Bunge la Afrika, Mwenyekiti wa Chama cha Wavuvi (TAFU) na Mwenyekiti wa Wabunge wa Mkoa wa Mwanza, Gertrude Ibengwe Mongella, alipata kusema miaka michache iliyopita kwamba, kama hatua za dharura hazitachukuliwa, samaki watakwisha katika ziwa hili la pili kwa ukubwa duniani. Ni la kwanza Afrika lenye maji baridi.

Lina ukubwa wa eneo la kilometa za mraba 68,800. Kina chake ni wastani wa meta 40 chini, na juu meta 80; lina ujazo wa maji wa kilometa 2,760. Linachangiwa na nchi tatu; Tanzania inayomiliki kilometa za mraba 34,488 sawa na asilimia 51; Uganda kilomita 27,484 sawa na asilimia 43 na Kenya kilomita 6,828 sawa na asilimia sita.

Mongella alipata kusema katika vikao vya Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mwanza kuwa, kuna madai ya wavuvi kutoka nchi jirani kuvua upande wa Tanzania, kwa kutumia zana bora zaidi, zinazowawezesha ‘kuchota’ maliasili hii na kujipatia faida wakati watu wetu wakiendelea kuwa maskini!

Inakisiwa kuwa watu zaidi ya milioni 50 wanategemea ziwa hili kwa chakula chao, uchumi wao na hata maisha yao yote. Hivyo, kwamba taarifa za kupungua kwa kina cha maji cha ziwa hili; na kupungua kwa samaki kunakoletwa pia na uharibifu wa mazingira, ni kitisho kikubwa kwa uhai.

Mjadala unaoendelea kuhusu filamu ya mapanki, Darwin’s Nightmare, kwamba nchi za Kaskazini zimeanza kutumia ukoloni mamboleo kunyonya rasilimali za nchi za Kusini, hapa katika kuanza kupungua kwa samaki wetu, lazima kutafakari kwa kina.

Kwamba, kwa sababu ya umaskini, ujanja-ujanja, uroho, ujinga na kukurupukia soko huria katika utandawazi, tunauza mamilioni ya tani za samaki (chakula bora na chanzo cha uhai wetu) ili kupata vijisenti; kisha baadaye watakapokwisha kabisa, tujitoe kwa hiari kuwa makoloni ya kudumu, na watumwa wa nchi za Kaskazini ya dunia, ambao sasa hivi wanalinda sana na kuhifadhi rasilimali zao!

Kwamba, kwa kuuza sana rasilimali zetu, tena bila kusindikwa ili kuongeza thamani, au kwa kukabidhi kila tulichonacho kikiwa ghafi, kwa hao wageni, tunakubali kunyonywa sana, na hao hao tuliowahi kuwakataa miaka 40 tu iliyopita, na sasa wananyonya kwa mrija, bila jasho! Tusijivunie kuuza sana nje, tujiulize: Tunapata nini na wao wananufaikaje?

Hawalazimiki kutumia mitaji mikubwa kutunyonya! Mashirika makubwa ya kinyonyaji, kama Benki ya Dunia (WB), Fuko la Fedha la Kimataifa (IMF) na Shirika la Biashara la Kimataifa (WTO) yamekwisha kuandaa sera, masharti na mikataba ya kuchota kwa mara nyingine rasilimali zetu, zaidi ya ilivyokuwa enzi za ukoloni.

Safari hii, hawa wanawatumia viongozi wetu kuwapigia debe kusomba kila tulicho nacho…mwisho wa siku tutasalia jangwa! Maziwa, mito na mabwawa yatakauka! Misitu itafyekwa yote, ardhi yote yenye rutuba itauzwa; mbuga za wanyama zitauzwa, sangara waliokwisha kumeza samaki wengine wote zaidi ya aina 300 nao watakwisha ziwani…hata mapanki hayatakuwapo! Kutakuwa kilio na kusaga meno!

Naam, madini yote yatakuwa yameuzwa yakiwa ghafi; ili faida kwetu iwe kiasi kidogo sana. Lengo ni kutufanya tusijekuinuka na kuwa ‘super powers’ tukaanza kushindana nao kama Japan, China, India, Malaysia na mataifa mengine ambayo miaka 40 tu nyuma yalikuwa makoloni yao! Tutasaliwa na mashimo na sumu mbaya katika maziwa yetu yatakayokuwa yamekauka kiasi cha kutisha!

Kwa sababu ya uharibifu huu wa kutisha, tutaendelea kuathiriwa na sumu zinazosafiri kwa maji ya mvua kutoka migodini hadi katika vyanzo vya maji.

Bila shaka wataanza kuzaliwa watoto wasio na pua au mimba zilizotungiwa nje ya nyumba ya uzazi n.k! Tutamlaumu nani?

Tumeshaonywa juu ya hatari hii ya wawekezaji, hasa sekta ya samaki, kuachwa kuendelea kusomba samaki ziwani bila kuhakikiwa…samaki ni kama dhahabu, almasi, tanzanite, wanyamapori, misitu, rutuba, mito, maziwa na theluji ya milima: Hufika muda vyote hivi vikatoweka!

Kizazi kijacho tutakiambia nini? Kwamba tuliwahi kuwa na madini kama tanzanite yasiyopatikana popote ulimwenguni, samaki wengi kuliko ukimwengu wote, wanyamapori, vyura wa Kihansi, misitu, milima mirefu na kila kitu kizuri; lakini vikatoweka baada ya kuuzwa kama wazee wa Mwadui walivyopewa shanga za kuvaa kiunoni badala ya utajiri wa almasi?

Ni hayo hayo aliyosema mtunzi wa Darwin’s Nightmare, Hubert Sauper, kwamba rasilimali zetu zitakwenda Ulaya kwa ujira kidogo; sisi tutafanywa walinzi, vibarua: Tutalipwa kiduchu…Wahindi, Wazungu, na wageni wengine watalipwa fedha nyingi.

Sisi tutakanywa; “acheni wivu wa kijinga!” Watachota mali yote…watabeba hata mchanga na kupeleka Japan. Dada zetu watageuzwa malaya; na hata watoto wetu wa kiume watageuzwa ‘wake’ ili kujinusuru kwa njaa!

Naam, baadhi ya madini na rutuba vitahamia hata Mashariki ya Mbali. Kwa kuwa baadhi ya wanaharakati wataanza kupinga madhara haya ya utandawizi, ndugu zetu walioajiriwa kazi ya ulinzi wataendelea kuwapiga risasi, ili kutetea masilahi ya bwana zao.

Mwisho wa siku, tutabaki kusutana, pengine hata tutaanza kuumizana wakati wengine wakipiga hatua mbele ya maendeleo.

Ukitazama kiasi kinachopatikana sasa kama mrahaba wa rasilimali zetu, hakilingani na kile wanachobeba hawa wawekezaji – mawakala wa wakoloni mamboleo. Huu ubishi haupo hapa Tanzania.

Hata Jimbo la Ogoni, Nigeria, Waijaw hawajakoma kudai mapato zaidi ya mafuta yao yanayochimbwa na kuuzwa Ulaya, wakati wao hawana shule, zahanati, barabara na hata mafuta yenyewe!

Hali ya Niger Delta, haiko tofauti sana na Wilaya ya Kishapu, Shinyanga; ambako watu hawana maji ya kunywa au kunywesha mifugo, hawana nyumba za kuishi. Kwa kifupi wanaishi nyumba za mbavu za mbwa; mahali ambapo mwekezaji kaweka uzio katika utajiri wote wa almasi wenye neema ya peponi, kuwatenga wazawa na bustani ya Eden au na utajiri huo!

Kamwe huu si uchochezi. Watanzania tutafakari; almasi zikiisha, dhahabu zikatoweka, ziwa lenye sangara likakauka, mapanki yaliyoleta ubishi yakaisha, tutakula nini? Tutakwenda wapi? Ulaya siyo? Hatutakuwa watumwa hata kufa kwetu, bila uhuru? Lo, simanzi!

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu; 0754324074 na barua pepe; congesdaima@yahoo.com


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.