RAIS Jakaya Kikwete amesema utendaji wa viongozi wa serikali na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), utapimwa, pamoja na mambo mengine, kwa kutekeleza azima ya serikali ya kuendeleza kilimo na elimu nchini.
Rais Kikwete alisema hayo jana wakati akihutubia taifa kutoka mjini Dodoma.
Alisema viongozi wana wajibu wa kutekeleza kwa umakini mkubwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo imeainishwa mambo ya kuwafanyia Watanzania kwa kipindi cha miaka mitano.
“Katika Ilani ya uchaguzi ya CCM tumewaahidi Watanzania kwamba tutafanya jitihada kushirikiana nao kuleta mapinduzi ya kilimo yatakayokitoa kilimo na ufugaji kutoka hali duni na tija ndogo na kutupeleka kwenye kilimo na ufugaji wa kisasa,” alisema Rais Kikwete.
Alisema ili mapinduzi hayo yaweze kufikiwa, viongozi wanapaswa kuwa mstari wa mbele kutekeleza programu ya kuendeleza sekta ya kilimo iliyoanza mwaka huu na itakamilika katika kipindi cha miaka saba.
“Programu hii ina shabaha na madhumuni mbalimbali, inakadiriwa tutahitaji sh bilioni 2,492 kuitekeleza. Shabaha ya kwanza ni kuongeza matumizi ya maji katika kilimo.
“Lengo la programu ni kufikisha hekta 1,000,000 za mashamba yanayotumia maji mwishoni mwa programu, hivi sasa ni hekta 264,388 zinazomwagiliwa. Tutawekeza katika utengenezaji miundombinu itakayowezesha wakulima kutumia maji yaliyopo juu ya ardhi na yaliyopo chini ya ardhi,” alisema Rais Kikwete.
Alionya kwamba kilimo cha kutegemea mvua ni cha shaka kutokana na majira kuelekea kutobadilika.
Rais Kikwete alisema programu hiyo itahimiza matumizi ya mbegu bora kwa kuendeleza uzalishaji wake hapa nchini pamoja na kuagiza kutoka nje.
Alisema jambo jingine likalozingatiwa katika programu hiyo ni matumizi ya mbolea ili kuhakikisha ardhi ina rutuba stahiki kwa mazao.
“Matumizi ya mbolea katika kilimo chetu ni jambo tulilolipa umuhimu mkubwa katika programu hii, nawasihi Watanzania wenzagu tukubali kuongeza matumizi ya mbolea.
“Tunatumia kiasi kidogo sana cha mbolea ukilinganisha na nchi nyingine duniani, Watanzania tunatumia kilo nane za virutubisho vya ardhi kwa hekta, Uholanzi wanatumia kilo 578 kwa hekta….Malawi wanatumia kilo 27 kwa hekta na Afrika Kusini wanatumia kilo 63 kwa hekta.
“Kwa kutambua ukweli huo, tumeanza kuchukua hatua za kuongeza matumuzi ya mbolea nchini. Bajeti ya mwaka huu tumeongeza fedha za mbolea takriban mara tatu ukilinganisha na mwaka jana.
“Mwaka huu tumepanga kutumia sh bilioni 21 kununulia mbolea ya ruzuku ikilinganishwa na sh bilioni saba kwa mwaka jana. Lengo letu ni kuongeza mchango wa serikali mwaka hadi mwaka,” alisema Rais Kikwete.
Alisema mwaka jana hapakuwa na maandalizi mazuri ya upatikanaji wa dawa za kuulia wadudu wanaoharibu mazao. Zilitengwa sh bilioni moja. Aliahidi kurekebisha upungufu huo ili dawa zipatikane kwa uhakika na kwa bei nafuu.
Aliitaja shabaha nyingine ya programu hiyo kuwa ni kuboresha miundombinu na huduma nyingine muhimu zitakazosaidia kukuza kilimo.
“Programu inatilia mkazo kuimarisha barabara za vijijini kwa ajili ya usafirishaji wa pembejeo na mazao, pia imelenga kuimarisha huduma za maghala na hifadhi ya mazao ili kuzui upotevu wa mazao baada ya mavuno.
“Pia inasisitiza kuwapo kwa viwanda vinavyozalisha pembejeo za kilimo na mifugo, viwanda vinavyotumia mazao ya kilimo na mifugo kama malighafi
“Programu ya kuendeleza sekta ya kilimo nchini ni mkakati wa uhakika wa safari ya kuelekea kwenye neema, inalenga kuondoa vikwazo vilivyopo ili kilimo na ufugaji vikue na kuwa tija zaidi,” alisema Rais Kikwete.
Akizungumzia elimu ya sekondari, alisema wakuu wa wilaya na mikoa, na viongozi wengine wa serikali na CCM wanapaswa kuanza maandalizi ya kukabiliana na idadi kubwa ya watoto watakaojiunga na sekondari mwaka 2008.