Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Qaresi, Qorro wajibu tuhuma
Qaresi, Qorro wajibu tuhuma
By Habari Tanzania | Published  09/2/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu

WANASIASA wakongwe, Mateo Qaresi, na Patrick Qorro, ambao wanadaiwa kuingia mkataba wa kukodisha mashamba na kisha kulimbikiza madeni, wamejitokeza na kutoa ufafanuzi wa sakata zima.

Qaresi na Qorro, juzi walifika katika Ofisi za Tanzania Daima zilizopo Mtaa wa Mkwepu, Dar es Salaam, na kusema taarifa zilizotolewa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika, zililenga kupotosha ukweli wa mambo.

Viongozi hao walitoa taarifa zao kwa maandishi, nasi tunaona ni vema tukazitoa kama zilivyoandikwa.

Qaresi:

“Kabla mimi sijachukua uendeshaji wa shamba la kahawa la RIVACU (zamani lilikuwa la Mamlaka ya Kahawa Tanzania), lilikuwa linaendeshwa na chama hicho (RIVACU).

“RIVACU ilishindwa kuendesha shamba hili na likageuka pori lililohifadhi wanyamapori. RIVACU ilitafuta mwekezaji bila mafanikio. Mimi niliamua kuendesha shamba hili ili lisichukuliwe na serikali.

“Niliingia katika mkataba wa miaka 10 na RIVACU Oktoba 15, 1999. Baada ya miaka hiyo, ukodishaji unaweza kuongezwa kwa kipindi cha miaka mitano mitano. Katika mkataba kuna utaratibu wa kulipa pango. Malipo yalianza Desemba, 2000 kwa mujibu wa mkataba.

“Malipo yalikuwa sh 990,000 kwa miaka mitatu mfululizo. Malipo hayo yalipanda hadi sh 2,640,000 mwaka 2005. Malipo hufanyika baada ya mauzo ya malipo ya kahawa kila mwaka. Hadi tarehe ya leo (Agosti 30, 2006) deni la RIVACU ni sh 7,740,000.

“Siyo sahihi kusema kuwa RIVACU imeshindwa kununua mazao ya wananchi kwa sababu ya deni hilo. Pia si sahihi kuwa RIVACU ingeliweka rehani shamba hilo benki ili ipate mikopo.

“RIVACU ilishindwa kulihudumia shamba hilo likabadilika kuwa pori. Kama si mimi kulisafisha, ingeweka pori hilo rehani? Sikumbuki ni lini RIVACU ilinunua mazao ya wananchi.

“Mimi na Mrajis tulionana kuhusu suala la mkataba kutopelekwa kwa idhini ya Mkutano Mkuu wa RIVACU. Hii ni kazi iliyotakiwa kufanywa na Bodi ya RIVACU na msimamizi wa sheria (Ofisa Ushirika wa Mkoa).

“Haya hayanihusu mimi. Pia kazi ya kupeleka nakala kwa Mrajis ni shughuli za utekelezaji ya wahusika – RIVACU na Ofisa Ushirika Mkoa. Kama hawa walifanya makosa, lazima kuna utaratibu wa kisheria wa kuwaadhibu.”


Qorro:

“Tausi Investment Ltd ina mkataba baina yake na Chama cha Ushirika (RIVACU Ltd). Mkataba ni wa miaka 10. Mkataba ni wa kukodi shamba kwa ajili ya kulima ngano shairi, mahindi na mazao mengine ya muda mfupi.

“Tausi Investment Ltd inataka kutoa kauli yake kuhusu habari zilizochapishwa katika gazeti la Tanzania Daima la Agosti 30, 2006.

“Kwanza, Tausi Investment inapenda kueleza kwamba shamba ambalo imepewa kulima lina eneo la ekari 800; na si ekari 1,500. Umetokea ubishi kuhusu eneo la shamba na pande mbili zimekubaliana kuhakiki eneo la shamba.

“Kutokana na eneo hilo, na kwa mujibu wa vipengele vya mkataba, Tausi Investment ina deni la sh milioni 14 baina ya Tausi Investment na RIVACU Ltd. Mwezi huu tulikubaliana kuwa deni hilo litalipwa baada ya mavuno ambayo yanaendelea hivi sasa.

“…Kwanza mkataba baina ya Tausi Investment LTD na RIVACU ulisainiwa Septemba, 2001, wala si mwaka 2000.

Makosa ya mkataba kutofikishwa mbele ya Mkutano Mkuu ni ya halmashauri, menejimenti na Ofisa Ushirika wa Mkoa aliyekuwa amekuwapo Babati tangu mwaka 2003.

“Inashangaza kwamba hakuchukua hatua za kushauri RIVACU Ltd ilivyopasa.

Sisi Tausi Investment Ltd hatujaelezwa na RIVACU Ltd juu ya nia yake ya kuvunja mkataba, kama hiyo ndiyo nia yao, basi watueleze basi na sisi tujitetee mbele ya sheria ambako tunaamini haki inapatikana.”


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.