Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Majambazi JWTZ kukiona
Majambazi JWTZ kukiona
By Habari Tanzania | Published  09/2/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Happiness Katabazi

MNADHIMU Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali, Davis Mwamunyange, amewataka wanajeshi wasijihusishe na ujambazi na vitendo vingine viovu.

Luteni Jenerali Mwamunyange alitoa agizo hilo Dar es Salaam jana wakati wa maadhimisho ya ‘Siku ya Majeshi’. JWTZ jana ilitimiza miaka 42 tangu ilipozaliwa mwaka 1964, baada ya kuvunjwa jeshi la kikoloni la Tanganyika Rifles (TR).

Sherehe hizo zilifanyika katika viwanja vya Makao Makuu ya JWTZ, Upanga, Dar es Salaam.

Luteni Jenerali Mwamunyange, alisema kwa siku za karibuni, wanajeshi kadhaa wameripotiwa kuhusika na ujambazi na vitendo vya utovu wa nidhamu uraiani, jambo alilosema linatoa sifa mbaya kwa Jeshi.

“Vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti baadhi ya wanajeshi wanajihusisha na ujambazi na vitendo viovu…..nakiri kabisa, hii si sifa nzuri mbele ya raia ambao wametupa dhamana ya kuwalinda na mkumbuke ipo siku watahoji,” alisema.

Luteni Jenerali Mwamunyange ambaye jana ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuhutubia wanajeshi akiwa na wadhifa huo mpya, alisema kama ndani ya jeshi hilo bado kuna wanajeshi wanajihusisha na ujambazi, wafichuane ili sheria ichukue mkondo wake.

“Nasisitiza taarifa hizi za askari kujihusisha na ujambazi zimeibuka hivi karibuni tu, miaka ya nyuma taarifa kama hizi hazikuwapo na kwa kifupi hazipendezi kuzisikia, kwa kuwa zinachafua jeshi na wanajeshi wote ….. sasa nasema hivi, sisi wanajeshi wenyewe kwa wenyewe tuanze kufichuana, tena bila haya, kama kuna wanajeshi wapo ndani ya jeshi hili, wanajihusisha na ujambazi na vitendo viovu, wafichuliwe.

“Samaki mmoja akioza ni wote, hivyo mwanajeshi mmoja akikamatwa katika matukio ya ujambazi na vitendo viovu, tunaonekana wanajeshi wote ni majambazi, hivyo narudia tena, acheni kujihusisha na ujambazi na vitendo viovu ili jeshi letu liendelee kuaminiwa na raia ambao hili ni jeshi lao, wametupa dhamana na wanaligharamia jeshi hili kupitia kodi wanazolipa,” alisema kiongozi huyo.

Amewataka wanajeshi waache tabia ya kufanyakazi kwa kubahatisha, badala yake wajiendeleze kielimu, kwa kuwa sasa jeshi haliwezi kwenda sambamba na mabadiliko ya kisayansi bila kuwa na wanajeshi wasomi na wenye taaluma mbalimbali.

Luteni Jenerali Mwamunyange, alisema jeshi hilo kwa sasa limepanuka na lina mafanikio makubwa, kwa kuwa wanajeshi wenye taaluma ni wengi ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Katika hatua nyingine, kabla ya Luteni Jenerali Mwamunyange kuhutubia, upepo mkali uliezua mahema matatu na kusababisha taflani.

Watu kadhaa walijeruhiwa kwenye harakati za kujiokoa. Walipelekwa hospitali kwa matibabu.

Hali hiyo ilisababisha mahema yang’olewe na hivyo sherehe zilifanyika katika hali ambayo haikukusudiwa awali.

Watu wengi walionyesha kuvutiwa na sherehe hizo.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.