UJENZI wa wodi ya watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambao awali ungegharimu sh bilioni 1.031, sasa utagharimu sh 5,729,333,225.
Gharama hiyo imetokana na kutotekelezwa kwa mradi huo katika muda uliopangwa, na hivyo kufanya gharama za ujenzi zipande.
Akitoa taarifa kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali hospitalini hapo jana, Wazirii wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa, alisema mradi huo ulianza mwaka 1992.
Msimamizi wa mradi alitoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Ardhi na Usanifu wa Majengo (UCLAS); na mkandarasi alikuwa Masasi Construction Company Limited.
Alisema mradi ulisimama mwaka 1992 kutokana na kile kilichoelezwa kwamba ni ukosefu wa fedha uliokuwa unaikabili serikali.
“Mradi ulisimama mwaka 1994, katika kipindi hiki serikali ilikuwa na matatizo ya kiuchumi, hivyo kulisababisha mradi kutoendelea,” alisema Profesa Mwakyusa.
Alisema mradi huo uliendelea kwa awamu baada ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Wahisani.
Mwaka 2002 ulisimama hadi mwanzoni mwa mwaka 2004.
“Sasa mradi umefanyiwa marejeo kabla ya kupata gharama halisi ili kuukamilisha, inakisiwa mradi utagharimu sh 5,729,333,225,” alisema.
Kilichokamilishwa hadi sasa katika mradi huo ni ‘basement ground’ na ghorofa ya kwanza.
Alisema katika mwaka huu wa fedha wa 2006/2007, serikali imetenga sh milioni 728 kwa ajili ya kufunga lift moja, na kukamilisha sehemu za paa na zege na kuweka madirisha ya nje.
“Fedha zilizotumika kumlipa mkandarasi hadi sasa ni sh bilioni 4.1 ambapo ili kukamilisha mkataba kunahitajika sh bilioni 1.6,” alisema.
Alisema gharama za kukamilisha kazi hiyo zinaweza kuongezeka kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi.
Naye Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye ni Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP), aliitaka wizara ikamilishe bajeti halisi ya mradi huo ili kuwe na uwezekano wa kuomba fedha za kutosha kutoka serikalini. Aliitaka serikali iwe makini na miradi inayoanzisha.
Mbunge wa Singida Kusini, Lazaro Nyalandu (CCM), alishauri serikali iwashirikishe wafanyabishara wenye uwezo wa kukopa fedha katika miradi kama hiyo.