Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mabilioni yaongezwa mikopo ya wanafunzi
Mabilioni yaongezwa mikopo ya wanafunzi
By Habari Tanzania | Published  09/1/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
Shabani Matutu na Deogratius Temba

SERIKALI imeongeza fedha kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Kiasi kilichoongezwa ni sh bilioni 47.8 ambacho sasa kinajumuishwa na kiasi cha sh bilioni 63.5 kilichokuwa kimeshapitishwa kwenye bajeti ya Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia ya mwaka 2006/2007.

Uamuzi huo wa serikali umo kwenye tamko lake ambalo lilitolewa kwa waandishi wa habari jana na Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Peter Msolla.

“Pamoja na ufinyu wa pato la taifa, serikali imeamua kuongeza kiasi cha sh bilioni 47.8; sawa na ongezeko la asilimia 75.3 ya bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Profesa Msolla alitaja baadhi ya sababu za kuongezwa kwa fedha hizo.

“Ongezeko la udahili kwa wanafunzi walio na sifa za kujiunga na vyuo vya elimu ya juu; ongezeko la mahitaji ya fedha ya mikopo ya chakula na malazi; na ongezeko la muda wa mafunzo kwa vitendo kulingana na mitaala ya vyuo,” alisema.

Profesa Msolla alirejea baadhi ya sifa za wanafunzi wanaostahili kupewa mikopo hiyo kwa mwaka 2006/2007.

“Wanafunzi ambao walinufaika na mikopo ya mwaka 2005/2006 na ambao wanaendelea na masomo, wataendelea kupata mikopo hadi watakapohitimu masomo.

“Hata hivyo, kuanzia sasa na baada ya sheria namba 9 ya mwaka 2004 ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kurekebishwa ili kuondoa kasoro zilizojitokeza, itahakikishwa kwamba wanafunzi watakaopata mikopo ni wale tu wenye stahili hiyo kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Kuna ongezeko la wanafunzi 51,064 mwaka 2005 hadi wanafunzi 99,729 mwaka 2006.

Profesa Msolla, alitaja makundi mengine kuwa ni wale waliofaulu vizuri zaidi, yaani wavulana waliofaulu kwa daraja la kwanza, na wasichana waliofaulu kwa madaraja ya kwanza na pili.

Wengine ni wale waliosajiliwa kwenye programu ya elimu. “Serikali imeamua kutoa mikopo kwa wanafunzi wote watakaochukua mafunzo ya ualimu katika vyuo vikuu vya umma na binafsi ambao tayari wamesajiliwa,” alisema.

Wengine wenye sifa ni wale waliosajiliwa kuchukua taaluma za sayansi. Hatua hiyo alisema itahamasisha Watanzania wengi zaidi kusoma masomo hayo ili kukabiliana na changamoto ya maendeleo ya sayansi na teknolojia.

“Pia serikali imeamua kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wote waliosajiliwa kuchukua masomo katika programu zifuatazo:

“Wanafunzi wote watakaopata udahili katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA); wanafunzi wote watakaopata udahili na kuchukua masomo ya uhandisi katika vyuo vya ndani vinavyotoa masomo hayo; wanafunzi wote watakaopata udahili na kuchukua masomo ya fani zinazofundishwa katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Ardhi na Usanifu wa Majengo (UCLAS); na wanafunzi wote watakaopata udahili kwenye vyuo vya umma na binafsi katika fani za sayansi za afya,” alisema Profesa Msolla.

Alisema wanafunzi wa mwaka wa kwanza watakopeshwa hadi asilimia 60 katika ada ya mafunzo kwa vitendo na mahitaji maalumu ya vitivo.

“Wanafunzi watapaswa kuchangia asilimia 40 iliyobaki. Aidha, wanafunzi wa mwaka wa kwanza watakopeshwa asilimia 100 katika chakula na malazi, vitabu na viandikio vya utafiti,” alisema.

Kuhusu urejeshaji mikopo, alisema atakayekiuka utaratibu huo atashitakiwa kwa mujibu wa sheria. Walionufaika na mikopo kuanzia mwaka 1994/1995 wanatakiwa waanze kurejesha mikopo hiyo sasa.

Ameagiza marejesho ya mikopo yapelekwe kwenye akaunti maalumu namba 2011100205 itakayotumika kuhifadhi fedha hizo katika benki ya makabwela ya NMB, Tawi la Bank House, Dar es Salaam.

“Waajiri wa sekta ya umma na binafsi waanze kuwakata mishahara waajiriwa wao waliopata mikopo hiyo. Hii ni pamoja na wale wakopaji waliojiajiri wenyewe,” alisema.

Waziri huyo alisema uwezo wa serikali kifedha ukiwa mzuri, makundi mengine ya wanafunzi yataendelea kunufaika na mikopo.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.