MPAKA wa Tanzania na Zambia, upande wa Tunduma na Nakonde, jana uligeuka uwanja wa vita, magari yakichomwa moto, mali zikiporwa na polisi wa Zambia wakiwapiga risasi Watanzania.
Mapigano hayo yalianza asubuhi kwa kuwahusisha Watanzania na Wazambia, baada ya Watanzania hao kukasirishwa na kitendo cha polisi wa Nokonde, Zambia, kumuua mwenzao, Lucas Msuya, akiwa mahabusu.
Jana, Tunduma na Nakonde kulitawaliwa na milio ya risasi, huku polisi wa Kikosi Maalumu cha Kutuliza Ghasia (FFU), kutoka Mbeya wakilemewa na wingi wa watu.
Vurugu zilianza baada ya kundi la Watanzania kutaka kuvuka kwenda Nakonde kuchukua maiti ya mwenzao.
Wananchi wa pande zote mbili walivamia malori na kuyaharibu. Kila upande ulipoona gari la upande mwingine, liliharibiwa, ama kwa kuchomwa, au kwa kupigwa mawe.
Waporaji walitumia mwanya huo kupora mali kwenye magari, makontena na kila mahali walipoona mali.
Baadhi ya magari ya Tanzania yaliyoharibiwa upande wa Zambia yana namba T 990 ABW, T 133 ADF na T 244 AMZ.
Malori mengine mawili yaliyochomwa moto, namba zake hazikuweza kufahamika.
Madereva walionusurika kuuawa waliiambia Tanzania Daima kwamba magari yao yaliharibiwa chini ya ulinzi wa polisi wa Zambia.
“Walikuwa mpakani wakitaka wayavushe waingie Tanzania, wakaagizwa wayaegeshe,” alisema mmoja wa walioshuhudia tukio hilo.
Kwa upande wa Tanzania, malori matatu ya Zambia yaliteketezwa kwa moto baada ya kupakuliwa shehena ya matairi na vifaa mbalimbali.
Lori jingine lilipakuliwa magunia 450 ya dagaa, huku mengine mawili yakiharibiwa kwa mawe na hivyo kufanya jumla ya malori yaliyoharibiwa kufikia matano. Takwimu hizo ni zile zilizopatikana wakati Tanzania Daima inakwenda mitamboni.
Wananchi wa Tanzania pia walichoma nyumba moja ya Mzambia baada ya Wazambia kuharibu vibanda vya biashara vya Watanzania vilivyoko upande wa Zambia.
Polisi wa Zambia walimpiga risasi na kumjeruhi Mtanzania Emmanuel Ipyana (22), akiwa katika ardhi ya Tanzania. Alipigwa risasi mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile. Alipelekwa katika Hospitali ya Vwawa.
Mwingine aliyepigwa risasi na polisi hao ni Yohana Mwaruanda (27), ambaye alivunjwa mguu akiwa katika ardhi ya Zambia.
Mwakipesile aliwataka wananchi kuwa watulivu kwa kuwa tatizo hilo linashughulikiwa na serikali.
Alisema juhudi zinafanywa ili kumaliza migogoro ya mara kwa mara katika eneo hilo.
Mapigano ya jana ni ya tatu kutokea eneo hilo. Mwaka jana zilitokea vurugu kubwa, kiasi cha mpaka kufungwa kwa muda.