SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limepunguza kiingilio cha mechi ya kimataifa kati ya timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars dhidi ya Burkina Faso itakayofanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Taarifa ya TFF iliyotolewa jana na kusainiwa na rais wake, Leodegar Chilla Tenga, punguzo hilo limehusu kiingilio cha mzunguuko ambako itakuwa ni sh 2,000 badala ya sh 3,000.
Punguzo hilo limekuja siku moja baada ya wapenzi na mashabiki wa soka kulalamika mbele ya Rais Jakaya Kikwete juzi kuwa, kiingilio ni kikubwa.
Hata hivyo, punguzo hilo limehusu mzunguko tu kwani viti maalumu itakuwa ni sh 20,000, jukwaa kubwa sh 10,000 na kijani ni sh 6,000.
Juzi, Rais Kikwete alifika katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume ulioko Ilala, Dar es Salaam na kushuhudia mazoezi ya timu hiyo kabla ya kuzungumza na wachezaji.
TFF imempongeza Rais Kikwete kwa kusema, ameonyesha ni jinsi gani alivyo na uchungu wa maendeleo ya soka na kwamba, amechochea hamasa kwa wachezaji na Watanzania kwa ujumla.
Aidha, kambi ya Stars jana ilihama kutoka Karume yaliko makao makuu ya TFF hadi Hoteli ya Regency Park iliyoko Msasani na Burkina Faso, wanatarajiwa kuingia leo saa 11:00 jioni.
Stars Jumamosi itacheza mechi ya kwanza dhidi ya Burkina Faso ikiwa ni mwanzo wa kampeni ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Mataifa Afrika mwaka 2008.