RAIS Jakaya Kikwete, leo hatalihutubia taifa kama ilivyo kawaida yake kufanya hivyo kila mwisho wa mwezi, badala yake shughuli hiyo ataifanya kesho akiwa mjini Dodoma.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu, Dar es Salaam jana, ilisema hotuba yake itarushwa moja kwa moja kupitia televisheni na redio, kutoka Ukumbi wa Kilimani.
Atahutubia kupitia viongozi wa serikali na wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Haikuelezwa sababu za rais kuwatumia viongozi hao, badala ya kuwashirikisha viongozi na wanachama wengine wa vyama vya siasa.
Wakati huo huo, Rais Kikwete jana aliagana na Balozi wa Libya aliyemaliza muda wa kuiwakilisha nchi yake hapa nchini, Bashir Albedaim Bashir.
Katika mazungumzo yao Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete, alimpongeza kwa kazi kubwa na nzuri aliyofanya katika kipindi chake cha miaka tisa akiwa hapa nchini.
Balozi Bashir alisema ingawa anaondoka, ataendelea kuyatangaza mazuri yote ya Tanzania.
Viongozi wote hao walisifu mafanikio yanayoendelea kupatikana kutokana na urafiki wa Tanzania na Libya