WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa, anaondoka nchini leo kwenda Thailand na Vietnam kwa ziara rasmi ya kikazi kwa mwaliko wa mawaziri wakuu na nchi hizo.
Madhumuni ya ziara hiyo ni kupanua ushirikiano wa Tanzania na nchi hizo; kisiasa, kiuchumi na kijamii na kupata uzoefu wa nchi hizo wa kurekebisha uchumi kwa muda mfupi.
Akiwa Thailand, atazuru viwanda vinavyoshughulika na madini, hasa ukataji na usafishaji wa vito na miradi ya kuondoa umasikini, na uanzishwaji wa benki ya wanawake.
Waziri Mkuu atafuatana na Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha; Waziri wa Viwanda Biashara na Masoko, Nazir Karamagi; Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk. Batilda Burian.
Septemba 4, Waziri Mkuu atakapoondoka Thailand, Dk. Msabaha atabaki kufuatilia masuala ya madini na Dk. Burian atabaki kujifunza shughuli za akiba na mikopo kwa ajili ya uanzishwaji wa benki ya wanawake.
Akiwa Vietnam, Waziri Mkuu, amepangiwa kukutana na wafanyabiashara aweze kuwashawishi kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji na viwanda vya kusindika mazao.
Atafanya pia ziara katika Chuo cha Sayansi ya Kilimo na kuzuru mashamba ya kahawa na korosho na viwanda vya kusindika mazao hayo.
Nchini Vietnam, Waziri Mkuu atafuatana na mkewe, Mama Regina Lowassa; Waziri wa Kilimo na Chakula, Joseph Mungai; Waziri wa Kilimo na Mazingira Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Burhan S. Haji.
Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dk. Christine Ishengoma; Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile; Mbunge wa Iramba Magharibi, Mgana Msindai (CCM) na Magdalena Sakaya (CUF, Viti Malum, Tabora).
Wengine ni Balozi Mteule wa Tanzania nchini China, Vietnam na Cambodia, Ramadhan Mapuri; Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australia, Balozi Nguma.
Waziri Mkuu na ujumbe wake wanatarajia kurejea nchini Septemba 10, mwaka huu