MIAKA ya hivi karibuni, hapa jijini Dar es Salaam, kumezuka kundi kubwa la vijana walioamua kushinda kwenye vituo vya daladala wakiwalazimisha makondakta wawapatie sh 100 hadi sh 200 kila gari linapoingia na kutoka kwenye vituo vilivyopo maeneo mbalimbali ya jiji.
Vijana hawa ambao wengi wao wanaonekana kuchoka, wameanzisha hata utaratibu wa kuwa na madaftari ya kuchukulia hesabu ya idadi ya magari ambayo yanafika kituoni hapo mithili ya watoza ushuru.
Ukizungumza nao wanasema fedha hizo wanazodai kwa makondakta ni za kujaza gari, wakimaanisha wao ndio wanafanya kazi ya kuwahamasisha watu wapande magari hayo yanapofika kwenye vituo hivyo. Hili ni jambo la ajabu, kwa sababu mimi nikiwa mkazi wa Mbezi, siku zote magari ni ya kugombania, abiria wanaingia wenyewe.
Wakati mwingine vijana hawa wanatumia lugha za vitisho kwa makondakta wanaokataa kuwapa fedha na mara kadhaa wamekuwa wakitoboa matairi ya magari hayo kwa misumari na bisi bisi.
Kundi hili linaongezeka siku hadi siku, na hata kufikia hatua ya wao wenyewe kugombana kwenye vituo hivyo wakigombea magari. Wananchi wanaotumia kituo cha mabasi ya Posta Mpya hapa jijini watakuwa wamewaona vijana hawa ambao huanza kugombania mabasi hayo tangu yanapokata kona ya Barabara ya Bibiti Titi, yanapoingia Barabara ya Azikiwe kilipo kituo hicho.
Vijana hao ambao wengi wao wana umri zaidi ya miaka 25, wamelemaa kabisa, maisha yao yamekuwa ni ya kulazimisha kupewa sh 100 na 200 ambazo hata hivyo wanazitumia kununulia dawa za kulevya na pombe.
Ni kundi linalosikitisha sana, kwa sababu baadhi yao wanaonekana wana nguvu na wangeweza kufanya kazi nyingine lakini wanaonekana kukata tamaa na kuamua kuishi maisha hayo ya kubangaiza.
Shughuli hiyo wanayofanya vijana hao ni sawa na unyang’anyi, kwa maneno mengine ni wizi ambao wanaufanya kwa kushirikiana na makondakta kuwaibia wamiliki wa daladala fedha za makusanyo ya nauli.
Jambo la kushangaza ni kuwa wanapofanya unyang’anyi huo na vitisho kwa makondakta, wanafanya hayo mbele ya askari, wakiwamo wale wa usalama barabarani lakini hakuna hatua yoyote inayochukuliwa. Bahati mbaya sana, watu wengine wanadhani baadhi ya askari hao wanashirikiana na vijana hao, kwa sababu katika vituo vingine vijana hao hukusanya kiasi cha kutosha cha fedha na kuhisi kuwa hugawana nao.
Ukizungumza na vijana hawa watakwambia kuna tatizo kubwa la ajira, wanasema hakuna ajira, kwa hiyo hawana cha kufanya na ndiyo maana wameamua kutumia hiyo njia ya mkato.
Kwa mtazamo wangu, labda na wa wengine pia, hawa vijana ni wavivu wa kufikiri na waoga wa maisha, kwa sababu mawazo yao ni kupewa ajira ya kupata fedha za haraka haraka. Wanachowaza wao ni kupata fedha ya kuwatoa katika shida zao. Wana ndoto ya kuwa na mambo makubwa bila kufanya kazi.
Mawazo yao unapozungumza nao kuhusu nini wanafikiria juu ya maisha yao ya baadaye, utaelewa kweli wana ndoto za mchana. Mawazo yao siku zote ni kuwa iko siku watatoka (wakimaanisha watakuwa matajiri).
Bangi na dawa za kulevya wanazonunua kwa visenti vidogo wanavyoomba, zinawafanya waendelee kubaki na ndoto hizo za alinacha.
Serikali ya Awamu ya Nne imeanza kazi kwa kutamba kabisa kuwa itaongeza ajira kwa vijana, na labda imeanza kufanya hivyo, lakini vijana hao ambao ni nguvu kazi inayopotea wangeweza kutafutiwa mkakati wa maana kuanzia kwenye serikali za mitaa.
Kwenye ngazi hiyo ya serikali kuna kazi nyingi za kufanya ambazo zinahitaji nguvu kazi kama hiyo. Ile mipango inayoanza kupangwa kama ya usafi wa mazingira, ukusanyaji wa taka na nyingine ambazo wakati mwingine zinakuwa na mlolongo mrefu wa tenda ambazo hata utekelezaji wake si makini.
Kwa mtazamo wangu, vijana hawa wangekusanywa tena ikiwezekana chini ya ulinzi mkali wakaamrishwa kufanya kazi hizi hata kwa ujira wa kawaida zingewafaa. Shida yao ya kwanza ni namna ya kupata mlo wao na mengine yanafuata. Wakiwezeshwa kupata mlo kwa kazi za kijamii watakazopewa, inamaana utakuwa umetatua shida yao kubwa inayowafanya wakaee barabarani na kuomba fedha.
Vijana hawa wasipoangaliwa ni sawa na kutunza bomu mfukoni ambalo wakati wowote linaweza kulipuka. Vijana hawa kutokana na matatizo waliyonayo, ndio hao wanaotumiwa na baadhi ya watu kupata masilahi yao binafsi, wanaweza kutumiwa kama chambo kuingia mahali popote kufanya uhalifu kwa kupewa ujira mdogo maadamu wana njaa.
Haya ndiyo yamekuwa yakifanywa na vijana hawa ambao hawaoni thamani ya maisha, inawalazimu kuingia kwenye mkumbo wowote ili wapate chochote.
Vijana hao ambao ni wa kiume, ni ndugu zetu, watoto wetu na kaka zetu, lazima tuwabadilishe waache tabia hiyo tegemezi na wakikataa kubadilika tutumie nguvu, kwa sababu tukiendelea kucheka nao na kuwapa hivyo vi-senti, tunaendelea kuwalemaza. Kuendelea kuwa na mawazo ya kila wakiamka asubuhi wanaamkia kwenye stendi za mabasi kuvuna mavuno wasiyolima ni wizi.
Askari wa usalama barabarani, na wengine wanaofanya doria kuendelea kuwaacha vijana hawa ambao wanawafahamu, ni kuendelea kuwaangamiza. Wafukuzeni wajue wanachofanya si halali, ni wizi, mkifanya hivyo mtafanya akili zao zibadilike na wafikirie njia nyingine za kufanya ili wapate kipato.
Vijana hawa wa Kitanzania, waumize vichwa vyao, wafungue macho waangalie wenzao wanafanya nini kujipatia riziki, wasikubali kuwa watumwa wa njaa ya leo pekee. Nitoe mwito kwa asasi nyingine za kiraia ambazo ziliweza kuwakusanya watoto wa mitaani na kuwaweka pamoja na kuwatafutia maisha mapya, ziwaangalie na vijana hawa na kuwatafutia njia mbadala za kuwaondoa kwenye lindi hilo la kuwa waombaji kwenye vituo vya daladala