MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), ameteuliwa na Rais wa Shirikisho la Ujerumani, Horst Kohler kuwa miongoni mwa viongozi 40 vijana kutoka Ujerumani na Afrika watakao mshauri.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na chama hicho na kusainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Erasto Tumbo, ilieleza kuwa viongozi hao vijana watashiriki kongamano la pamoja lililoitishwa na Rais Kohler kumshauri kuhusu changamoto za pamoja zinazoikabili Ujerumani na Afrika na nini kifanyike kwa faida ya pande hizo mbili.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa katika kongamano hilo, ni agenda ya mazingira na makazi, migogoro na machafuko, elimu na ajira na ushiriki wa vijana katika masuala ya uandaaji sera na siasa.
Sanjari na vijana hao 40, kongamano hilo litaudhuriwa pia na watu 30 mahiri katika medani za siasa, biashara na jumuiya ya kiraia.
Maandalizi ya kongamano hilo yataanza kwa vijana hao kujadili agenda hizo katika makundi kwa njia ya mtandao, na kuanzia Novemba 23-27, mwaka huu, watakutana kwa mara ya kwanza Lutherstadt Wittenberg, Ujerumani na kongamano rasmi Januari 12, 2007, Accra, Ghana