SERIKALI imetangaza ratiba mpya ya mgawo wa umeme kutokana na kuharibika kwa mashine namba sita ya Songas iliyopo Ubungo, Dar es Salaam.
Kwa hatua hiyo, serikali imewatahadharisha wananchi kwa kuwataka wawe tayari kukabiliana na hali ngumu itakayosababishwa na mgawo huo.
Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha, jana aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake kuwa, makali ya mgawo wa umeme sasa yatauma siku tano kwa wiki.
Jumamosi na Jumapili pekee ndizo siku ambazo watumiaji umeme wataupata bila shaka. Kiasi kidogo cha maji katika Bwawa la Mtera, ndicho kinachotumika sasa. Hali huenda ikarejea kuwa nzuri mwezi Oktoba, 2006.
Alisema watakaoathirika zaidi ni watumiaji wa majumbani ambao watakuwa wakipata umeme siku mbili kwa wiki.
“Kabla ya kuharibika mashine namba sita ya Songas, mgawo uliendeshwa kwa kupunguza MW 100-120 kwa maana kwamba watumiaji wa umeme majumbani walikuwa wanakosa umeme kwa siku tatu kwa wiki.
“Kwa tukio la Songas, MM 180 zinatakiwa zipunguzwe, mgawo huo utawafanya watumiaji wa majumbani kukosa umeme saa 12 kwa siku tano kwa wiki hadi uzalishaji utakapoongezeka,” alisema Dk. Msabaha.
Dk. Msabaha alisema makali ya mgawo wa umeme yataongeza pia gharama kwa uchumi na ustawi wa jamii.
“Ni ukweli ulio wazi kuwa gharama kwa uchumi na ustawi wa jamii wa nchi yetu utakuwa mkubwa zaidi kutokana na kukosekana kwa MW 40 katika mfumo wa gridi ya umeme wa nchi.
“TANESCO peke yake inapoteza sh bilioni 4 kwa mwezi kutokana na mgawo wa umeme unaoendelea hivi sasa, hivyo kuongeza kwa makali ya mgawo kuna maana kuwa kiasi cha fedha wanachopoteza kitaongeza,” alisema Dk. Msabaha.
Dk. Msabaha alisema mashine hiyo iliharibika Agosti 23 na kusababisha upungufu wa MW 40 katika mfumo wa uzalishaji umeme nchini.
Alisema ilikaguliwa na mtaalamu wa General Electric Agosti 26, 2006 ambaye alithibitisha kuwa ina tatizo kubwa na ilipaswa kufanyiwa matengezo nchini Uholanzi.
Alisema mashine hiyo ilisafirishwa jana kwenda Uholanzi kwa matengenezo yatakayochukua wiki nane.
“Gharama ya kutengeneza turbines hizo inakisiwa kuwa dola milioni moja za Marekani na zitatolewa na Songas.
“Serikali haitahusika kwa namna yoyote na gharama hizo,” alisema Dk. Msabah