MKURUGENZI wa Idara ya Wanyamapori, Emmanuel Severe, anazidi kuula katika idara hiyo, awapiku waziri wake, Anthony Diallo, na wabunge wanaomlalamikia.
Severe ambaye mwezi uliopita alishambuliwa na wabunge kwa kumtaka ang’oke kwenye madaraka hayo, haonyeshi dalili za kuondoka kwa hiari.
Ofisi ya Rais ambayo ndiyo yenye uwezo wa kumwondoa, imesalimu amri na kumwacha mkurugenzi huyo akiendelea kushika wadhifa huo.
Muda mfupi baada ya Diallo kushika wizara hiyo, alifanya mabadiliko, akilenga kuleta ufanisi zaidi katika wizara yake, lakini Severe akayapinga. Akakataa kuhama, badala yake akaendelea kukalia ofisi hadi sasa.
Maelezo ya kutohama kwake ni kwamba waziri hakuwa na uwezo kisheria wa kumng’oa, kwani yeye ni mteule wa rais.
Alipokataa kuhama, kuliibuka hoja ya kwamba anayemlinda ni Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo. Baadaye katibu huyo aling’aka, na kueleza kwamba kinachomlinda Severe, ni taratibu za utumishi, kwani waziri hana mamlaka ya kumwondoa.
Hata hivyo, kauli hiyo ilitafsiriwa vingine, kwani vyanzo vya habari vilisema Severe na Luhanjo ni marafiki walioshibana, na wanaosaidiana kwenye raha na katika shida.
Baadaye kukatokea uvumi kwamba miongoni mwa wanaomlinda mkurugenzi huyo ni Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kwa madai kwamba wote wanatoka sehemu moja.
Watu wanaomjua Lowassa, walipinga madai hayo, wakisema Waziri Mkuu kwa tabia yake, halindi mtu, hasa linapokuja suala la maslahi ya taifa.
Severe analaumiwa kwa mambo kadhaa, yakiwamo ya kutoa mwanya kwa wageni kumiliki vitalu vya uwindaji, huku wazawa wakiendelea kuwa watazamaji.
Muda mrefu alioshika wadhifa huo, unaelezwa kwamba ni miongoni mwa mambo yaliyomfanya abweteke.
Wananchi bado wanasubiri kuona Rais Jakaya Kikwete, atachukua uamuzi gani ili kuleta mabadiliko katika idara hiyo ambayo uongozi wake unalalamikiwa mno