Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Wakristo waandaa muswada
Wakristo waandaa muswada
By Habari Tanzania | Published  08/29/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Mwandishi Wetu

UMOJA wa kitaifa ambao Tanzania imejivunia kwa miaka mingi, sasa uko hatarini kutoweka.

Mvutano wa chini chini kati ya serikali na Wakristo kuhusu masuala mbalimbali hapa nchini, umezifanya taasisi za Kikristo, yakiwamo Kanisa Katoliki, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na makanisa mengine ya Kikristo, kuanza mchakato wa kuandaa muswada wa kuanzisha Mahakama ya Kanisa.

Habari zilizoifikia Tanzania Daima, zimesema uamuzi huo umefikiwa na kikundi cha wataalamu kadhaa, wakiwamo wasomi waliobobea, kuanza majadiliano jijini Dar es Salaam kwa wiki tatu sasa, kwenye mkutano usio rasmi. Tayari wameafikiana kuasisi muswada wa sheria ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Kanisa.

Vyanzo vyetu vya habari vinasema wataalamu hao wameamua kulishughulikia suala hilo kama njia ya kujihakikishia haki sawa baada ya kuona serikali imejizatiti kupitisha sheria ya kuundwa Mahakama ya Kadhi Mkuu kwa ajili ya Waislamu.

“Kwa muda mrefu, tumekuwa na serikali isiyojiingiza katika masuala ya kidini moja kwa moja… lakini sasa tunaona dhamira ya serikali iko wazi… kama watajiingiza katika uundaji wa Mahakama ya Kadhi Mkuu, kwa nini serikali hiyo hiyo isijihusishe na uanzishwaji wa mahakama zetu?

“Dhamira ya serikali inakuzwa zaidi na ukweli kwamba suala hili liliingizwa kijanja katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2005. Waumini wa dini nyingine (Waislamu) wamedhamiria kushinikiza serikali iwaundie chombo, huku Wakristo wakipinga… Hatuwezi kuacha mijadala hii iishie hewani…

“Hata baadhi ya maaskofu wetu wameshaliona hilo, na wanasubiri hatima ya kazi za wataalamu…maana wameona wakati juhudi za kuendelea kuifafanulia serikali umuhimu wa nchi hii kuendelea na msimamo wa serikali kutokuwa na dini wala kujiingiza katika masuala ya dini, hutawafaa wengine, iwapo njia muafaka haitakuwapo, hilo litashindikana.

“Kazi inakwenda kwa kasi kubwa… tunaona kama serikali imeamua kwenda mkondo wa dini, nasi tuanzishe Mahakama ya Kanisa, ambayo itatumia Amri Kumi 10 za Mungu, Amri za Kanisa, Sheria za Kanisa (Canon Law) na kanuni mbalimbali zinazoongoza makanisa,” kilisema chanzo chetu.

Mtoa habari alifafanua kuwa mazungumzo na maandalizi ya muswada wa kupeleka bungeni yamekamilika. Anasema:

“Kwa wasomi waliomo makanisani, muswada unaandaliwa hata kwa mwezi mmoja unakuwa tayari. Wanataka Bunge lipitishe, nasi tuwe na mahakama yetu, serikali ibaki na mahakama zake kwa watu wasio na dini. Labda nao wakitaka kuunda zao, watu wetu wasije kunyanyasika pasipo ulazima.

“Hatupingi kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi, ila tunataka haki itendeke. Kimsingi, serikali ingefanya jambo jema kujitoa katika masuala ya dini, iache dini zianzishe mahakama zake bila kutungiwa sheria na Bunge, wala kuhusisha kodi ya wananchi wasiohusika.

“Lakini kama imeamua kujiingiza, haiwezi kupendelea upande mmoja, wengine wakakaa kimya… Vinginevyo, serikali ibaki na mfumo wake wa kimahakama na dini zijiendeshe kwa taratibu na sheria zake, na kama wanaanzisha Waislamu, mahakama hii isiwe na nguvu ya kufunika mfumo wa Mahakama wa sasa,” alisema.

Sura ya 8, Ibara ya 108 (b) ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2005, inaahidi: “Kulipatia ufumbuzi suala la kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara.” Ibara hii ndiyo imewafanya Waislamu nchini waseme kuwa Ilani iliahidi kuanzishwa kwa mahakama hiyo.

“Lakini tunavyoona sisi, walioahidi kuanzisha mahakama hiyo ni CCM, si serikali. Hata kama ni serikali ya CCM, itengue jambo hili kwa masilahi ya taifa. Ijisahihishe,” kilisema chanzo hicho.

Historia inaonyesha kuwa mataifa mengi yaliyokumbwa na migogoro ya kidini yalianza hivi hivi, kwa serikali kuwasikiliza na kuwapendelea watu fulani kisera, na kuziba masikio kwa wengine.

Sudan kuna ugomvi mkubwa kati ya Waislamu na Wakristo na inadhaniwa kuwa mgogoro huo ndio uliozaa mgogoro wa Darfur.

Palestina na Israel zipo katika mgogoro mkubwa kwa zaidi ya miaka 50 sasa kutokana na Israel kujinadi kama Wayahudi, huku Wapalestina wakijinadi kuwa Waislamu. Imani za kidini zimeingizwa katika nguzo za uongozi.

Nchini Uganda, kiongozi wa North Resistance Army (NRA), Joseph Konny, amepigana vita ya msituni kwa miaka 20 na maelfu ya watu wamepoteza maisha kutokana na NRA kutaka taifa la Uganda liongozwe kwa Amri Kumi za Mungu.

Iwapo serikali itapuuza sauti hizi zinazokinzana, ikapeleka bungeni muswada wa kuanzisha mahakama hiyo kwa ajili ya Waislamu, na iwapo Wakristo watajibu mapigo kwa njia hii, ni wazi hizi ni dalili za kuibuka mgogoro wa kidini nchini, utakaoifanya Tanzania isitawalike


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.