Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema wabunge na wawakilishi wa CUF, wamekuwa wakikimbia kuhudhuria shughuli za uzinduzi wa miradi ya maendeleo Kisiwani Pemba.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi wa Zanzibar, Brigedia mstaafu Adamu Mwakanjuki baada ya kukamilisha ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo katika mikoa ya Kusini na Kaskazini Pemba.
Alisema tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu, Serikali imekuwa ikiwaalika wabunge na wawakilishi wa chama hicho lakini hawahudhurii na hivyo viti vyao kubakia wazi.
Waziri Mwakanjuki alisema serikali imekuwa ikiwaalika ili waweze kuhudhuria katika shughuli hizo kwa kuwa wananchi katika mikusanyiko hiyo hupata nafasi ya kuelezea matatizo yao mbalimbali kwa viongozi wa kitaifa.
Akitoa mfano, alisema Rais Amani Abeid Karume alipotembelea ujenzi wa barabara ya Kangani na Bandari ya Wesha, Kiongozi wa Upinzani katika Baraza la Wawakilishi, Bw. Abubakar Khamis Bakar, alialikwa lakini hakuhudhuria.
”Tunapowaalika katika shughuli za miradi ya maendeleo sio kama tunawasuta kwa kupeleka maendeleo Pemba bali ni kutaka wasikie kero mbalimbali za wananchi wanazozitoa kwa viongozi wa kitaifa,” alisema.
Alisema kitendo hicho ni kinyume na sheria kwa vile Wabunge na Wawakilishi ni wawakilishi wa wananchi na siyo vyama vya siasa.
Waziri Mwakanjuki alisema yeye binafsi aliwasiliana na Kiongozi wa Upinzania Barazani, lakini alisema hawezi kuhudhuria ziara hiyo kwa vile alikuwa akihudhuria kikao cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kama Mbunge katika Kamati ya Bunge la Muungano.
Waziri Mwakanjuki alisema ni jambo la kushangaza Wawakilishi wa CUF wamekuwa mstari wa mbele kulalamika katika vikao vya Baraza hilo kuwa Pemba inatengwa kimaendeleo, wakati wanashindwa kuhudhuria katika shughuli za maendeleo na kutoa michango yao.
Hata hivyo, alisema SMZ itaendelea kupeleka miradi ya maendeleo kisiwani Pemba bila ya kujali msimamo wa Wabunge na Wawakilishi wa kujitenga katika shughuli za maendeleo katika majimbo yao.
Katika ziara hiyo, Rais Karume alitembelea mradi wa maendeleo wa barabara ya Kangani, ujenzi wa gati mpya ya Wesha katika Wilaya ya Chake Chake.
Barabara ya Kangani yenye urefu wa kilomita saba, ilikuwa kero kwa wananchi kutokana na kutopitika kwa magari ya abiria na kuathiri shughuli za usafirishaji wa mazao katika soko la ndani.
Hata hivyo, akizungumzia tuhuma hizo, Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma, Bw Salim Biman alisema Wabunge na Wawakilishi wa chama hicho wanajitenga kwa sababu ya kutoitambua serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
”Kwa mujibu wa Tamko la Baraza kuu la chama chetu? Wabunge na wawakilishi wametakiwa wasishirikiane na SMZ hadi hapo suala la mgogoro wa kisiasa litakapopatiwa ufumbuzi, ” alisema Bw Bimani.
Alisema Wabunge wa chama hicho wameruhusiwa kushirikiana na Serikali ya Muungano kwa kuwa matatizo ya uchaguzi yaliyojitokeza Zanzibar tofauti na Tanzania bara.