Mwanamke mkazi wa Mbezi, Jijini Dar es Salaam, Happy Nyirenda (22), amefikishwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka ya kutaka kumuua mtoto wake mwenye umri wa miezi 10 pamoja na mume wake.
Mlalamikaji katika kesi hiyo ni mume wake, Bw. Salvatory Mtui ambaye ameifikisha katika Mahakama ya Mwanzo Magomeni, Jijini Dar es Salaam.
Bw. Mtui alidai kuwa, alitofautiana na mke wake huyo na hivyo akaamua kuondoka na mtoto huyo mchanga.
Alidai kuwa, baadaye alipata taarifa kuwa mke wake alishindwa kumtunza vizuri mtoto wao na badala yake alikuwa akimtelekeza na wakati mwingine hata kutishia kumtupa.
Alidai baada ya kusikia taarifa hizo, aliamua kufuatilia na kugundua sehemu anayoishi na alipofika aliamua kumchukua mtoto huyo.
Mlalamikaji alidai baada ya hapo mshtakiwa alimtumia ujumbe mfupi wa maandishi wa vitisho na matusi kwa kumwambia kuwa atamuua kama hatamrudisha mtoto.
”Mheshimiwa Hakimu, mimi simpi huyu mtoto kwa sababu hawezi kumtunza na ana matatizo mengi,” alidai baada ya kuelezwa kuwa mtoto huyo anastahili kuishi na mama yake kwa vile bado ni mdogo na anaendelea kunyonya.
Alidai mbele ya Hakimu Mary Matoi wa mahakama hiyo kuwa hali ilizidi kuwa mbaya baada ya kukataa kumpa mtoto ambapo alisema kuwa kama akiendelea kukataa basi atamuua pamoja na mtoto huyo kwa sababu yeye ndiye aliyemzaa.
”Mimi nikaona hali sasa ni mbaya yaani amuue mtoto wangu kwa sababu eti yeye ndiye aliyemzaa na pia ataniua na mimi, ndipo nikaamua kumshtaki kwa sababu alionekana amedhamiria kutenda kosa,” alidai.
Mlalamikaji huyo alidai kuwa, amezaa na mwanamke huyo watoto wengine wawili ambao ni mapacha.
Akijibu tuhuma hizo, mshtakiwa alidai kuwa, mtoto huyo anayemng’ang’ania si wa kwake bali ni wa mwanaume mwingine.
”Huyu ni mume wangu, lakini baada ya kuzaa naye mapacha, tulitengana na akaninyang’anya wale watoto nikaenda kuishi peke yangu”, alidai.
Alidai kuwa, alikuwa akihudumiwa na mume aliyekuwa akiishi naye kwa wakati huo lakini baadaye alifuatwa na mlalamikaji akamuomba msamaha ambapo naye alikubali lakini bila kurudi kwake.
”Kwa hiyo nikapata mimba na kuzaa huyu mtoto, sasa kwa sababu tulikuwa sote kwa kipindi hicho, anadhani ni wake, lakini ajue kuwa si wake bali ni wa mtu mwingine, mimi nina bwana wangu anayenihudumia na ambaye pia ndiye mwenye mtoto, yeye anamg’ang’ania,” alidai.
Hata hivyo, mshtakiwa alikana tuhuma za kutaka kumuua mtoto pamoja na mume wake.
Hati ya mashtaka ya kesi hiyo ilidai kuwa, Agosti 3, mwaka huu, saa 10:00 jioni eneo la Magomeni Mapipa, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alitishia kumuua mlalamikaji ambaye ni mume wake na mtoto wake mchanga mwenye umri wa miezi 10.
Hakimu aliiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 4, mwaka huu na mshtakiwa alipelekwa mahabusu baada ya kukosa wadhamini