Watu wanaodhaniwa kuwa majambazi, wakiwa na bunduki aina ya shotgun, wameliteka gari dogo la abiria aina ya Hiace lililokuwa likitokea Horohoro kwenda Tanga mjini na kuwapora fedha abiria Sh. 190,000 na dola 600 za Kimarekani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Bw Issaya Mngulu, alisema tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki saa 1:30 usiku katika eneo la Magaoni Mzambarauni baada ya majambazi hayo kuweka gogo kubwa kwenye daraja.
”Hiace iliyokuwa ikitokea Horohoro ilikuta gogo katika daraja eneo la Magaoni Mzambarauni lililowekwa na majambazi waliokuwa kati ya watatu au watano ambao baada ya kusimama, waliwateka abiria kwa kuwatisha na bunduki ya shotgun na kuwapora fedha zao,” alisema Kamanda Mngulu.
Alisema mmoja wa abiria hao Bw. Salim Hussein (32), aliibiwa Sh. 190,000 na dola 600 za Kimarekani, simu na vitu vingine vidogo vidogo ambavyo walipora kutoka kwa abiria.
Hata hivyo, alisema watu wawili wanashikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo.
Katika hatua nyingine, Kamanda Mngulu amesema mvulana mwenye umri wa miaka 15, (jina limehifadhiwa), anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa Shule ya Msingi Stahabu wilayani Pangani mwenye umri wa miaka 16 (jina limeahifadhiwa).
Alisema tukio hilo lilitokea Agosti 23, mwaka huu huko katika kijiji cha Stahabu wilayani Pangani mkoani hapa saa 5:00 usiku ambapo mvulana huyo alimuingilia kwa nguvu mwanafunzi huyo baada ya kumkuta nyumbani kwao amelala.
Hata hivyo, Kamanda Mngulu alisema wanafanya uchunguzi wa kina kuhusiana na madai hayo ili waweze kumfikisha mtuhumiwa mahakamani.