Rais Jakaya Kikwete amesema si vizuri kwa Wakuu wa Wilaya kupewa ofa za vinywaji na maofisa wanaowaongoza wilayani, kama vile Wakurugenzi wa Wilaya (DED) na wengineo.
Pia, amesema si tabia nzuri na kinyume cha maadili kwa Wakuu wa Wilaya kuwa na tabia ya kukopakopa watu na kudaiwa na watu wengi.
Alisema hayo wakati akifunga Semina Elekezi kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya na Makatibu Tawala wa Mikoa.
Kuhusu masuala ya ? za vinywaji na chakula, Rais Kikwete alisema Mkuu wa Wilaya ni mtu mkubwa sana wilayani na ana uwezo wa uhakika kipesa, hivyo si vizuri kununuliwa bia na vinywaji na ’’wadogo” zake.
”Siyo vizuri mkubwa kununuliwa bia. Sisi Jeshini tunasema it is an offence bosi kununuliwa bia na mdogo wako,” alisema Rais Kikwete, ambaye pia ni Mwanajeshi.
Alisema kinachotakiwa ni wewe bosi, uwe wa kwanza kumnunulia mdogo wako kinywaji na ikitokea alishakununulia bila taarifa, basi wewe bosi mnunulie vinywaji vingi zaidi.
Kuhusu madeni na kukopakopa, Rais Kikwete alisema siyo sifa nzuri kwa Wakuu wa Wilaya na Mikoa, kusifiwa kwa kuwa na madeni mengi.
’Si vizuri kwa Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa kukopa hapa kesho pale, Hizi siyo sifa nzuri,” alisema.
Rais, Kikwete alisema alilazimika kuwaacha kwenye uteuzi baadhi ya wakuu wa wilaya, waliokuwa na sifa hiyo ya madeni na kukopakopa kwa watu.
Alisema kiongozi anapokuwa na madeni, husababisha hata awe mwongo anapojaribu kutafutwa na watu.
”Ukimpigia simu na kuuliza uko wapi, anakujibu nipo Monduli kwa shughuli. Anaogopa kukwambia alipo kutokana na madeni, alisema.
Pia, alisema wananchi huwachoka viongozi wenye tabia ya kukopakopa na hufikia hatua ya kutoboa tabia hiyo kwa wakubwa kwa kusema ’’Unafahamu DC wako huyu ana madeni. Anakopa tu.”
Rais Kikwete alisisitiza kuwa lazima Wakuu wa Wilaya na Mikoa, wawe mfano wa tabia nzuri na mwenendo mzuri kwa viongozi na wananchi wanaowaongoza.
’’Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanatakiwa kuwa waadilifu, wanyenyekevu na wasikivu, alisema.