Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Waheshimiwa wabunge, yapo mengi ya kukemea
Waheshimiwa wabunge, yapo mengi ya kukemea
By Habari Tanzania | Published  08/27/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated

NINANYANYUA macho juu na kuona jua la siku mpya. Hali ya hewa inavutia na najisikia mwenye afya njema. Ninatoa dua ya shukrani kwake yeye anayetukutanisha kila Jumapili kupitia waraka huu mfupi na mwepesi. Ninatazama kwa matumaini mbele ya safari, nikiamini kasi mpya tuliyonayo itatufikisha kwenye neema bila hiana.

Wabunge wetu wamemaliza kikao cha bunge la bajeti. Wamerudi majimboni kwao kuwatumikia wananchi. Ni bunge lililokuwa na mambo mengi yanayoacha tafakari kubwa. Wabunge kadhaa walilazimika kukimbia walichoamini au kung’ang’ania wasichoamini.

Hii ilitokana na ile hoja ya kuthibitisha kauli wanazozitoa. Niliwahi kujadili hili. Mbunge anatoa hoja, anaambiwa athibitishe, anafuta kauli yake. Maana yake ni moja kati ya hizi: Au alisema asichoamini au ameamua kufunika kombe mwanaharamu apite. Usahihi wa kutaka mbunge athibitishe kile alichotumwa na wapiga kura wake ni swala la mjadala unaojitegemea.

Hata hivyo, wakati kikao hicho cha bunge kikifikia mwisho, wabunge walitoa karipio kali kwa mtengezaji filamu ya Darwin’s Nightmare na kama nimeelewa vyema, wale waliowezesha utengezaji wa filamu hiyo nao wanapaswa kuchukuliwa hatua. Wabunge wametoa tamko hilo ili kulinda heshima ya Mtanzania na pengine pia kulinda soko la sangara katika jumuiya ya kimataifa.

Ninatamani sana kuona au kusikia wabunge wakitoa makaripio mengi kwa mambo yanayodhalilisha taifa letu. Nina hamu ya kusikia malalamiko yao kwa hao wanaotufikisha tulipo kama walivyomkemea Sauper. Yapo mengi ya kukemea, lakini sijui kwa nini wameamua kwa kauli moja kukemea hili kwa nguvu zao zote. Labda mengine wameyaweka kiporo.

Ningetamani sana nikisikia wabunge wakikemea vitendo mbalimbali vinavyofanywa dhidi ya raia. Unakumbuka hukumu ya Jaji Robert Kisanga wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala wa Sheria? Nazungumzia ile hukumu ya wanakijiji wa Kijiji cha Nyamuma.

Jaji Kisanga akathibitisha kwamba watu wale walifanyiwa unyama kuliko wanyama wenyewe. Nyumba zao zikachomwa moto na hata vyakula vyao vikateketezwa. Kitendo hicho kilifanywa na chombo cha dola. Kwa nini wabunge hawajatoa kauli kali kukaripia hao wanaokiuka haki za binadamu kwa kiwango hiki? Labda watawakaripia kikao kijacho cha bunge.

Kuna jambo lingine linaisononesha sana nafsi yangu. Ni haya mapigano ya huko wilayani Tarime. Nasikia huko kuna watu wanaitwa Waanchari wanapambana na wenzao Waryanchoka. Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Paschal Mabiti, aliwahi kusweka mahabusu waandishi waliojaribu kufuatilia suala hili.

Ni lini bunge litakemea wale wote wanaoondosha amani katika kaya yetu ambayo sote twafahamu pasi shaka kwamba ni kisiwa cha amani na utulivu? Ni kweli wabunge hawajui ugomvi huo uliodumu kwa muda sasa? Chanzo chake ni kipi na suluhu iko wapi? Natamani nisikie wahusika wa ugomvi huu wakilaaniwa kuliko alivyolaaniwa Sauper wa watu!

Januari 2001 kulitokea ghasia mbaya sana kule Zanzibar. Walikufa watu na inasemekana tulizalisha wakimbizi kwa mara ya kwanza katika historia ya kaya yetu. Rais mstaafu Benjamin Mkapa, alikiri kwamba jambo hilo lilimkosesha usingizi. Watetezi wa haki za binadamu wakalalamika. Wasomi wakalaani, wanaharakati wakapiga kelele. Sikusikia bunge likilaani tukio lile. Kwangu lile tukio lililonyofoa nafsi za watu lilipaswa kupewa laana kubwa kuliko hili la Sauper. Sijui, labda ni ufinyu wa mawazo yangu mepesi.

Yawezekana kabisa kwamba doa tulilolipata baada ya damu kumwagika visiwani Zanzibar Januari 2001 ni dogo na linatakasika haraka zaidi kuliko doa lililotengenezwa na Sauper? Haiwezekani kwa namna yoyote kwamba chokochoko za huko visiwani zinaathiri biashara ya utalii kwa kiwango sawa na filamu ya mapanki inavyodaiwa kuathiri soko la samaki? Kwa nini hatujasikia tamko kali lenye kulaani wote wanaoendekeza siasa zisizo na ustaarabu huko Zanzibar? Nausikitikia uelewa wangu mdogo!

Kuna mikataba inayotuingizia hasara kila kukicha. Inasemwa hadharani na kimya kimya, nani alisaini mikataba hii? Watu wanahoji na kwa mbali utasikia wakiulizia mikataba kama ya IPTL. Ukitega sana masikio utasikia fununu za uuzaji wa mashirika ya umma kwa bei ambayo watu hawaridhiki nayo. Wapo wenye utani wanasema kampuni inauzwa kwa bei ya ukwaju. Ipo kampuni kubwa iliyouzwa kwa bei ndogo kuliko gharama za kumnunua mchezaji wa kulipwa Ulaya. Kampuni hiyo inafanya biashara Tanzania nzima na inapata faida kbwa. Kwani wao mazuzu wanunue kisichokuwa na faida? Lini na wapi bunge watakaa wakemee mikataba hii? Kwani lazima kwanza rais akemee ndipo wabunge watoe tamko?

Kuna kashfa za rushwa na ufisadi zinazoendela hapa na pale. Kuna kelele za kusema hivi nyumba yetu ya ubaloz huu au ule ni shilingi ngapi? Kuna utata wa bei, lakini nani amekemewa na wabunge kuhusu hitilafu zinazotia shaka katika mwenendo mzima wa ununuzi na uuzaji? Haya hayaliangamizi na kulidhalilisha taifa sawa na filamu ya mapanki? Sina hakika. Nani anaridhika na hiki kinachoitwa mrahaba? Yuko wapi? Ni wabunge au wananchi au wote kwa pamoja? Simo!

Unakumbuka mambo kama ya wizi wa mitihani? Unafahamu habari za hicho kinachoitwa ‘ten percent’? Umewahi pia kusikia kuhusu wafanyakazi hewa? Bado huna habari zozote kuhusu dawa za kulevya? Inawezekana wabunge hawajasikia hizi porojo za vijiweni kwamba biashara hiyo inayozuzua vijana wetu inaendeshwa na hao wanaoitwa vigogo? Hilo halionekani kama jambo la kukemea kuliko uongo wa Sauper?

Sasa hivi kuna mpango wa kuuza mashamba ya Kipunga na Mbarali kwa wawekezaji. Ni kweli mashamba hayo ni ya serikali lakini si kweli kwamba serikali ina haki ya kufanya itakavyo na ardhi. Ardhi yetu imekabidhiwa kwa rais akiwa kama mdhamini tu, lakini wenye ardhi ni wananchi. Sasa hivi kwa sababu zozote zile ziwazo, ardhi hiyo inabinafsishwa. Waliokuwa wakijipatia neema hapo, sasa itawalazimu waondoke.

Sijasikia wabunge wakitoa tamko kwamba ardhi hii ni ya wanachi na si busara kuwaondoa na kumuuzia mwekezaji haidhuru analeta shilingi ngapi! Yawezekana wamekubaliana na maoni ya Mzee Mungai kwamba Edwin Mtei (bila shaka na wote wenye mawazo kama ya Mtei) anazeeka vibaya kupinga uuzaji wa mashamba ya Kapunga na Mbarali? Wanasubiri hadi mwekezaji aingie ndio watoe tamko la kutaka mkataba wa uuzaji wa mashamba hayo utazamwe upya? Maswali ni mengi kuliko majibu.

Sitaki wala sipendi nisikie wabunge wakisema hawakuwepo bungeni wakati baadhi ya matukio haya yakitokea. Sitaki. Kwanza wapo waliokuwepo bungeni wakati baadhi ya kero zinazochefua zikifanyika. Lakini cha muhimu zaidi ni kwamba bunge ni taasisi si nafsi za watu. Siku zote taasisi zinadumu bali nafsi zinabadilika. Kwani hawakuwepo bungeni wakati roho za watu zilipokuwa zikinyofoka visiwani? Kama hawakuwepo bungeni wakati huo basi wajue pia hawakuwepo bungeni wakati Sauper anatengeneza filamu yake. Naam, tukemee kwa ukali yote yanayodhalilisha taifa bila ubaguzi wala nia ovu.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.