ASILIMIA 63 ya Waisrael wanamtaka Waziri Mkuu, Ehud Olmert ajiuzulu kutokana na namna alivyoshughulikia vita dhidi ya wapiganaji wa Hezbollah nchini Lebanon.
Kwa mujibu wa kura za maoni, Waisrael wengi wanaona kwamba mkataba wa kusitisha mapigano uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa (UN) na kukubaliwa na Olmert unaonyesha kushindwa kwake kwa sababu uongozi wa kundi la Hezbollah haukutetereka na askari wawili waliotekwa nyara na kundi hilo Julai 12 na kuzusha vita bado wanashikiliwa mateka.
Watu karibu 1,110 wa Lebanon na 157 wa Israel waliuawa katika vita hiyo.
Kura ya maoni iliyoendeshwa na Gazeti la The Yedioth Aronoth kwa mara ya kwanza ilionyesha idadi ya watu wanaomuunga mkono Olmert ikipungua.
Kura nyingine zilionyesha kwamba kwa sasa chama cha mlengo wa kulia cha Likud na kiongozi wake Benjamin Netanyahu kinaungwa mkono zaidi baada ya siku 34 za vita.
Kura ya maoni iliyoendeshwa na Gazeti la Maariv ilionyesha kwamba ni asilimia 14 tu ya Waisrael waliosema watamchagua Olmert iwapo uchaguzi utafanyika huku asilimia 26 ikimuunga mkono Netanyahu, waziri mkuu wa zamani.
Kura za maoni za The Yedioth zilisema kwamba asilimia 45 watamuunga mkono Netanyahu.
Olmert, mwanasiasa ambaye tofauti na mawaziri wakuu waliomtangulia waliokuwa na sifa nyingi za kijeshi, ameshuhudia akipungua umarufu kwa kasi tangu ashindwe kulitokomeza kundi la Hezbollah, ambalo lilivurumisha maroketi 4,000 kaskazini mwa nchi wakati wa mgogoro huo.
“Olmert ang’oke,” lilisomeka moja ya mabango yaliyokuwa yameshikwa na mamia ya askari wa akiba na familia zao kwenye kaburi la Waziri Mkuu wa zamani Golda Meir, juzi.
Waandamanaji hao walimtaka Olmert afuate mfano wa Meir, ambaye alilazimika kujiuzulu baada ya vita ya Mashariki ya Kati mwaka 1973 ambayo ilishuhudia Misri na Syria zikifanikiwa kuitia Israel hasara kubwa.
Yedioth, ambalo ni gazeti kubwa zaidi la kila siku nchini hapa, liliyaita matokeo hayo ya kura ya maoni kuwa tetemeko kubwa la kisiasa kwa Olmert, ambaye chama chake cha mlengo wa kati, Kadima kilikishinda chama cha Netanyahu, Likud kwenye uchaguzi mkuu wa Machi mwaka huu.
Kura kama hizo zilizochapishwa wiki iliyopita zilionyesha asilimia 41 walimtaka Olmert ajiuzulu.
Asilimia 22 ya Waisrael kwenye kura hiyo ya maoni walisema kwamba Netanyahu ndiye anayefaa zaidi kuwa waziri mkuu kulinganisha na asilimia 11 dhidi ya Olmert.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa matatizo yanayomkabili Olmert mbali ya vita, pia yanachangiwa na kashfa zinazomkabili rais wa nchi kuwadhalilisha wanawake kimapenzi.
Pia kura za maoni zimeonysha kwamba wananchi wengi wanataka Waziri wa Ulinzi, Amir Peretz, wa chama cha mlengo wa kushoto, Labour pamoja na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Dan Halutz wajiuzulu.
CNN