SERIKALI imesema itatenda haki katika kumpata mwekezaji wa miradi ya makaa ya mawe Mchuchuma na chuma cha Liganga.
Imesema mpaka sasa hakuna mwekezaji aliyepewa miradi hiyo; na kwamba waombaji wote walioomba kuiendeleza bado wanachunguzwa ili kumpata mwenye sifa zinazostahili kukabidhiwa miradi hiyo.
Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dk. Mathayo David Mathayo aliiambia Tanzania Daima ofisini kwake, Dar es Salaam kuwa, serikali haiwezi kukurupuka katika suala hilo.
“Serikali inatambua umuhimu wa miradi ya makaa ya mawe ya Mchuchuma na chuma cha Liganga, haiwezi kukurupuka tu na kumpa mwekezaji ambaye hana uwezo wa kuiendeleza, mpaka sasa hakuna mwekezaji aliyekwishapewa japo kipande cha ardhi chenye rasilimali hiyo.
“Tunayo orodha, walioomba wapo wengi, wanafanyiwa kazi ili kubaini mwenye uwezo wa kuiendeleza miradi hiyo. Hatuwezi kufanya makosa, serikali iko makini sana, wanaofikiri kwamba kuna mchezo mchafu utafanyika wanajidanganya, katika hili Watanzania wasiwe na wasiwasi,” alisema Dk. Mathayo.
Hata hivyo, Dk. Mathayo alikataa kueleza vigezo vilivyoweka kuwachuja waombaji ili kumpata mwekezaji anayestahili kwa maelezo kwamba suala hilo ni la kitaalamu na limekabidhiwa kwa wataalamu walishughulikie.
“Haya mambo ni ya kitaalamu, serikali inao wataalamu wa kutosha imewakabidhi jukumu hilo, ni vizuri wapewe muda washughulikie kazi waliyopewa, lakini Watanzania wote waelewe kwamba haki itatendeka kumpata mwekezaji anayestahili,” alisisitiza Dk. Mathayo.
Akizungumzia tuhuma za wizara yake kumbeba mwekezaji mmoja, Shubash Patel anayemiliki Kampuni ya MMI Steel ambaye anadaiwa kubebwa na serikali, alisema jambo hilo ni geni kwake.
Alisema hata kama kuna kiongozi anayempendelea Shubash, ingawa yeye haamini, itakuwa vigumu kumkingia kifua kwa sababu mwekezaji wa Mchuchuma na Liganga hachaguliwi na kiongozi mmoja.
“Ninaamini wizara haimbebi mwekezaji yeyote, na hata kama kuna kiongozi mwenye urafiki na Shubash ni vigumu kumbeba kwa sababu mwekezaji wa Mchuchuma na Liganga hachaguliwi na kiongozi mmoja.
“Binafsi simfahamu Shubash wala sijawahi kukutana naye, kama tuhuma anazodaiwa kuzifanya za kutumia ushawishi kuipata miradi hiyo, labda anazifanya kwa wengine, lakini hapa kwangu hajawahi kufika wala kwa waziri sijawahi kumuona,” alisema Dk. Mathayo.
Aidha, alieleza kuwa taarifa kwamba waziri wake, Nazir Karamagi aliwaita wabunge wa Mkoa wa Iringa na kuwaweka sawa ili wasimpe kibano katika bajeti yake, siyo za kweli.
“Waziri anaweza kuwaita wabunge kadhaa na kuzungumza nao, lakini ikitokea hivyo sio kwamba anawaweka sawa, ila mawaziri huwa wanatumia muda huo kutoa ufafanuzi wa mambo ambayo hayajaeleweka kwa wabunge. Hapo huwa wanazungumza na kufahamishana zaidi kuhusu jambo husika,” alisema Dk. Mathayo.
Miradi ya Mchuchuma na Liganga imekuwa gumzo miongoni mwa Watanzania baada ya kupatikana taarifa kwamba baadhi ya viongozi wa serikali wanatumia madaraka yao kuitoa kwa mwekezaji ambaye hana sifa zinazostahili kuiendeleza.
Baadhi ya viongozi wa serikali na wanasiasa wakiwamo wabunge, wameonyesha migongano ya wazi kuhusu kumpata mwekezaji wa miradi hiyo.