Bei ya nafaka kwenye masoko na maduka mbalimbali nchini, imezidi kupanda kwa kasi ya kutisha.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwenye masoko na maduka jijini Dar es Salaam, umebaini kuwa unga wa mahindi umepanda kutoka Sh. 350 hadi Sh 600 kwa kilo, wakati mchele wa Mbeya ulikuwa ukiuzwa kutoka Sh.550 hadi Sh 1,500 kwa kilo.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali hiyo, Katibu wa Umoja wa Wauza Nafaka na Wawekezaji katika soko la Tandale (TAMAGRASAI), Bw. Abdul Kambaya, alisema hali hiyo inatokana na kiwango cha mchele kinachoingia sokoni kuwa kidogo.
Alisema msamaha wa ushuru, haujawanufasha mwananchi kwa kuwa bei ya unga, imepanda kutoka Sh. 550 hadi 600 kwa kilo.
Naye Makamu Mwenyekiti wa soko la Tandale, Bw. Alli Uledi, alisema hali hiyo inasababisha pia bei ya mchele kuuzwa kati ya Sh. 1,100 hadi Sh 1,200 kwa kilo.
Alisema mchele uliongizwa nchini uliopunguziwa ushuru, nao unauzwa kwa bei ya kati ya Sh. 900 hadi Sh 1,000 kutoka bei ya mwaka jana ya Sh. 285.
Alisema wenye vinu vya kukobolea mahindi, wanauza mahindi hayo kwa bei ya Sh. 308, badala ya ile ya zamani ya Sh. 80 hadi Sh 106 kwa kilo moja.
Alisema unga wa mahindi ambayo yameondolewa ushuru wa kuingiza nchini, unauzwa kwa bei ya rejareja ya Sh. 600.
Alisema ’Kutokana na hali hiyo, wananchi hawajanufaika na msamaha wa ushuru kwa kuwa bei ya bidhaa hiyo kuzidi kupanda kwa kasi ya kutisha’.
Alitaja bidhaa zingine ambazo bei yake imepanda kuwa ni sukari na mafuta na kwamba atakayeathirika zaidi ni mlaji wa mwisho.
Alisema cha kushangaza ni kwamba sukari inazalishwa kwenye viwanda vya Mtibwa na Kilombero, lakini sukari inauzwa kwa bei ya juu ya kuanzia Sh. 900 hadi Sh 1,000 kwa kilo.
Lakini, alisema wanachi wa Zanzibar wananunua sukari kwa bei ya Sh. 500 hadi 600 kwa kilo. Alisema sukari hiyo huagizwa kutoka Brazil.
Inakadiriwa kuwa mahitaji ya sukari nchini ni tani 300,000 kwa mwaka, lakini uzalishaji wa viwandani ni tani 270,000 tu.
Kuhusu maharage, Bw. Kambaya alisema bei yake hivi sasa imeshuka kutoka Sh. 850 hadi kati ya Sh.600 na 550 kwa kilo.
Kushuka kwa bei hiyo,kumesababishwa na mavuno mapya ya maharage yanayowasili jijini kutoka mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Morogoro, Tanga na Kilimanjaro.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Kilimo na Chakula, Bw. Richard Kasuga, alisema kwa mujibu wa tangazo la Serikali mwisho wa muda wa punguzo la ushuru wa nafaka ni Aprili 23 mwaka huu.
Alisema msamaha huo ulikuwa wa miezi mitatu kuanzia Januari 23 mwaka huu.
Alisema hadi mwishoni mwa Aprili mwaka huu
tani 134,575 za mahindi zilikuwa zimeingizwa nchini, wakati mchele zilikuwa tani 27,388.
Alisema serikali ilipunguza ushuru kwa waagizaji wa vyakula kutoka nje ili wananchi waweze kununua chakula hicho kwa bei nafuu.
Tathmini iliyofanywa na Serikali katika mikoa 17, kati ya Januari 22 na Februari 2 mwaka huu, ilibainisha kuwa wananchi wapatao 3,764,543 wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula.
SOURCE: Nipashe