RAIS Jakaya Kikwete amesema serikali haitafanya biashara 'kichaa' ya kulipa madeni ya watu binafsi katika vyama vya ushirika kwa sababu biashara hiyo haina faida.
Amesema kuwa wakati wa kuwalinda wanaofilisi vyama vya ushirika umekwisha, na kwamba serikali haina nafasi hiyo tena.
Rais alikuwa akifanya majumuisho ya siku nzima juzi katika semina elekezi kwa wakuu wa mikoa, makatibu tawala na wakuu wa wilaya inayoendelea katika Hoteli ya Ngurdoto mkoani hapa. Alisema imefika wakati wananchi wajiulize ni kwa nini vyama vya ushirika vinakufa.
Alisema vyama hivyo ni vya wanachama na serikali haina mamlaka ya kuingilia uendeshaji wake. “Wenye vyama wanawachagua watu wao, wanaiba, kisha wanaiomba serikali iwasaidie, haiwezekani!
"Kama chama cha ushirika kimefilisika kwa viongozi kuiba fedha za ushirika, hatuwezi kuendelea kulindana, mwenyekiti aendelee kutajirika yeye tu huku umma unaendelea kufilisika, tunalindana eti mwenzetu, mwenzetu kwa lipi? Ni kuachana nao tu na kutafuta watu wengine,” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Rais Kikwete alibainisha kuwa, kwa vile vyama ambavyo vimo katika hatari ya kufilisiwa kwa mali zao kuuzwa, watafute fedha za kulipa kwani serikali haitaingilia kati kulipa madeni hayo na akasisitiza kuwa ifikie mahali ieleweke hivyo, kwamba serikali haitalipa.
Alionya kuwa kama wakulima ambao ndio wamiliki wa vyama vya ushirika hawatafanya juhudi za kuondokana na viongozi wabadhirifu, iko siku vyama vya ushirika vya akiba na mikopo (SACCOS) vitakuja kuchukua nafasi ya vyama vya ushirika vya msingi (Cooperatives).
Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Siasa na Mahusiano ya Kijamii, Kingunge Ngombale-Mwiru alisema uchumi wa kisasa utajengwa na watu wa kisasa na ndiyo maana Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeibuka na sera ya uwezeshaji wananchi.
Alisema inahitajika juhudi zaidi katika elimu ili kuwafanya wananchi wawe wa kisasa. “Watu wanahitaji kupata elimu ili wawe ‘modern’, utawezaje kujenga kilimo cha kisasa au viwanda kama watu wako hawana elimu? Mkazo uwe ni katika ‘ku-modernise’ elimu kwani bila hivyo tutabaki tunachezewa tu,” alisema.
Aliwataka wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na makatibu tawala wa mikoa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo inalenga kujenga msingi wa uchumi wa kisasa wa taifa linalojitegemea. “Vipaumbele vyenu viwe ni elimu na kilimo kama ambavyo Rais na Waziri Mkuu wanasisitiza kila mara,” alisema.
“Vipaumbele viwe ni elimu, elimu, elimu na hata ikibidi fufueni elimu ya watu wazima ili iwawezeshe kujishughulisha na mambo yao… iwasaidie kujifunza kilimo cha kisasa, ufugaji wa kisasa na uvuvi wa kisasa kulingana na maeneo walipo.”
Alisisitiza kuwa mageuzi ya kilimo ambayo serikali inataka kuyafanya, watekelezaji ni wananchi wa sasa, na sio watoto walioko shuleni, ndio maana anasisitiza ufufuliwaji wa elimu ya watu wazima.
“Ili kuleta mapinduzi ya kilimo, hakuna haja ya kusubiri trekta wakati katika wilaya yako hakuna hata plau, jaribuni kutumia vile mlivyo navyo kubadilisha hali ya sasa.”
Aliitaka serikali kuu itimize wajibu wake kwa kupeleka pembejeo katika muda muafaka na akawataka wakuu wa mikoa na wilaya watimize wajibu wao katika muda uliopangwa.
Mada zilizojadiliwa jana ni ‘Hali ya Uchumi wa Nchi’ iliyowasilishwa na Juma Reli, Naibu Gavana Benki Kuu; ‘Dira ya Maendeleo ya Taifa na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini’, iliyowasilishwa na Mkurugenzi Msaidizi, Mwakipesile; ‘Changamoto za Tatizo la Ajira na Mikakati ya Kukabiliana Nalo’, iliyowasilishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Kazi na Maendeleo ya Vijana, Dk. Ladislaus Komba; ‘Mkakati wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (MKURABITA)’, iliyowasilishwa na Ladislaus Salema.
Mada nyingine zilikuwa ni ‘Sera ya Uwezeshaji na Ubinafsishaji, iliyowasilishwa na Eliseta Kwayu, na ‘Nafasi za Mabaraza ya Biashara ya Mikoa katika Kukuza Uchumi wa Taifa’, iliyowasilishwa na Dan Mrutu.