RAIS Jakaya Kikwete ameziagiza mamlaka zinazohusika na masuala ya sheria kukaa na kuzipitia sheria na kanuni zinazohusu matumizi ya fedha katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kwa lengo la kuwabana wabadhirifu wa fedha za umma.
Alisema sheria zilizopo sasa zinawafanya watuhumiwa wa ubadhirifu hao katika Serikali Kuu na halmashauri kutuhumiwa kwa makosa ya kinidhamu zaidi badala ya kosa la jinai.
Rais aliyasema hayo juzi wakati akifunga majadiliano kwenye semina elekezi katika Hoteli ya Ngurdoto, Arumeru, mkoani Arusha.
Majadiliano hayo yalihusu mada zilizowasilishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, Ludovick Utoh; Nidhamu ya Matumizi ya Fedha iliyotolewa na Mhasibu Mkuu wa Serikali, Blandina Nyoni; na Taratibu za Manunuzi iliyotolewa na Mtendaji Mkuu Mamlaka ya Manunuzi, Dk. Ramadhani Mlinga.
“Haiwezekani kwa wabadhirifu wa fedha za umma, wakashitakiwa kuwa wamefanya kosa la kinidhamu ilhali walichofanya ni kosa la jinai.
“Tukae tuzungumze tu, mambo ambayo hayana maana tuondokane nayo,” alisema Rais.
Alisema kuwa udhaifu uliomo katika sheria hizo, unawafanya wakosaji kutopelekwa polisi pale wanapogundulika, badala yake hupelekwa kwenye kamati ili wakajadiliwe kwa kosa la kinidhamu.
Alisema haiwezekani wananchi wasio na hatia wakaendelea kuteseka, kwa kunyimwa fedha za maendeleo kwa kosa ambalo si lao.
“Mnakwenda mnakagua mahesabu, mnagundua kuna upotevu wa fedha za umma, hivi nyie hamna mamlaka ya kumkabidhi mtuhumiwa polisi?
“Badala ya kumpeleka polisi, nyie mnamrudisha kwenye kamati za halmashauri na kuwaambia eti ‘mjadilini nyie’. Namna hii hatuwezi kumaliza matatizo ya ubadhirifu wa fedha za umma,” alisema.
Akionyesha dhahiri kukerwa na hali hiyo, Rais alisema mwizi au mbadhirifu wa fedha za umma dawa yake ni kupelekwa polisi ambako kuna wataalamu watakaomchunguza na kama akipatikana na hatia, achukuliwe hatua za kisheria.
Alibainisha kwamba imekuwa kawaida sasa, mtuhumiwa wa ubadhirifu wa mamilioni ya fedha za umma na ambaye hupelekwa kwenye kamati za nidhamu ili akajadiliwe, huachiwa huru kutokana na mianya ya sheria hizo.
Aliongeza kuwa hali hiyo imezisababishia hasara kubwa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kwa kuendelea kupoteza mamilioni ya fedha za umma, huku wakosaji wakitamba mitaani.
“Hatuwezi kuendelea na utaratibu huu ambao hautatufikisha kokote. Kama ni suala la sheria, sheria hii haitusaidii kujenga nidhamu. Kosa la jinai lishughulikiwe kwa taratibu za kijinai,” alisisitiza.
Alisema zamani mhasibu alikuwa akitweta aliposikia kuwa wakaguzi wanakwenda kumkagua.
Alisema hali ni tofauti siku hizi, wahasibu hawatweti kwa kuwa wanajua kuwa kama watakutwa na hatia, watapelekwa kwenye kamati ya nidhamu ambako nako atajadiliwa na kusamehewa.
Alielezea pia kushangazwa kwake na mtuhumiwa wa wizi wa fedha za umma kupelekwa Taasisi ya Kuzuia Rushwa badala ya Polisi.
Alisema PCB wanashughulikia rushwa, na si wizi wa mali au pesa.
Rais alitaka pia kutafutwe muafaka wa kuangalia uhalali wa wilaya ambazo hazina wahasibu au wakurugenzi kunyimwa fedha za maendeleo.
Alitaka jambo hilo lifanyiwe kazi na kutapatiwa ufumbuzi, kwa kuwa wanaoteseka ni wananchi ambao hawahusiki na uteuzi wa wahasibu au wakurugenzi.
Akiwasilisha mada yake, pamoja na mambo mengine, Utoh alisema ni makosa kuwaadhibu wananchi kwa kutowapatia fedha za miradi ya maendeleo kwa makosa ambayo hawakuyafanya.
Alisema kuwa itakuwa vizuri ikiwa wahusika wa wizi wa fedha za umma watachukuliwa hatua za kisheria badala ya kuwatesa wananchi.