UONGOZI wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar umesema taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari nchini kwamba umekataa msaada wa mfanyabiashara Mohamed Raza, ni za uongo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya Ngurdoto mkoani hapa, Mkurugenzi wa Afya na Ustawi wa Jamii wa Hospitali hiyo, Dk. Juma Sadala, alisema kilichoelezwa na Raza hakina ukweli.
Alisema msaada wa Raza haukukataliwa, bali walitofautiana katika maudhui.
“Raza alitaka kutoa msaada wa magodoro na vitanda, hakuwasiliana na uongozi kufahamu nini hasa kipaumbele cha hospitali hiyo kwa sasa, ukweli unabaki pale pale kwamba hatukukataa msaada,” alisema Dk. Sadala.
Aliongeza: “Haiwezekani mtu akatoa msaada bila kutuuliza aina ya msaada tunaouhitaji.”
Alisema baada ya kumweleza hivyo, Raza alikwenda kwenye vyombo vya habari kulalamika.
Alitoa mfano kwamba kuna wakati mfanyabiashara huyo alitoa msaada wa glovu zikiwa pungufu ya ahadi aliyotoa.
Dk. Sadala alisema kwa sasa wanahitaji msaada wa kukarabati maabara na paa la Mnazi Mmoja. Kazi zote zinagharimu kiasi cha sh milioni 30.
Alisema wasingekubali vitanda kwa vile tayari vipo.
Kauli hii inagongana na iliyotolewa na Raza, akishutumu kukataliwa kwa msaada aliopanga kuipa Hospitali ya Mnazi Mmoja.