Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mabohora wafichua
Mabohora wafichua
By Habari Tanzania | Published  08/25/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu

MABILIONI ya shilingi yanadaiwa kuhamishwa nchini kila mwaka kupitia Kiongozi wa Madhehebu ya Bohora Duniani, Dk. Syedna Mohammed Burhanuddin.

Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima umebaini kuwa yapo malalamiko mengi kutoka kwa waumini wa madhehebu hayo ambao hawaridhishwi na michango wanayotoa, na baadaye kusafirishwa nje ya nchi.

Wanadai kwamba kuna usiri mkubwa mno kuhusu michango na fedha zinazokusanywa, kwani waumini wanaothubutu kuhoji, hufukuzwa na kutengwa kwenye jumuiya hiyo.

Wanadai kuwa fedha hizo zinapelekwa nje ya nchi bila kupitia utaratibu wa kibenki kwa kuwa kiongozi huyo ana hadhi ya mtu mashuhuri (VIP), hivyo hakaguliwi kama wanavyokaguliwa watu wengine wa kawaida.

Wiki iliyopita, kiongozi huyo aliwasili nchini na kupokewa na maelfu ya waumini na viongozi kadhaa wa serikali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Dar es Salaam.

Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabohora hapa nchini, Zainudin Adamjee, jana alisema kwamba waumini 6,000 walimpokea.

Duru za uchunguzi zinaonyesha kuwa, mwaka 1967, Serikali ya Awamu ya Kwanza, chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ilimfukuza nchini Dk. Burhanuddin, kutokana na haya anayofanya sasa.

“Ujio wa kiongozi huyo hapa nchini, badala ya kuleta faraja, ni kipindi kigumu mno kwa waumini, kwa sababu ni kipindi cha viongozi kukusanya michango ya mamilioni ya shilingi,” kimesema chanzo chetu.

Kuna uvumi kwamba safari hii, mchango wa kumuona kwa kila aliyetaka kufanya hivyo, ulikuwa ni dola 650 (sh 854,000). Kwa sasa dola moja ni wastani wa sh 1,300.

Watoto ambao ni wafuasi wa madhehebu hayo, walitakiwa kila mmoja alipiwe sh 100,000.

Mchango mkubwa kabisa ni wa dola 152,000 za Marekani (sh milioni 197) kutoka kwa kila aliyetaka kumkaribisha Dk. Burhanuddin, nyumbani kwake.

Kumkaribisha kiongozi huyo hakuna maana kwamba alale, au ale chakula; bali afike na kumaliza japo dakika tano tu na kutoa baraka kwa wenye nyumba.

Imeleezwa kwamba alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kila aliyetaka kwenda kumlaki uwanjani, na kupata baraka zake, alitakiwa alipe dola 1,000 (sh milioni 1.3).

Tofauti na siku zilizopita, ziara hii imemfikisha Dk. Burhanuddin, katika mbuga kadhaa za wanyama kaskazini mwa nchi.

Huko alikwenda mwanzoni mwa wiki kwa ajili ya shughuli ya uwindaji.

“Muumini aliyetaka kwenda huko alitakiwa atoe dola 3,000 (karibu sh milioni 4), bila kulipa kiasi hicho, hakuna kwenda,” kilisema chanzo chetu.

“Fedha hizi ni nyingi, na waumini waliojitokeza ni maelfu, wapo waliotoka Mombasa, Tanga, Arusha na sehemu nyingine ndani na nje ya nchi.

“Kumekusanywa mabilioni ya shilingi, lakini nakuhakikishia kuwa zote zinavushwa kwenda India.

“Tusingekuwa na ugomvi kama fedha hizi zingetumika hapa hapa nchini kujenga shule, hospitali na kadhalika,” kimesema chanzo chetu.

Inadaiwa kwamba ili kuhakikisha kwamba unakuwapo mtandao madhuibuti, madhehebu hayo yameweka utaratibu wa kuwa na viongozi mikoani ambao wote wanatolewa India.

Viongozi hao wanaitwa Amir Saheb; na wapo Dar es Salaam, Tanga, Moshi, Arusha, Zanzibar; Morogoro; na Mwanza ambako hawana Amir maalumu.

“Kwa kuwaleta viongozi hao kutoka India, inabidi waumini wakamuliwe fedha nyingi kwa ajili ya mishahara na mambo mengine; mbona wapo Watanzania hapa wenye elimu ya kutosha ambao wanaweza kuwa viongozi wazuri wa kiroho?” kimehoji chanzo chetu.

Pia wale wanaohoji michango na mambo mengine jinsi yanavyoendeshwa katika madhehebu hayo, wametengwa katika jumuiya.

Mwalimu Nyerere alimfukuza kiongozi huyo baada ya kubaini kuwa mabilioni ya shilingi yalikuwa yakivushwa nje ya nchi kwenda India, na hivyo kuiacha nchi ikiwa katika lindi kubwa la umasikini.

Adamjee anakiri kuwa ni kuwa ni kweli kiongozi huyo alifukuzwa, lakini aliruhusiwa tena kuingia nchini mwaka 1972.

Katika mtandao wa intaneti, kuna waumini kadhaa ambao wanamchukia Mwalimu, na kumweleza kama mwizi. Wanaeleza wazi chuki yao kwake baada ya kumpiga marufuku Dk. Burhanuddin, kuonekana nchini.

Burhanuddin ni kiongozi wa 52 wa madhehebu hayo ya Bohora.

Alizaliwa Machi 6, 1915 katika mji wa Surat, Gujarat, India. Akiwa na umri wa miaka 19, baba yake alimteua kuwa kiongozi wa baadaye wa madhehebu hayo.

Ukoo wake ni miongoni mwa koo tajiri kabisa katika India na duniani kwa jumla.

Adamjee alizungumza na Tanzania Daima jana kwa simu, na kukanusha madai yanayotolewa dhidi ya kiongozi huyo na madhehebu hayo kwa jumla.

Alisema maneno ya chuki na ya uongo yanaenezwa na watu wanaotaka kuvuruga amani na utulivu.

Adamjee alikanusha vikali kuwapo kwa michango ya lazima, akisema ni waumini wenyewe ambao huamua kuchanga fedha, tena kwa kiasi wanachotaka, kwa ajili ya mapokezi ya kiongozi wao.

Alisema hakuna fedha zinazotolewa kwa ajili ya kumuona, kumpeleka nyumbani, au kumpokea uwanjani.

“Haji kutafuta hela, ni tajiri, tena tajiri mkubwa, hapa (nchini) anakuja kutoa baraka kwa waumini wake, hakuna nyumba aliyotembelea, kama ipo nitajie.

“Waumini wanachanga kama waumini wengine wanavyochangia viongozi wao wanaokuja nchini.

“Yeye alikutana na Rais Jakaya Kikwete, akachanga dola 10,000 kwa ajili ya NGO ya Mama Kikwete.

“Sisi tuna SACCOS yetu, alituchangia dola 551,000 (zaidi ya sh milioni 700), kwa hiyo yanayosemwa dhidi ya kiongozi wetu ni uongo mkubwa,” alisema Adamjee.

Adamjee ambaye ni mmoja wa watu maarufu nchini, alisisitiza kuwa michango inayotolewa na waumini, inatolewa kwa ridhaa yao wenyewe bila kulazimishwa


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.