Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Bw Purnell Delly, amefunga mafunzo ya wiki mbili kwa polisi wa upelelezi, yanayolenga kupambana na ugaidi na uhalifu duniani.
Mafunzo hayo juu ya ufuatiliaji wa nyendo mbalimbali za magaidi na wahalifu yalihusisha askari polisi 15, wakiwemo maafisa wa vyeo vya juu na polisi wa kawaida wa Idara ya Upelelezi.
Mafunzo hayo yalianza Mei 8 mwaka huu na kumalizika jana na yaliendeshwa na wataalamu watano kutoka Marekani.
Sherehe fupi ya kufunga mafunzo hayo, ilifanyika katika Chuo cha Polisi Kurasini jijini Dar es Salaam juzi.
Mgeni rasmi katika sherehe hiyo, alikuwa Mkuu wa Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Rashid Hemed, ambaye pia alitoa vyeti kwa wahitimu hao.
Akihutubia, Bw Delly alisema Marekani imedhamiria kuboresha ushirikiano wake na Serikali ya Tanzania katika nyanja mbalimbali za maendeleo na kijamii.
Alisema mafunzo hayo yaliendeshwa na Serikali ya Marekani, chini ya mpango wake wa kulinda raia na kupambana na ugaidi duniani.
Alisema operesheni za kufuatilia nyendo mbalimbali za magaidi na wahalifu, zitaliwezesha Jeshi la Polisi kuanzisha kitengo maalum kitakachohusika na ulinzi wa viongozi wa juu serikalini, maafisa wa serikali, viongozi wa taasisi nyeti na viongozi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa.
Bw. Delly alisema Tanzania ilichaguliwa kama nchi ya mwanzo kupewa mafunzo hayo na Marekani kwa lengo kuwa programu hiyo, itaendelezwa katika nchi nyingine duniani.
Kwa upande wake, DCP Hemed aliishukuru Marekani kwa kusaidia kutoa kozi mbalimbali kwa askari wa Jeshi la Polisi wa vyeo na ngazi tofauti..
’Ukienda kila mkoa hapa Tanzania huwezi kukosa askari aliyepelekwa na Ubalozi wa Marekani nchini kwenda kuchukua mafunzo huko Marekani,’ alisema Hemed na kuongeza kuwa hata yeye ameshapelekwa mara mbili Marekani kuchukua mafunzo.
SOURCE: Nipashe