YULE Mbunge mashuhuri wa kulipua 'mabomu' Bungeni, Dakta Christant Majiyatanga Mzindakaya, siri yake imefichuka kwamba amezeekea Bungeni, kwani imeelezwa amekaa kwenye chombo hicho nyeti kwa miaka 40 sasa.
Hayo yamo kwenye taarifa ndefu kwa vyombo vya habari, iliyotolewa mjini hapa.
Taarifa hiyo ilikuwa ikitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali, yaliyojadiliwa kwenye Semina Elekezi kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya.
Semina hiyo kwa MaRC na DC, inaendelea katika hoteli ya kifahari ya Ngurdoto, kilometa 25 kutoka mjini hapa.
Taarifa hiyo imeeleza kwa urefu juu ya mada, iliyowasilisha kwenye semina hiyo na Dakta Mzindakaya, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kwela mkoa wa Rukwa.
Mada hiyo ni "Nafasi na Majukumu ya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Makatibu Tawala wa Mikoa katika Utendaji wa Serikali."
Katika mada hiyo Dakta Mzindakaya amewaeleza MaRC na DC hao, kuwa linapokuja suala la kuwaletea maendeleo wananchi, hakuna haleluya.
"Pambaneni na watu wanaowazuia kuwaletea wananchi maendeleo yao. Hakuna haleluya kwenye suala maendeleo," amesisitiza Dakta huyo, wakati akielezea uzoefu wake katika uongozi.
Akawakumbusha viongozi hao wakumbuke kuwa miaka mitano haipo mbali.
Ukurasa wa pili wa taarifa hiyo ndiyo uliompamba mno Dakta Mzindakaya, kwa kumweleza kuwa amewahi kuwa Mkuu wa Mkoa kwa miaka 13 na mikoa aliyowahi kuongoza ni Morogoro, Kigoma, Mbeya na Rukwa. Pia amewahi kuwa Naibu Waziri kwa miaka tisa na Mbunge kwa miaka 40. Ndiyo miaka arobaini taslimu akiwa Mheshimiwa!
Waandishi wa habari waligawiwa taarifa hiyo ya semina majira ya jioni kabisa, kutokana na kutoruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi wa semina.
Waandishi husubiri nje ya ukumbi kutwa nzima, ili kupewa briefing ya kinachojadiliwa ndani. Briefing hiyo hutolewa na maofisa wa serikali. Hata hivyo, waandishi waliruhusiwa kwenye ufunguzi.
Dakta Mzindakaya inasemekana aliingia Bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 1965.